Wednesday, April 2, 2014

TUME KUCHUNGUZA CHANZO CHA MGOGORO WA ARDHI KISHAPO NA IGUNGA

Na Magdalena Nkulu,Ofisi ya Mkuu wa Mkoa- SHINYANGA
Tume ya watu 18 imeundwa kuchunguza chanzo cha mgogoro wa kugombea ardhi kati ya wakulima na wafugaji wa wilaya za Kishapu mkoani Shinyanga na Igunga mkoani Tabora kufuatia matukio ya mauaji ya watu watano na uharibifu wa makazi.

Hatua hiyo imeazimiwa na kikao cha kamati za ulinzi na usalama za mikoa ya Shinyanga na Tabora kilichofanyika jana katika kijiji cha Magogo ambako vurugu hizo zimetokea.
 
Wakitoa taarifa baada ya  kikao hicho, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Ally N. Rufunga na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Bi. Fatuma Mwasa wamesema pamoja na kuundwa tume hiyo kikao kimeazimia kuwa, wafugaji walioko katika kijiji cha Magalata wilayani Kishapu mkoa wa Shinyanga wabaki kwenye eneo lao na wasivuke mto Manonga kulisha ng'ombe wao..

Pia, wakulima walioko katika vijiji vya Magogo na Isakamaliwa wilaya ya Igunga mkoani Tabora wabaki huko na wasivuke mto Manonga.

Aidha,wakulima walioharibiwa makazi waendelee na shughuli zao kama kawaida katika vijiji vya Magogo na Isakamaliwa mkoani Tabora aidha,ulinzi wa wananchi wa vijiji vya Magogo na Isakamaliwa unaimarishwa, askari polisi wameongezwa ili kuhakikisha usalama wa eneo hilo

Kikao pia kimeazimia waharibifu wa makazi ya watu na  wauaji wakamatwe ndani ya siku saba.

Azimio lingine ni kamati zote mbili kutoa Elimu kwa wananchi wa vijiji vya Magalata wilaya ya Kishapu na Magogo na Isakamaliwa wilaya ya Igunga, vilevile Halmashauri zote mbili za Igunga na Kishapu zihakikishe zinaboresha sheria ndogo ili kuwaadhibu wanaokiuka utaratibu wa mipaka.

Kwa pamoja, Mhe.Rufunga na Mhe. Mwasa wamesema serikali imelaani vikali vitendo hivyo vilivyofanywa na wafugaji wa jamii ya Kitaturu na kusema ni vitendo visivyovumilika kwani siyo desturi ya Watanzania hivyo serikali imetoa salamu za pole kwa wafiwa na itahakikisha majeruhi mmoja anahudumiwa na pia watuhumiwa lazima wakamatwe.
=30=