RAIS Jakaya Kikwete amesema Mwaka
2014 ni mwaka maalumu na wa aina yake katika historia ya Tanzania kwa kuwa
utakuwa na mambo makubwa matatu yatakayofanywa.
Jambo kubwa alililosisitiza ni
mchakato wa Katiba Mpya ambao alisema ni lazima ukamileke mwakani kama mambo
yatakwenda sawa sawa.
Rais Dk. Jakaya Kikwete akihutubia umma wa wananchi
Akiyataja mambo mengine alisema
“Tutasheherekea miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar yaliyoondoa udhalimu na
kuwarudishia wazanzibari heshima ya mwanadamu na utu wake, na tutasherehekea
miaka 50 ya Muungano wetu,” alisema.
Aliwaomba watanzania wajiandae
kuyafanikisha vizuri mambo hayo ili historia mpya ifunguliwe nchini.
“Wazanzibar waanze miaka mingine
baada ya miaka hamsini ya uhuru wao, muungano uanze miaka mingine baada ya
miaka hamsini na katiba mpya itupeleke miaka mingine tukiwa wamoja,” alisema.
Aliyasema hayo jana wakati
akiadhimisha kilele cha mbio za Mwenge Uhuru zilizofanyika katika uwanja wa
Samora mjini Iringa.
Maadhimisho hayo yalitaka kuingia
dosari baada ya mtu mmoja (mwanaume) ambaye hata hivyo jina lake halikuweza
kupatikana mara moja kujichomeka katika kundi la wanahabari akiwa na nia ovu.
Wakati Rais Kikwete akiwa ameshuka
chini katika jukwaa dogo akisubiri kukabidhiwa Mwenge huo, mtu huyo alichomoka
kutoka katika kundi hilo na kujaribu kumvaa kiongozi wa mbio za mwenge, Juma
Ali Sima aliyekuwa kaubeba Mwenge huo.
Lengo lake likiwa halieleweki, mtu
huyo alitaka kuunyang’anya Mwenge huo kutoka kwa kiongozi wa mbio hizo kabla
hajadhibitiwa vikali na askari Polisi na baadhi ya walinzi wa Rais waliokuwa
jirani.
Wakati tukio hilo likitokea Rais
Kikwete pamoja na wasaidizi wake wengine walikuwa mita kama kumi kutoka katika
eneo la tukio akisubiri kukabidhiwa Mwenge huo.
Sherehe hizo zilizofana
zilihudhuriwa na maelfu ya wakazi wa mjini Iringa na vitongoji vyake, na
zilisindikizwa na burudani za vikundi mbalimbali vya ngoma za asili, kwaya na
Bongo fleva.
Maelfu ya wananchi wakisikiliza hotuba ya Rais Kikwete
Wengine waliohudhuria sherehe hizo
ni viongozi mbalimbali wa serikali kutoka wizarani, mikoani na wilayani
mbalimbali za Tanzania Bara na Visiwani.
Akifafanua umuhimu wa Mbio za Mwenge
wa Uhuru, Rais Kikwete alivipongeza vyombo vya kufikisha ujumbe wa mwenge kwa
wananchi kwa uhodari mkubwa.
“Bila vyombo vya habari wapotoshaji
hawakosekani, na wasiopenda mwenge pia wapo, hawawezi kukosekana
Alisema kilele cha maadhimisho ya
mbio za Mwenge imefanywa kuwa pia siku ya kumbukumbu ya Baba wa Taifa Mwalimu
Nyerere tangu afariki miaka 14 iliyopita.
Alisema watanzania wote bila kujali
itikadi zao wanawajibu wa kuyakumbuka mema yoote yaliyofanywa na baba wa Taifa,
mafundisho yake na urithi kwa Taifa hili.
Vijana wa Halaiki
“Nia ya maadhimisho haya, watu
wasimsahau kiongozi huyu maalumu katika hostoria ya nchi; tunahitaji kumkumbuka
hasa wakati huu wa mchakato wa Katiba,” alisema.
Alisema “tunahitaji kujikumbusha
mawazo ya mwalimu kuhusu umoja wa nchi yetu, umoja wa watu wake na Muungano wa
Zanzibar na Tanganyika.”
Alisema “hotuba zake na maandishi
yake kuhusu mambo hayo yana mafundisho mazuri na yenye manufaa, tukiyaelewa na
kuyazingatia yatatusaidia katika mjadala unaoendelea na tutakamilisha mchakato
huu salama na tutakuwa na katiba nzuri.
Alisema fikra za Mwalimu na mtazamo
wake kuhusu umoja wa watanzania na muungano tulioanao bado vina maana mpaka leo
hii ikiwa ni miaka 14 baada ya kifo chake.
Ili kumkumbuka zaidi Mwalimu Nyerere
alipendekeza siku yake ya kuzaliwa ndiyo iitwe Nyerere Day na ianze
kusheherekewa kwa mbwembwe, iwe na mijadala ya kazi zake na itumiwe kufanya
shughuli mbalimbali kuenzi kazi zake.
Alisema pamoja na mtazamo wake huo
hana maana kwamba hataki mabadiliko, lakini akayasema mabadiliko anayoyata kuwa
ni yale yatakayoipeleka nchi mbele sio kuirudisha nyuma.
Aliwapongeza watanzania wanaokataa
ushawishi wa kugawanya kwa misingi ya dini, siasa na mambo mengine.
Alisema dhambi kubwa ya kubaguana
kwa misingi yoyote ile ni kupotea kwa amani na kwamba amani ikipotea watu
watatumia muda mwingi kujihami badala ya kufanya shughuli zao za maendeleo.
Alisema kama watanzania watakubali
nchi ifike hapo, itayumba na hakuna atakayebaki salama hivyo ni muhimu kuziba
nyufa zinazoweza kuleta hali hiyo.
Alisema serikali yake itaendelea
kukemea vitendo vyote vya kuvuruga amani na watakaohusika watachukuliwa hatua
kali za kisheria.
Katika maadhimisho hayo Rais Kikwete
alizungumzia mkakati wa serikali yake wa kupambana na madawa ya kulevya,
mapambano ya Ukimwi, rushwa na maendeleo katika sekta mbalimbali kupitia mpango
wa Matokeo Makubwa Sasa.
=30=
Habari hii ni kwa Hisani ya
Mtandao wa Bongo Leaks