Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa - IRINGA
Sekta ya kilimo ni muhimili wa uchumi
nchini pamoja na kukabiliwa na changamoto nyingi katika ukuaji wake hasa upatikanaji mikopo.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Mkoa
wa Iringa, Amina Masenza wakati wa utiaji saini makubaliano ya mikopo kati ya Benki
ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania na wakulima wadogo wadogo wa mkoa wa Iringa
katika kijiji cha Igomaa wilayani Mufindi.
Masenza alisema “ikumbukwe kuwa umuhimu wa sekta ya kilimo unachagizwa na ukweli kuwa ni
sekta ambayo inaajiri zaidi ya asilimia 75 ya wananchi wanaoishi vijijini,
ambao wanategemea kilimo, ufugaji na uvuvi kwa ajili ya maisha yao. Kadhalika,
wakulima, wafugaji na wavuvi wanatumia zana na mbinu duni katika shughuli zao,
hivyo kushindwa kupata matokeo mazuri ya mazao”. Aliongeza kuwa pamoja na
mchango mkubwa wa wakulima kwenye ukuaji wa uchumi wa nchi, kwa mujibu wa
takwimu zilizopo kuhusu hali za maisha ya wakulima nchini siyo ya kuvutia hata
kidogo. Wengi mapato yao yapo chini na wanaishi maisha duni sana.
Lengo la serikali ya awamu ya tano ni
kuimarisha sekta ya kilimo ili iweze kutoa mchango mkubwa zaidi katika uchumi
wa nchi na kuwanufaisha wakulima, wafugaji na wavuvi katika kuyabadilisha
maisha yao kwa kupitia mikopo na
pembejeo za kisasa na mbegu bora zaidi. “Naamini
ujio wa benki ya maendeleo ya kilimo (TADB) ni mwanzo tu wa maandalizi ya
matokeo halisi ya ndoto na matamanio ya rais wetu, hivyo sina budi kuwapongeza
na kuwaunga mkono katika hatua zote mnazozifanya katika kuwakopesha wakulima
wadogo wadogo” alisisitiza Mkuu wa Mkoa wa Iringa.
Akiongelea changamoto iliyopo katika
upatikanaji wa mikopo kwa ajili ya kilimo katika taasisi za kifedha, Mkuu wa Mkoa
wa Iringa, alisema kuwa upatikanaji wa fedha ni mgumu kutokana na mikopo mingi
kuelekezwa katika biashara za bidhaa na riba kubwa kwenye mikopo ya kilimo. Aliongeza
kuwa masharti ya dhamana ni kikwazo kikubwa kwa wakulima wadogo wengi. Alisema kuwa
kuanzishwa kwa Benki ya Maendeleo ya Kilimo ni fursa kubwa kwa wakulima nchini.
=30=