Wednesday, September 22, 2010

Amani na Utulivu kazi ya matokeo ya CCM
Mgombea urais akumbusha amani na utulivu watanzania wanaojivunia leo hii ni matokeo ya sera nzuri za chama cha mapinduzi zisizolenga ubaguzi wa aina yoyote kwa raia wake imeelezwa.
Kauli hiyo imeelezwa na mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa tiketi ya chama cha mapinduzi (CCM) Jakaya Kikwete katika uwanja wa Samora mjini Iringa.
Kikwete amesema “sema nzuri za chama cha mapinduzi zisizobagua raia wake hali zao, rangi, dini, kabila, ndiyo misingi ya amani tuliyonayo”. Ameongeza kuwa CCM ni waaminifu na wakiahidi wanatekeleza na yote ya msingi waliyoahidi wameyatekeleza isipokuwa kidogo sana.


Mgombea urais wa CCM Jakaya Kikwete akiwa na Fredrick Mwakalebela katika uwanja wa Samora
Akizungumzia changamoto za elimu, mgombea urais wa CCM amesema serikali imejipanga kukabiliana na upungufu wa waalimu, maabara, vitabu na nyumba za walimu. Amesema kuwa serikali ya awamu ya nne imeamua kujenga chuo kikuu cha Dodoma na kitakapokamilika kitadahili wanafunzi 40,000 na kati yao 15,000 ni waalimu. Mkakati mwingine wa kuongeza waalimu ameutaja kuwa ni kuviomba vyuo binafsi kuongeza udahili wa wanafunzi wa fani ya ualimu nchini na pindi wanapohitimu serikali itawaajiri. Kikwete amesema kuwa kila shule ya sekondari itapata walimu wasiopungua watano. Mkakati mwingine katika elimu ameutaja kuwa ni kujenga uwezo wa ndani ili kuchapisha vitabu ndani ya nchi. Akizungumzia wafadhili wan je katika elimu amesema kuwa tayari Tanzania imepata vitabu 800,000 toka nchini Marekani na vingine 2,400,000 vipo njiani kufikia mwezi Februari, 2011.
Mgombea huyo urais kupitia tiketi ya CCM amesema lengo la serikali yake ni kuhakikisha kila mwanafunzi anakuwa na kitabu chake cha hisabati, phisikia, chemia na biolojia ifikapo mwaka 2011/ 2012.
Naye mgombea ubunge wa jimbo la Iringa Mjini kwa tiketi ya chama cha mapinduzi, Monica Ngenzi Mbega akielezea mafanikio ya serikali ya awamu ya nne katika utekelezaji wa Ilani ya CCM amesema kuwa wakazi wa Manispaa ya Iringa wananufaika na mtandao wa maji kwa asilimia 95 mwaka 2010 ukilinganisha na asilimia 72 mwaka 2005.
Kwa upande wa elimu Mbega amesema kuwa shule za sekondari zimeongezwa kutoka shule 5 (2005) hadi shule 13 (2010) sambamba na wanafunzi wanaomaliza kutoka 930(2005) hadi 14,970 (2010).
Uwanja wa Samora ulirindima kwa shangwe pale alipopanda jukwaani aliyekuwa mshindi katika kura za maoni kupitia chama cha mapinduzi na kuenguliwa Fredrick Mwakalebela alipopanda jukwaani na kutangaza rasmi kuvunja kundi lake na kutangaza kumuunga mkono mgombea ubunge wa jimbo la Iringa Mjini, Monica Mbega “kwa sasa naelekeza nguvu zote kwa Monica Mbega kama mgombea ubunge, madiwani wote na mgombea urais wa CCM”. Mwakalebela alichukua nafasi hiyo kuwaasa wanasiasa waotumia jina lake jukwaani kumsikitikia na kusema waache mara moja na wasimtumie kama sera yao.
Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano kupitia chama cha mapinduzi yupo mkoani Iringa katika ziara ya siku nne ya kampeni za urais, ubunge na udiwani.