Serikali
imeahidi kuendelea kushirikiana na mradi wa kuboresha mtandao wa maeneo
yaliyohifadhiwa kusini mwa Tanzania (SPANEST) katika kuboresha huduma kwa
watalii na wageni wanaotembelea nyanda za juu kusini.
Mkuu
wa Mkoa wa Iringa, Dk. Christine Ishengoma aliyesimama akisoma hotuba ya
kufunga mafunzo ya mbinu za kuboresha utoaji huduma kwa wateja mahala pa kazi
kwa watumishi wa TANAPA kutoka hifadhi za kusini. Kushoto ni mratibu wa mradi wa SPANEST, Godwell ole Maing'ataki na kulia ni Afisa Utalii wa TANAPA, Risala
Kabongo.
Kauli
ya serikali imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa Dkt. Christine Ishengoma
alipokuwa akifunga mafunzo juu ya mbinu za kuboresha utoaji wa huduma kwa
wateja mahala pa kazi kwa watumishi wa TANAPA kutoka hifadhi za kusini
yaliyofanyika katika ukumbi wa Neema Craft Manispaa ya Iringa.
Dkt.
Christine amesema “serikali itaendelea kuunga mkono jitihada zinazofanywa na
SPANEST na Wadau wengine wa utalii katika kuhakikisha kuwa huduma kwa wageni
wanaotembelea Nyanda za Juu Kusini zinaboreshwa, ili kuwafanya wageni kufurahia safari zao na kufikia matarajio yao
ili kuwa mabalozi wazuri wa kutangaza
vivutio vyetu”. Aidha, alishukuru juhudi za kukabiliana na huduma duni
zinazotolewa kwa wageni katika mikoa ya nyanda za juu kusini, alisema
“tunashukuru na kupongeza jitihada za SPANEST kukabiliana na changamoto ya
huduma duni kwa wageni wanaotembelea mikoa ya nyanda za juu Kusini kupitia
mafunzo kama haya”.
Alisema
Dkt. Christine. Alitoa wito kwa Mratibu wa mradi wa SPANEST kuendelea kushirikiana
na wadau wengine katika mkoa wa Iringa na mikoa mingine kuandaa mafunzo kama
hayo kwa watumishi ambao wanatoa huduma kwa wageni kwa kuzingatia umuhimu na
upana wa sekta ya utalii ambayo ina wadau wengi wa ndani na nje. Amesema kuwa watalii
wanaotembelea hifadhi za Taifa pia hutembelea vivutio na maeneo yaliyopo nje ya hifadhi hivyo huduma
bora zinahitajika kuboreshwa katika hifadhi na maeneo yote nje ya hifadhi.
Akiongelea
mantiki ya mafunzo hayo kwa washiriki wa mafunzo hayo, Mkuu wa mkoa alisema “kwa
washiriki wote wa mafunzo haya kutoka hifadhi za nyanda za juu kusini chini ya
TANAPA, nawapongeza na kuwataka kuonyesha kwa vitendo yale yote ambayo
mmejifunza kwa kipindi cha siku nne za mafunzo”. Amesema kuwa anategemea kuwa washiriki
hao watakuwa mfano bora katika utoaji wa huduma katika maeneo yao ya kazi na
kuwa waalimu kwa wale ambao hawakupata nafasi ya kushiriki katika mafunzo hayo.
Mkuu
wa Mkoa wa Iringa amesema kuwa mikoa ya nyanda za juu kusini ina sifa ya kuwa
na hifadhi zenye maliasili za kipekee zisizopatikana katika maeneo mengine
nchini. Amezitaja hifadhi hizo kuwa ni ruaha ambayo ni hifadhi kubwa kuliko
zote nchini, kitulo ambayo ni bustani ya maua ya asili isiyopatikana popote
duniani, katavi yenye viboko na mamba wengi, udzungwa yenye misitu na
maporomoko ya maji yanayofikia urefu wa mita 170. Hifadhi nyingine amezitaja
kuwa ni mikumi na mapori ya akiba ya mpanga kipengere, rungwe-kizigo na hifadhi
za jamii zinazosimamiwa na wananchi pamoja na maeneo ya historian a kitamaduni.
Akitoa
maelezo ya mafunzo hayo, mratibu wa mradi wa kuboresha mtandao wa maeneo
yaliyohifadhiwa kusini mwa Tanzania (SPANEST), Godwell Meing’ataki amesema kuwa
tatizo la uduni wa huduma zisizo za viwango kwa wageni wanaotembelea mikoa ya
Kusini limekuwa kubwa hasa katika maeneo yanayopokea na kutoa huduma kwa wageni.
Ameyataja maeneo yenye changamoto kubwa kuwa ni mapokezi, malazi, chakula,
mawasiliano, utoaji taarifa na usafirishaji.
Meing’ataki
amesema kuwa mafunzo hayo yamejikita katika maeneo ya kutoa huduma bora, namna
ya kufanya mawasiliano, mbinu za kuboresha masoko, kujenga mahusiano, maadili
na taratibu za kuboresha huduma.
Mafunzo
ya mbinu za kuboresha utoaji wa huduma kwa wateja mahala pa kazi kwa watumishi wa
TANAPA kutoka hifadhi za kusini yameandaliwa na mradi wa kuboresha mtandao wa
maeneo yaliyohifadhiwa kusini mwa Tanzania (SPANEST).
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk. Christine Ishengoma
(wapili kushoto waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa mafunzo
ya mbinu za kuboresha utoaji huduma kwa wateja mahala pa kazi kwa watumishi wa
TANAPA kutoka hifadhi za kusini.
=30=
No comments:
Post a Comment