Serikali imemuongezea muda wa miezi
sita mkandarasi anayejenga barabara ya Iringa-Migori ili aweze kukamilisha
ujenzi huo na kukabidhi barabara hiyo serikalini.
Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli (kushoto) na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk. Christine Ishengoma (kulia)
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa
Ujenzi, Dk. John Magufuli alipokuwa akifanya majumuisho ya ziara yake ya
kukagua mradi wa barabara ya Iringa-Dodoma katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi
ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa.
Dk. Magufuli amesema kuwa Mkandarasi China
Sichuan International Cooperation Company Limited (SIETCO) anayejenga barabara
ya Iringa-Dodoma sehemu ya kwanza Iringa- Migori (km. 95.2) yupo nyuma, hivyo
serikali imemuongezea miezi sita.
Amesema kuwa baada ya kuongeza miezi hiyo
mkandarasi huyo atatakiwa kukabidhi barabara hiyo kwa serikali mwezi Septemba,
2014. Akiongelea sababu zilizomfanya mkandarasi huyo awe nyuma, Dk. Magufuli
amesema kuwa eneo la Nyang’oro lilikuwa na milima mikali na kuhitajika nguvu
zaidi katika kuikata kwa ajili ya ujenzi wa barabara. Amesema baada ya kipindi
hicho mkandarasi lazima akabidhi barabara na hakuna muda wa ziada
utakaoongezwa.
Kutokana na umuhimu wa kimkakati wa
barabara ya Iringa- Dodoma yenye urefu wa km 260 utakapokamilika, Waziri wa
Ujenzi ameshauri uandaliwe mpango wa kutengeneza barabara za michepuo. Amesema
kuwa umuhimu wa barabara hizo za michepuo ambazo zitakuwa haziingii katikati ya
mji zitaondoa msongamano wa magari katikati ya mji. Aidha, ameshauri
itengenezwe stendi kubwa ya magari nje ya mji ili kupunguza msongamano wa
magari mjini.
Mkuu wa Mkoa wa Mkoa wa Iringa, Dk. Christine
Ishengoma ameishukuru serikali ya awamu ya nne chini ya uongozi wa Rais, Dk.
Jakaya Kikwete kwa kuweka nguvu katika ujenzi wa miundombinu ya barabara nchini
hasa mkoani Iringa. Amesema kuwa Mkoa wa Iringa utaendela kusimamia barabara
zote ili ziweze kudumu kwa muda mrefu. Amesema kuwa serikali kupitia wizara ya
Ujenzi inafanya kazi nzuri na wale wasiyoiona basi hawana macho alisisitiza Dk.
Christine.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk. Christine Ishengoma (kulia) akitoa shukrani. Kushoto ni Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli
Mkuu wa Mkoa wa Iringa alitumia majumuisho
hayo kumuomba Waziri wa Ujenzi kuiangalia kwa jicho la pekee barabara kuu ya
TANZAM sehemu ya mlima Kitonga ipanuliwe ili kuondoa ajali za mara kwa mara na
hadha kwa watumiaji wa barabara hiyo. Waziri Dk. Magufuli alilipokea ombi hilo
na kuahidi kulitafitia ufumbuzi.
Mkataba wa ujenzi wa mradi wa
barabara ya Iringa-Migori (km. 95.2) ulisainiwa tarehe 13 Januari, 2011 kati ya
Tanroads na Mkandarasi China Sichuan International Cooperation Company Limited
(SIETCO) kwa gharama ya shilingi 84.216 bilioni kwa utekelezaji wa miezi 35.
=30=
No comments:
Post a Comment