Sunday, September 15, 2013

SERIKALI NA SPANEST KUSHIRIKIANA KUBORESHA HUDUMA KWA WATALII




Serikali imeahidi kuendelea kushirikiana na mradi wa kuboresha mtandao wa maeneo yaliyohifadhiwa kusini mwa Tanzania (SPANEST) katika kuboresha huduma kwa watalii na wageni wanaotembelea nyanda za juu kusini.


Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk. Christine Ishengoma aliyesimama akisoma hotuba ya kufunga mafunzo ya mbinu za kuboresha utoaji huduma kwa wateja mahala pa kazi kwa watumishi wa TANAPA kutoka hifadhi za kusini. Kushoto  ni mratibu wa mradi wa SPANEST, Godwell ole Maing'ataki na kulia ni Afisa Utalii wa TANAPA, Risala Kabongo. 


Kauli ya serikali imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa Dkt. Christine Ishengoma alipokuwa akifunga mafunzo juu ya mbinu za kuboresha utoaji wa huduma kwa wateja mahala pa kazi kwa watumishi wa TANAPA kutoka hifadhi za kusini yaliyofanyika katika ukumbi wa Neema Craft Manispaa ya Iringa.

Dkt. Christine amesema “serikali itaendelea kuunga mkono jitihada zinazofanywa na SPANEST na Wadau wengine wa utalii katika kuhakikisha kuwa huduma kwa wageni wanaotembelea Nyanda za Juu Kusini zinaboreshwa, ili kuwafanya wageni  kufurahia safari zao na kufikia matarajio yao ili kuwa  mabalozi wazuri wa kutangaza vivutio vyetu”. Aidha, alishukuru juhudi za kukabiliana na huduma duni zinazotolewa kwa wageni katika mikoa ya nyanda za juu kusini, alisema “tunashukuru na kupongeza jitihada za SPANEST kukabiliana na changamoto ya huduma duni kwa wageni wanaotembelea mikoa ya nyanda za juu Kusini kupitia mafunzo kama haya”.

Alisema Dkt. Christine. Alitoa wito kwa Mratibu wa mradi wa SPANEST kuendelea kushirikiana na wadau wengine katika mkoa wa Iringa na mikoa mingine kuandaa mafunzo kama hayo kwa watumishi ambao wanatoa huduma kwa wageni kwa kuzingatia umuhimu na upana wa sekta ya utalii ambayo ina wadau wengi wa ndani na nje. Amesema kuwa watalii wanaotembelea hifadhi za Taifa pia hutembelea vivutio na  maeneo yaliyopo nje ya hifadhi hivyo huduma bora zinahitajika kuboreshwa katika hifadhi na maeneo yote nje ya hifadhi.

Akiongelea mantiki ya mafunzo hayo kwa washiriki wa mafunzo hayo, Mkuu wa mkoa alisema “kwa washiriki wote wa mafunzo haya kutoka hifadhi za nyanda za juu kusini chini ya TANAPA, nawapongeza na kuwataka kuonyesha kwa vitendo yale yote ambayo mmejifunza kwa kipindi cha siku nne za mafunzo”. Amesema kuwa anategemea kuwa washiriki hao watakuwa mfano bora katika utoaji wa huduma katika maeneo yao ya kazi na kuwa waalimu kwa wale ambao hawakupata nafasi ya kushiriki katika mafunzo hayo.

Mkuu wa Mkoa wa Iringa amesema kuwa mikoa ya nyanda za juu kusini ina sifa ya kuwa na hifadhi zenye maliasili za kipekee zisizopatikana katika maeneo mengine nchini. Amezitaja hifadhi hizo kuwa ni ruaha ambayo ni hifadhi kubwa kuliko zote nchini, kitulo ambayo ni bustani ya maua ya asili isiyopatikana popote duniani, katavi yenye viboko na mamba wengi, udzungwa yenye misitu na maporomoko ya maji yanayofikia urefu wa mita 170. Hifadhi nyingine amezitaja kuwa ni mikumi na mapori ya akiba ya mpanga kipengere, rungwe-kizigo na hifadhi za jamii zinazosimamiwa na wananchi pamoja na maeneo ya historian a kitamaduni.

Akitoa maelezo ya mafunzo hayo, mratibu wa mradi wa kuboresha mtandao wa maeneo yaliyohifadhiwa kusini mwa Tanzania (SPANEST), Godwell Meing’ataki amesema kuwa tatizo la uduni wa huduma zisizo za viwango kwa wageni wanaotembelea mikoa ya Kusini limekuwa kubwa hasa katika maeneo yanayopokea na kutoa huduma kwa wageni. Ameyataja maeneo yenye changamoto kubwa kuwa ni mapokezi, malazi, chakula, mawasiliano, utoaji taarifa na usafirishaji.

Meing’ataki amesema kuwa mafunzo hayo yamejikita katika maeneo ya kutoa huduma bora, namna ya kufanya mawasiliano, mbinu za kuboresha masoko, kujenga mahusiano, maadili na taratibu za kuboresha huduma.

Mafunzo ya mbinu za kuboresha utoaji wa huduma kwa wateja mahala pa kazi kwa watumishi wa TANAPA kutoka hifadhi za kusini yameandaliwa na mradi wa kuboresha mtandao wa maeneo yaliyohifadhiwa kusini mwa Tanzania (SPANEST). 

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk. Christine Ishengoma (wapili kushoto waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa mafunzo ya mbinu za kuboresha utoaji huduma kwa wateja mahala pa kazi kwa watumishi wa TANAPA kutoka hifadhi za kusini. 
=30=