Wednesday, November 2, 2011

WALIMU WATOE DARASA LA VVU/UKIMWI

Walimu Mkoani Iringa wameshauriwa kutumia muda wao kuzungumzia masuala ya VVU/UKIMWI na madhala yake katika jamii pindi wanapokuwa wakifundisha katika utaratibu wao wa kawaida ili kuongeza uelewa kwa wanafunzi.

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk. Christine Ishengoma

Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk. Christine Ishengoma alipokuwa akiongea na waandishi wa habari wa Mkoa wa Iringa ofisini kwake katika utaratibu wake wa kawaida wa kukutana na waandishi wa habari mara kwa mara na kujadili masuala ya maendeleo na changamoto katika Mkoa.

Dk. Ishengoma amesema “ukimwi ni tatizo sana katika Mkoa wetu wa Iringa hivyo hata kama haupo katika mitala ya elimu lakini ni vizuri kila mwalimu akachukua angalau dakika tano anapoanza au anapomaliza kipindi kuelezea masuala ya UKIMWI”.

Amesema katika kukabiliana na janga hili ni lazima elimu itolewe kwa umakini mkubwa kuanzia darasa la tatu na kuendelea kwa misingi ya kuwaandaa vijana na mapambano hayo.

Akiongelea dawa ya kudumu dhidi ya UKIMWI amesema ipo wazi nayo ni wananchi kubadili tabia sambamba na elimu dhidi ya kujikinga na maambukizi. Amesema kwa wale waaminio basi watumie maandiko matakatifu kama kinga na wale wasioweza kabisa basi zana zitumike, “ila dawa ni wewe mwenyewe kubadili tabia”.

Mkuu wa Mkoa huyo aliwaagiza waandishi wa habari kujikita katika kuandika habari na makala zinazoelezea madhara ya UKIMWI katika jamii ili kuweza kueneza habari hizo na hatimae kuifikishia jamii taarifa sahihi ili kuweza kuinusuru na kuongeza nguvu kazi katika Mkoa na Taifa.  

No comments:

Post a Comment