Serikali Mkoani Iringa imeahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa vyombo vya habari vya Mkoani hapa na nje ya Mkoa ili kuhakikisha uhuru wa upatikanaji habari unashamiri na wananchi wanapata habari zinazohusu maendeleo yao .
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk. Christine Ishengoma akizundua gazeti la Kwanza Jamii-Iringa
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk. Christine Ishengoma akiongea na mmoja wa wajumbe wa bodi wa gazeti la Kwanza Jamii Maggid Mjengwa
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk. Christine Ishengoma wakati akizindua gazeti la Kwanza Jamii-Iringa katika sherehe za uzinduzi zilizofanyika katika uwanja wa shule ya sekondari Mwembetogwa katika Manispaa ya Iringa.
Dk. Ishengoma amesema “ieleweke kuwa serikali imekuwa na ushirikiano mkubwa na mzuri na vyombo vya habari, mara nyingi Mhe. Rais amehimiza ushirikiano huo kwa watendaji wengine, huku akiwataka wananchi kuvitumia vyombo hivyo kwa manufaa ya taifa”.
Aidha, amewataka wananchi wa Mkoa wa Iringa kujitokeza na kutoa ushirikiano wao kwa gazeti hilo kwa manufaa ya maendeleo ya Mkoa wa Iringa. Amewataka kuwa wadau kwa kununua nakala na kutoa matangazo yao ili kulifanya gazeti hilo kuwa endelevu.
Mkuu wa Mkoa amewataka wananchi wa Mkoa wa Iringa, kulitumia gazeti hilo kama jukwaa la kusemea na kuwaunganisha na viongozi wao kwa manufaa ya maendeleo ya wana Iringa.