Wednesday, September 23, 2015

JAMII YATAKIWA KUPAMBANA NA UTAPIAMLO IRINGA



Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Jamii imetakiwa kulipa uzito tatizo la utapiamlo ili kupunguza udumavu, ulemavu na vifo vya watoto na wanawake wanaonyonyesha.
Kauli hiyo imetolewa na mkuu wa mkoa wa Iringa, Amina Masenza alipokuwa akifungua mkutano wa kamati za lishe za halmashauri na mkoa wa Iringa  kuhusu masuala ya lishe ya mama na mtoto katika ukumbi wa Veta.
Masenza alisema “matatizo mbalimbali ya utapiamlo yanaendelea kudumaza, kulemaza na hata kuua watoto wetu na wanawake hasa wale wajawazito na wanaonyonyesha. Pia jamii kwa ujumla imekuwa ikiathirika kwa njia moja au nyingine kwa kuwepo kwa utapiamlo”. Masenza aliongeza “pamoja na maendeleo ambayo nchi yetu imeyapata katika maeneo mbalimbali, bado tatizo la lishe duni linaendelea kuathiri uchumi na kuchangia kuwepo kwa umasikini. Lishe duni pia huathiri ukuaji na maendeleo ya mtoto kimwili na kiakili hivyo kufifisha mchango wake katika maendeleo ya jamii na taifa”.
Alisema kuwa uboreshaji wa hali ya lishe nchini ni msingi wa afya njema, ubunifu, maendeleo mazuri ya kiuchumi na kupunguza umasikini kwa mtu mmoja mmoja na nchi kwa ujumla. Aliongeza kuwa kwa upande wa watoto lishe husaidia kuongeza uwezo wao kiakili na usanisi shuleni.
Mkurugenzi wa Mwanzo bora Dkt. Daniel Nyagawa alilitaja lengo kuu la mradi huo kuwa ni kuisaidia serikali katika kutekeleza mkakati wa taifa wa lishe pamoja na mkakati wa taifa wa kubadili tabia na mienendo ya maisha.
Aliongeza kuwa mradi wa lishe wa mwanzo bora unalenga kupunguza upungufu wa damu kwa wajawazito na wanawake wanaonyonyesha kwa asilimia 20. Aidha, unalenga kupunguza udumavu kwa watoto chini ya umri wa miaka miwili kwa asilimia 20. Mwisho mradi unalenga kujengea uwezo wa utekelezaji kwa serikali mashirika yasiyo ya kiserikali na kijamii.
Dkt. Nyagawa alisema kuwa mradi unatumia mkakati wa mawasiliano yanayolenga kubadili tabia katika masuala ya lishe. Alisema kuwa mradi unalenga tabia ambazo zikifuatwa zitaleta matokeo makubwa katika kupunguza udumavu na upungufu wa damu. Aliongeza mradi unalenga kubadilisha tabia binafsi ambazo zamani miradi mingi haikufanya.
Akiongelea walengwa wa mradi huo, Dkt. Nyagawa aliwataja “walio ndani ya siku 1,000 tangu kutungwa kwa mimba hadi mtoto anapofikisha umri wa miaka miwili”.Alifafanua kuwa ni mama mjamzito, anayenyonyesha na mama mwenye mtoto umri usiozidi miaka miwili. Baba ambaye mwenza au mke wake ana sifa zilizotangulia na wale wote wanaolea watoto wenye umri usiozidi miaka miwili.
Mradi wa lishe wa mwanzo bora ni mradi wa lishe uliofadhiliwa na serikali ya marekani kupitia USAID ukitekelezwa katika mikoa ya Iringa, Morogoro, Dodoma, Manyara na Mbeya.
=30=                                          

No comments:

Post a Comment