Mkuu wa Mkoa
wa Iringa Dkt. Christine Ishengoma kwa mara nyingine tena ametoa pole kwa
wananchi na waandishi kwa ujumla kufuatia kifo cha mwandishi wa habari wa kituo
cha luninga cha Channel Ten Iringa kilichotokea katika kijiji cha Nyololo
wilayani Mufindi.
Dkt.
Christine amesema hayo alipokuwa akiongea mambo mbalimbali ya kimkoa na kitaifa
na wananchi wa mkoa wa Iringa kupitia vyombo vya habari mkoani Iringa ofisini
kwake.
Mkuu wa Mkoa
amtoa kwa mara nyingine kwa mauti ya Daud Mwangosi. Amemtaja Mwangosi kuwa
alikuwa ni kijana katika umri wa kulitumikia taifa lake na kusema kuwa yeye
binafsi alimzoea sana na kufanya nae kazi vizuri pamoja na Ofisi ya Mkuu wa
Mkoa. Katika kuthibitisha hilo amemtaja Mwangosi kuwa alikuwa ni mjumbe katika
kamati mbalimbali za mkoani Iringa, akiwa mjumbe wa kamati ya Sensa ya Watu na
Makazi na muda mfupi kabla ya kufikwa na mauti alikuwa amekabidhiwa barua ya
uteuzi katika kamati ya kuendeleza utalii na mazingira katika mkoa wa Iringa.
Amemuomba mwenyezi Mungu kuipa heri familia ya marehemu Mwangosi.
Aidha, Mkuu
wa Mkoa wa Iringa katika mkutano huo amevishukuru vyombo vya habari mkoani hapa
kwa ushirikiano wote walioutoa katika kuhamasisha zoezi la Sensa ya Watu na
Makazi na kuwaelimsha wananchi juu ya umuhimu wa zoezi hilo na watu kuhesabiwa
kwa naendeleo ya taifa. Aidha, amewashukuru wananchi wa mkoa huu kwa muitikio
wao mzuri katika kufanikisha zoezi hilo kwa ufanisi mkubwa. Vilevile,
ameshukuru ushirikiano uliotolewa na wananchi kwa makarani ya Sensa ya Watu na
Makazi.
Akiongelea
shughuli za kitaifa zitakazofanyika Mkoani Iringa hivi karibuni, Dkt. Christine
amesema kuwa Mkoa wa Iringa utakuwa mwenyeji wa Wiki ya nenda kwa Usalama
barabarani kitaifa kuanzia tarehe 17-22 Septemba, 2012. Ametoa wito kwa
wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki katika wiki hiyo katika maonesho
yatakayokuwa yakioneshwa katika uwanja wa Samora na katika kilele cha maonesho
hayo. Akiongelea mgeni rasmi katika
maadhimisho hayo, amesema kuwa atakuwa ni kiongozi wa kitaifa katika
maadhimisho hayo.
Wakati
huohuo, Mkuu wa Mkoa wa Iringa ameongelea maadhimisho ya wiki ya utalii katika
Mkoa wa Iringa. Amesema kuwa maadhimisho hayo yataanza tarehe 23-25 Septemba,
2012 na yataambatana na maonesho ya bidhaa mbalimbali zinazoambatana na
shughuli za utalii na shughuli nyingine zinazoendana na utalii. Ametoa wito kwa
wananchi kushriki kwa wingi katika maadhimisho hayo.
Nae Kaimu
Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Adam Swai amesema kuwa katika maadhimisho
hayo kamati ya maandalizi inaendelea
kufanya maandalizi ya safari za kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii
vilivyopo mkoani hapa. Amewaarifu waandishi wa habari kuwepo kwa ofisi ya
utalii ya kanda inayojumuisha Tanapa, Bodi ya utalii na Wizara ya Maliasili na
Utalii kwa lengo la kuendeleza utalii kwa ukanda wa kusini.
=30=