Thursday, December 30, 2010

...Bibi Mpaka awapongeza walimu wa shule ya Msingi Ikonda

Walimu wa shule ya msingi Ikonda wamepongezwa kwa kuwafundisha na kufaulu mtihani wa darasa la saba mapacha walioungana kwa moyo wa huruma, upendo na kujituma.

Pongezi hizo zimetolewa na Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Bibi Gertrude Mpaka jana katika hafla fupi ya kuwapongeza na kuwapa zawadi mapacha walioungana Maria Mwakikuti na Consolata Mwakikuti baada ya kufaulu mtihani wa darasa la saba iliyofanyika katika ukumbi wa hospitali ya Consolata iliyopo katika kijiji cha Ikonda wilayani Makete.
 Mkuu wa Wilaya ya Makete, Bibi. Zainabu Kwikwega, Katibu Tawala Mkoa wa Iringa,
Bibi Gertrude Mpaka na Dr. Allesandro Nava

Katibu Tawala wa Mkoa wa Iringa amesema “nawapongeza sana walimu wa shule ya msingi Ikonda kwa kuwafundisha watoto hawa kwa moyo wa huruma, upendo na kujituma hadi kuhakikisha wanafaulu vizuri mtihani wao wa darasa la saba”. Kufaulu vizuri kwa mapacha hawa ni mchanganyiko wa juhudi za ufundishaji makini wa walimu na jitihada zao wenyewe za kujisomea kwa bidii. Ameongeza kuwa kufaulu vizuri pia kumetokana na ushirikiano wa wanafunzi wenzao kwa kuwaonesha upendo na kuwachangamsha na hatimae kujiona ni sehemu ya jamii inayowazunguka.

Bibi Mpaka ambaye pia ni mwenyekiti wa Kamati ya uchaguzi wa wanafunzi waliofauli ya Mkoa wa Iringa amesema kuwa “nimekuja hapa kuwapongeza kwa kufaulu vizuri katika mtihani wenu wa darasa la saba na kuwapa zawadi”. Aidha alitoa wito kwa jamii kuwasaidia mapacha hao ili wasione kama jamii imewapa kisogo. Amewataka Maria na Consolata kusoma kwa bidii zaidi na kuongeza maarifa ili kulitumikia taifa katika kuliletea maendeleo.

 Bibi Gertrude Mpaka, Katibu Tawala Mkoa wa Iringa akikabidhi
zawadi za vitabu vya sekondari kwa Consolata na Maria

Afisa Elimu Taaluma Mkoa wa Iringa, Mwl. Leonard Msigwa akiwa katika picha ya pamoja na
Consolata na Maria mara baada ya kukabidhi zawadi za Mkoa

Mapacha hao kwa pamoja wanamatarajio ya kusomea sayansi ya kompyuta. Aidha walisema kuwa wanaridhika sana na jamii jinsi inavyowachukulia na kutoa wito kwa viongozi wengine kuwa wanakwenda kuwatembelea.

Mkuu wa Hospitali ya Consolata- Ikonda walipozaliwa mapacha hao na muangalizi wao Padre Dr. Allesandro Nava amesema kuwa “sikushangaa kwa kufaulu kwao sababu ni wajanja sana”.

Mapacha hao walioungana walizaliwa Disemba 1997 na wamefaulu mtihani wa darasa la saba kwa alama 151 kila mmoja lakini katika masomo tofauti tofauti na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi imewapangia kujiunga na kidato cha kwanza katika shule ya sekondari ya wasichana ya Jangwani iliyopo Dar es Salaam.



Cheers