Wednesday, October 16, 2013

RAIS KIKWETE WAUTAJA 2014 MWAKA MAALUMU



RAIS Jakaya Kikwete amesema Mwaka 2014 ni mwaka maalumu na wa aina yake katika historia ya Tanzania kwa kuwa utakuwa na mambo makubwa matatu yatakayofanywa.

Jambo kubwa alililosisitiza ni mchakato wa Katiba Mpya ambao alisema ni lazima ukamileke mwakani kama mambo yatakwenda sawa sawa.


             Rais Dk. Jakaya Kikwete akihutubia umma wa wananchi
 
Akiyataja mambo mengine alisema “Tutasheherekea miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar yaliyoondoa udhalimu na kuwarudishia wazanzibari heshima ya mwanadamu na utu wake, na tutasherehekea miaka 50 ya Muungano wetu,” alisema.

Aliwaomba watanzania wajiandae kuyafanikisha vizuri mambo hayo ili historia mpya ifunguliwe nchini.

“Wazanzibar waanze miaka mingine baada ya miaka hamsini ya uhuru wao, muungano uanze miaka mingine baada ya miaka hamsini na katiba mpya itupeleke miaka mingine tukiwa wamoja,” alisema.

Aliyasema hayo jana wakati akiadhimisha kilele cha mbio za Mwenge Uhuru zilizofanyika katika uwanja wa Samora mjini Iringa.
Maadhimisho hayo yalitaka kuingia dosari baada ya mtu mmoja (mwanaume) ambaye hata hivyo jina lake halikuweza kupatikana mara moja kujichomeka katika kundi la wanahabari akiwa na nia ovu.

Wakati Rais Kikwete akiwa ameshuka chini katika jukwaa dogo akisubiri kukabidhiwa Mwenge huo, mtu huyo alichomoka kutoka katika kundi hilo na kujaribu kumvaa kiongozi wa mbio za mwenge, Juma Ali Sima aliyekuwa kaubeba Mwenge huo.

Lengo lake likiwa halieleweki, mtu huyo alitaka kuunyang’anya Mwenge huo kutoka kwa kiongozi wa mbio hizo kabla hajadhibitiwa vikali na askari Polisi na baadhi ya walinzi wa Rais waliokuwa jirani.

Wakati tukio hilo likitokea Rais Kikwete pamoja na wasaidizi wake wengine walikuwa mita kama kumi kutoka katika eneo la tukio akisubiri kukabidhiwa Mwenge huo.
Sherehe hizo zilizofana zilihudhuriwa na maelfu ya wakazi wa mjini Iringa na vitongoji vyake, na zilisindikizwa na burudani za vikundi mbalimbali vya ngoma za asili, kwaya na Bongo fleva.
 
        Maelfu ya wananchi wakisikiliza hotuba ya Rais Kikwete
 
Wengine waliohudhuria sherehe hizo ni viongozi mbalimbali wa serikali kutoka wizarani, mikoani na wilayani mbalimbali za Tanzania Bara na Visiwani.

Akifafanua umuhimu wa Mbio za Mwenge wa Uhuru, Rais Kikwete alivipongeza vyombo vya kufikisha ujumbe wa mwenge kwa wananchi kwa uhodari mkubwa.

“Bila vyombo vya habari wapotoshaji hawakosekani, na wasiopenda mwenge pia wapo, hawawezi kukosekana

Alisema kilele cha maadhimisho ya mbio za Mwenge imefanywa kuwa pia siku ya kumbukumbu ya Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere tangu afariki miaka 14 iliyopita.

Alisema watanzania wote bila kujali itikadi zao wanawajibu wa kuyakumbuka mema yoote yaliyofanywa na baba wa Taifa, mafundisho yake na urithi kwa Taifa hili.
                                  Vijana wa Halaiki

“Nia ya maadhimisho haya, watu wasimsahau kiongozi huyu maalumu katika hostoria ya nchi; tunahitaji kumkumbuka hasa wakati huu wa mchakato wa Katiba,” alisema.

Alisema “tunahitaji kujikumbusha mawazo ya mwalimu kuhusu umoja wa nchi yetu, umoja wa watu wake na Muungano wa Zanzibar na Tanganyika.”

Alisema “hotuba zake na maandishi yake kuhusu mambo hayo yana mafundisho mazuri na yenye manufaa, tukiyaelewa na kuyazingatia yatatusaidia katika mjadala unaoendelea na tutakamilisha mchakato huu salama na tutakuwa na katiba nzuri.

Alisema fikra za Mwalimu na mtazamo wake kuhusu umoja wa watanzania na muungano tulioanao bado vina maana mpaka leo hii ikiwa ni miaka 14 baada ya kifo chake.

Ili kumkumbuka zaidi Mwalimu Nyerere alipendekeza siku yake ya kuzaliwa ndiyo iitwe Nyerere Day na ianze kusheherekewa kwa mbwembwe, iwe na mijadala ya kazi zake na itumiwe kufanya shughuli mbalimbali kuenzi kazi zake.

Alisema pamoja na mtazamo wake huo hana maana kwamba hataki mabadiliko, lakini akayasema mabadiliko anayoyata kuwa ni yale yatakayoipeleka nchi mbele sio kuirudisha nyuma.

Aliwapongeza watanzania wanaokataa ushawishi wa kugawanya kwa misingi ya dini, siasa na mambo mengine.

Alisema dhambi kubwa ya kubaguana kwa misingi yoyote ile ni kupotea kwa amani na kwamba amani ikipotea watu watatumia muda mwingi kujihami badala ya kufanya shughuli zao za maendeleo.

Alisema kama watanzania watakubali nchi ifike hapo, itayumba na hakuna atakayebaki salama hivyo ni muhimu kuziba nyufa zinazoweza kuleta hali hiyo.

Alisema serikali yake itaendelea kukemea vitendo vyote vya kuvuruga amani na watakaohusika watachukuliwa hatua kali za kisheria.

Katika maadhimisho hayo Rais Kikwete alizungumzia mkakati wa serikali yake wa kupambana na madawa ya kulevya, mapambano ya Ukimwi, rushwa na maendeleo katika sekta mbalimbali kupitia mpango wa Matokeo Makubwa Sasa.

=30=
Habari hii ni kwa Hisani ya Mtandao wa Bongo Leaks

No comments:

Post a Comment