Tuesday, September 11, 2012

DKT. ISHENGOMA AZUNGUMZA NA WAANDISHI HABARI IRINGA




Mkuu wa Mkoa wa Iringa Dkt. Christine Ishengoma kwa mara nyingine tena ametoa pole kwa wananchi na waandishi kwa ujumla kufuatia kifo cha mwandishi wa habari wa kituo cha luninga cha Channel Ten Iringa kilichotokea katika kijiji cha Nyololo wilayani Mufindi.

Dkt. Christine amesema hayo alipokuwa akiongea mambo mbalimbali ya kimkoa na kitaifa na wananchi wa mkoa wa Iringa kupitia vyombo vya habari mkoani Iringa ofisini kwake. 

Mkuu wa Mkoa amtoa kwa mara nyingine kwa mauti ya Daud Mwangosi. Amemtaja Mwangosi kuwa alikuwa ni kijana katika umri wa kulitumikia taifa lake na kusema kuwa yeye binafsi alimzoea sana na kufanya nae kazi vizuri pamoja na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa. Katika kuthibitisha hilo amemtaja Mwangosi kuwa alikuwa ni mjumbe katika kamati mbalimbali za mkoani Iringa, akiwa mjumbe wa kamati ya Sensa ya Watu na Makazi na muda mfupi kabla ya kufikwa na mauti alikuwa amekabidhiwa barua ya uteuzi katika kamati ya kuendeleza utalii na mazingira katika mkoa wa Iringa. Amemuomba mwenyezi Mungu kuipa heri familia ya marehemu Mwangosi. 

Aidha, Mkuu wa Mkoa wa Iringa katika mkutano huo amevishukuru vyombo vya habari mkoani hapa kwa ushirikiano wote walioutoa katika kuhamasisha zoezi la Sensa ya Watu na Makazi na kuwaelimsha wananchi juu ya umuhimu wa zoezi hilo na watu kuhesabiwa kwa naendeleo ya taifa. Aidha, amewashukuru wananchi wa mkoa huu kwa muitikio wao mzuri katika kufanikisha zoezi hilo kwa ufanisi mkubwa. Vilevile, ameshukuru ushirikiano uliotolewa na wananchi kwa makarani ya Sensa ya Watu na Makazi.

Akiongelea shughuli za kitaifa zitakazofanyika Mkoani Iringa hivi karibuni, Dkt. Christine amesema kuwa Mkoa wa Iringa utakuwa mwenyeji wa Wiki ya nenda kwa Usalama barabarani kitaifa kuanzia tarehe 17-22 Septemba, 2012. Ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki katika wiki hiyo katika maonesho yatakayokuwa yakioneshwa katika uwanja wa Samora na katika kilele cha maonesho hayo.  Akiongelea mgeni rasmi katika maadhimisho hayo, amesema kuwa atakuwa ni kiongozi wa kitaifa katika maadhimisho hayo. 

Wakati huohuo, Mkuu wa Mkoa wa Iringa ameongelea maadhimisho ya wiki ya utalii katika Mkoa wa Iringa. Amesema kuwa maadhimisho hayo yataanza tarehe 23-25 Septemba, 2012 na yataambatana na maonesho ya bidhaa mbalimbali zinazoambatana na shughuli za utalii na shughuli nyingine zinazoendana na utalii. Ametoa wito kwa wananchi kushriki kwa wingi katika maadhimisho hayo.

Nae Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Adam Swai amesema kuwa katika maadhimisho hayo  kamati ya maandalizi inaendelea kufanya maandalizi ya safari za kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo mkoani hapa. Amewaarifu waandishi wa habari kuwepo kwa ofisi ya utalii ya kanda inayojumuisha Tanapa, Bodi ya utalii na Wizara ya Maliasili na Utalii kwa lengo la kuendeleza utalii kwa ukanda wa kusini.
=30=


No comments:

Post a Comment