Na
Mwandishi Maalum, IRINGA
Kamati
ya maandalizi ya maonesho ya utalii ya karibu kusini na shughuli za viwanda
vidogo (SIDO) kanda ya nyanda za juu kusini imetakiwa kuhakikisha wanyamapori
hai wanakuwepo katika maonesho hayo.
Kauli
hiyo ilitolewa na mkuu wa mkoa wa Iringa, Amina Masenza alipokuwa akiendesha
kikao cha tatu cha maandalizi ya maonesho ya Utalii Karibu Kusini na shughuli
za viwanda vidogo (SIDO) kanda ya nyanda z juu kusini kilichofanyika katika
ukumbi wa mikutano wa Veta mjini Iringa.
Masenza
alisema kuwa wanyamapori hai ni muhimu katika maonesho hayo kwa sababu wananchi
wengi wanapenda kuwaona wanyamapori hai moja kwa moja. Aidha, alishauri kasi ya
kufuatilia wanyamapori hao inayofanywa baina ya kamati ya maandalizi na wizara
ya Maliasili na Utalii iongezwe.
Katika
taarifa ya kamati ya maandalizi iliyowasilishwa na Fikira Kisimba alisema kuwa
ufuatiliaji unaendelea kufanyika kwa kushirikiana na wizara ya Maliasili na
Utalii kwa lengo la kupata wanyama hao. “Wizara
imetoa bajeti elekezi ambapo mikoa inawajibika kuchangia jumla ya shilingi 4,000,000
kukodi mabanda yote manne ya wanyama” alisema Kisimba.
Akiongelea
wadau waliothibitisha kushiriki katika maonesho hayo, alisema kuwa wadau 312
wamethibitisha kushiriki. Aliwataja baadhi ya wadau hao kuwa ni wizara ya
Maliasili na Utalii; wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezeji; wizara ya
Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo; na TATO. Wengine ni KILI FAIR; Wakala wa
Misitu Tanzania; Ngonga beach; UPL Link Mbeya; Uyole cultural Enterprises;
Baraza la Biashara la Taifa; Heifer International; Care International na
Wajasiliamali 300.
=30=