VIJANA mkoani Iringa wametakiwa kuwa wajumbe makini katika kupunguza kasi ya maambukizi ya virusi vya UKIMWI na kujilinda kwa kutumia mafundisho ya MUNGU kama silaha kubwa katika kujilinda na ugonjwa huo.
Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk. Christine Ishengoma wakati akifunga semina ya siku mbili ya vijana iliyoandaliwa na Kanisa Katoliki Parokia ya Kihesa katika manispaa ya Iringa.
Dk. Ishengoma amesema “mkoa wetu sasa unaongoza kwa maambukizi ya UKIMWI ukiwa na kiasi cha asilimia 15.7 ya maambukizi”. “Naomba kila mmoja wetu awe mjumbe katika kupunguza kasi ya maambukizi haya”. Amesema kwa kufanya hivyo kiasi cha maambukizi kitapungua sana . Aidha, amewasisitiza vijana kujilinda kwa kufuata mafundisho ya Mungu kama silaha kubwa katika kujilinda huko. Akikariri Kitabu cha Waefeso 6:11 “vaeni silaha zote za Mungu mpate kuweza kuzipinga hila za shetani”.
Vilevile, amewaasa vijana wote kujenga tabia ya kushiriki kikamilifu katika michezo mbalimbali kwa malengo ya kuimarisha afya zao, uwezo wa kufikiri na kujipatia ajira.
Amewaomba walimu na viongozi wa dini kuhakikisha vijana wanafanikiwa. Amesema “walimu wa mafundisho ya dini ni nguzo muhimu katika kuhakikisha vijana wanafanikiwa, nawaomba walimu wote na viongozi mbalimbali wa taasisi za dini tutumie nguvu zetu zote kuwapa elimu vijana wetu” alisisitiza Mkuu wa Mkoa wa Iringa.
Ameshauri kuwa vijana ni taifa linalotegemewa hivyo kwa kutumia karama ya ualimu. Ni vizuri wakatumia tunu hiyo kuufikisha ujumbe wa Mungu kwa vijana na waumini wote. Ameshauri kuendelea kuwafundisha maadili mema ili wafanikiwe katika maisha. Amesema kuwa wapo vijana wakorofi ambao huchangia pia kuharibu nidhamu ya vijana wengine hao wanahitaji mtumie bisara na utu zaidi ili warudi katika nidhamu inayotakiwa.
Akiongelea suala la anami iliyopo nchini, Dk. Ishengoma amesema “niwakumbushe suala la amani iliyopo nchini kwa sasa”. Watanzania siku zote tunaishi kwa amani na mshikamano mkubwa. Amesema “hivi vyote vimejengwa na waasisi wetu ambao walituunganisha tukawa kitu kimoja”. Amesisitiza kuwa wote kwa pamoja kuimarisha na kudumisha zaidi mshikamano na amani iliyopo ili watanzania waendelee kuishi kwa utulivu na upendo.
Katika mmomonyoko wa maadili, Dk. Ishengoma amesema “katika jamii yetu wote tumeshuhudia mmomonyoko wa maadili, tumeshuhudia vijana wakilewa, wakikosa hekima na busara, dharau, vijana kuvuta na kusafirisha dawa za kulevya”. Amesema mmomonyoko huu unatokana na kutofuata mafundisho ya Mungu. Aidha, aliuomba uongozi wa kanisa kusaidia kwa kadri iwezekanavyo kuwafundisha maadili mema vijana na waumini wao kwa ujumla.
Kanisa Katoliki Parokia ya Kihesa kupitia umoja wa vijana umeandaa semina kwa vijana kwa lengo la kuwaimarisha kimwili na kiroho pamoja na kuwapokea vijana waliohitimu shule ya msingi na kujiunga na umoja huo ili kuweza kuepukana na majanga mbalimbali yanayowakumba vijana kulingana na hali halisi ya utandawazi.
No comments:
Post a Comment