HOTUBA YA
MKUU WA MKOA WA IRINGA MHESHIMIWA DR. CHRISTINE G. ISHENGOMA (MB) WAKATI WA
MAADHIMISHO YA SIKU YA UHURU WA TANZANIA BARA 09/12/2012 KIMKOA KATIKA TARAFA
YA MAHENGE WILAYA YA KILOLO
Ndugu Kaimu Katibu Tawala Mkoa,
Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya,
Mheshimiwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo,
Mheshimiwa Mbunge,
Mhe. Mwenyekiti wa CCM (W),
Ndugu Katibu wa CCM (W),
Makatibu Tawala Wasaidizi Sekretarieti ya Mkoa,
Waheshimiwa Madiwani,
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Kilolo,
Viongozi wa Madhehebu ya Dini,
Viongozi wa Vyama vya Siasa,
Waandishi wa Habari,
Mabibi na Mabwana.
Ndugu
Wananchi,
Awali
ya yote napenda kuchukua fursa hii kutoa shukrani zangu za dhati kwa wananchi
wa Tarafa ya Mahenge kukusanyika katika Viwanja hivi tukiwa na lengo la
kuadhimisha na kuyakumbuka yale yote yaliyofanyika toka tumepata uhuru
9/12/1961.
Aidha,
natumia fursa hii kuwashukuru Viongozi na Wananchi wa Wilaya ya Kilolo kwa
maandalizi mazuri na kwa kukubali kwao kuadhimisha siku hii muhimu kwa Watanzania
wote.
Vilevile, nawashukuru Vikundi vya burudani
kwa kutumbuiza vizuri, na kwa ujumbe ambao mumetuachia na kutuasa. Nasema
asanteni sana.
Ndugu
Wananchi,
Mkoa wa Iringa
ulianzishwa Mwaka 1964 kutoka Mkoa wa zamani ambao uliitwa Jimbo la Kusini la Nyanda
za Juu. Makao Makuu yakiwa Mbeya. Mkoa ulikuwa na Wilaya mbili ambazo ni Njombe
na Iringa. Wilaya ya Mufindi ilianzishwa Mwaka 1964, Wilaya ya Ludewa Mwaka
1975, Makete Mwaka 1979 na Kilolo Mwaka
2002.
Na Mwaka huu
2012 Mwezi Julai Mkoa wa Iringa uligawanywa rasmi na kuunda Mkoa mpya wa
Njombe. Haya ni mafanikio makubwa sana.
Mkoa wetu wa Iringa kiutawala umegawanyika katika Wilaya tatu
ambazo ni Iringa, Kilolo na Mufindi. Mkoa pia umegawanyika katika Halmashauri
nne ambazo ni Halmashauri ya Manipaa ya Iringa na Halmashauri ya Wilaya ya
Iringa, Kilolo na Mufindi. Aidha Mkoa
umegawanyika katika Tarafa 15 Kata 93, vijiji 357 na Mitaa 164.
Ndugu
Wananchi,
Shughuli kuu
za uchumi za Mkoa wa Iringa ni Kilimo, ufugaji, upasuaji mbao, uvuvi, biashara
na ajira za maofisini na viwandani.
Asilimia 85 ya wakazi wa Iringa hujishughulisha na kilimo au kilimo na
ufugaji na katika shughuli hizi tumepata mafanikio makubwa.
Ndugu
Wananchi,
Tuko hapa leo kuadhimisha sherehe za
miaka 51 ya uhuru wa Tanzania bara. Kauli mbiu ya sherehe za uhuru mwaka
huu ni uwajibikaji , uadilifu na uzalendo ni nguzo ya maendeleo ya Taifa letu.
Ni ukweli usio pingika tukiwajibika ipasavyo, tukiwa waadilifu, na
wazalendo kuanzia kweye kaya hadi Taifa tutalitumikia Taifa na kupata maendeleo
yanayohitajika. Hivi vitu 3 ni msingi mkubwa sana wa maendeleo ya Nchi yetu,
hivyo kila mmoja inampasa kutimiza kauli mbiu hii.
Ndugu
Wananchi,
Mkoa wa
Iringa umepata mafanikio makubwa toka tulipopata uhuru mpaka sasa kutokana na
Waasisi wetu, wazazi na walezi wetu kuwajibika, kuwa waadilifu na kuwa
wazalendo wa kweli katika kutekeleza majukumu yao. Miongoni mwa Mafanikio hayo
ni pamoja na:- Mwaka 1961 pato la Mkoa lilikuwa ni Sh. 5,693,000 na Wastani wa pato la mtu kwa mwaka lilikuwa ni Sh. 103. Aidha, pato la Mkoa kwa mwaka 2011
lilikuwa Sh. 1,985,708,000 na pato
la mkazi lilikuwa Sh. 1,225,503. Hii
ni hatua kubwa kwa Mkoa wa Iringa.
Katika
ukusanyaji wa Mapato ya Halmashauri mwaka 2011/12 Sh.9,357,013,391 zilikusanywa
kutoka vyanzo vya ndani, kumekuwa na ongezeko la Sh. 9,355,366,502 ikilinganishwa
na mapato ya Sh. 1,646,889
ya mwaka
1961/62.
Ndugu
Wananchi,
Kilimo,
Eneo
linalolimwa mazao mbalimbali limeongezeka kutoka Hekta 305,208.65 mwaka 1961/62
hadi kufikia Hekta 411,116 zilizolimwa msimu 2011/12. Elimu ya kilimo bora
ilitolewa kwa wakulima na jumla ya mashamba darasa 1,603 yalianzishwa na jumla
ya wakulima 49,075 wamepatiwa mafunzo kwa vitendo kupitia mashamba haya kwa
kipindi cha 1961 hadi 2011.Pia ili kufikisha Elimu kwa Wakulima waliowengi Mkoa
umeanzisha vituo vya rasilimali watu wa Kilimo katika Kata 17.
Mbolea,
Mbolea
zilizotumika mwaka 1961/62 zilikuwa tani 16,826 na tani 300 za mbegu.
Ukilinganisha na tani 42,250 za mbolea na tani 3,142 za mbegu mwaka 2011 hii ni
sawa na ongezeko la asilimia 251 kwa matumizi ya mbolea.
Ndugu Wananchi,
Mifugo,
Mwaka 1961 Mkoa
ulikuwa na Idadi ya Ng`ombe wa Kienyeji 9,176, Idadi ya
ng’ombe wa maziwa na nyama 19, Majosho 69, Uzalishaji wa Maziwa lita 1,592,662.
Hadi kufikia mwaka 2012 Mkoa una Ng’ombe kienyeji 568,749, Ng’ombe wa Maziwa
28,081, Majosho 211, uzalishaji wa Maziwa Lt 7,676,481.
Sekta ya Ushirika
Mwaka 1961 Mkoa ulikuwa na Vyama vya
ushirika 2 vyenye Idadi ya Wanachama 460 na mtaji wa Tsh. 1,620,000. Hadi sasa
Mkoa una jumla ya Vyama vya Ushirika hai 205 Vyenye Idadi ya Wanachama 36,873
na Mtaji wa Tsh 7,870,145,046.
Viwanda na Biashara
Mkoa hadi sasa
unavyo viwanda 29 vinavyojihusisha na usindikaji wa bidhaa mbalimbali. Sekta ya Viwanda na Biashara, inaajiri watu
takriban 15,000 hii ni sawa na asilimia
1.5 ya wakazi 1,006,731 wa Mkoa wa Iringa.
Vyanzo vya maji
Hadi kufikia 2012 jumla ya vyanzo vya maji
2600 vilikuwa vimetambuliwa na jumla ya vyanzo 1752 vimehifadhiwa. Mkoa unaendelea na jitihada za
kuhakikisha vyanzo vyote vinahifadhiwa.
Upandaji wa miti
Mwaka 1961
Jumla ya miti 3,507,802 ilipandwa katika Mkoa wa Iringa,
Mwaka 2011 Mkoa umefanikiwa kupanda Jumla ya miti 43,515,611. Wananchi
wanahamasishwa kuendelea kupanda miti ili kuweza kujipatika kipato na kuhifadhi
mazingira. Mizinga hadi kufikia 2012 Mkoa unajumla ya Mizinga 25,783 ya asili
ni 17,389 na ya Kisasa ni 8394.
Utalii
Katika kipindi
cha 1961 hadi 2012, Mkoa umeainisha vivutio vya Utalii na unaendelea na zoezi
hili kwa kushirikiana na wadau mbalimbali. Zaidi ya
vivutio 78 vilikuwa vimetambuliwa hadi kufikia 2012.
Ndugu Wananchi
Elimu,
Kwa kipindi cha
1961 hadi 2012 yamepatikana mafanikio yafuatayo:
·
Kuongezeka kwa madarasa ya awali toka 67
hadi 425.
·
Kuongezeka kwa wanafunzi toka 3,015 Hadi
28,725.
Elimu ya Msingi.
Mkoa umekuwa na
Maendeleo ya kuridhisha ya utoaji taaluma kwa kutumia kigezo cha matokeo ya
mtihani wa kuhitimu Elimu ya Msingi. Katika kipindi cha 1961 hadi 2011 idadi ya
wanafunzi waliofaulu imeongezeka kutoka 347 hadi 27,899 ikiwa ni ongezeko la
wanafunzi 27,552.
Elimu ya
Sekondari
Mwaka 1961 Mkoa
ulikuwa na shule za Sekondari zipatazo 6, hadi Mwaka 2012 Mkoa unajumla ya
shule za Sekondari 148, kati ya hizo za umma 104 na za Binafsi (Non-Government
Secondary Schools) i.e. Seminari, na za Watu na Mashirika mbalimbali ya Binafsi
44.
Ndugu Wananchi,
Afya,
Mkoa wa Iringa
hadi kufikia mwaka 2012 una jumla ya vituo vya kutolea huduma za Afya 254
vilivyogawanyika kama ifuatavyo; Hospitali 7, Vituo vya Afya 21 na Zahanati
226.
Kiwango cha
mama wajawazito wanaojifungulia katika vituo vya tiba imeongezeka kufikia
asilimia 88 mwaka 2011 ikilinganishwa na asilimia 5 mwaka 1961.
Ndugu Wananchi
Maji,
Asilimia ya
wakazi wa Mkoa wa Iringa waliokuwa wakipata huduma ya maji safi na salama
Desemba 1961 ni 10%. Asilimia ya wakazi
wanaopata huduma ya maji safi na salama Desemba 2011 ni 67.3 %. Ongezeko la asilimia ya wakazi wanaopata
huduma ya maji ni 56.4%.
Ndugu Wananchi,
Barabara,
Mwaka 1961 Mkoa
ulikuwa na mtandao wa barabara upatao Km. 1,209.5 kati ya hizo Km. 76.0 ni
barabara za vumbi na Km. 1,133.5 ni changarawe.
Mtandao huo Desemba 2011 umeongezeka hadi kufikia Km. 4,786 kati ya hizo
Km. 359 ni Lami, Km. 2123 changarawe na
Km.2,304 ni udongo.
Ndugu Wananchi, Teknolojia,
Mwaka 1961 Technolojia ya Kompyuta, Mawasiliano na habari
haikuwepo Mkoani Iringa. Tulikuwa na Radio moja tu, Radio Tanzania. Lakini hadi kufikia Mwaka,
2012 Mkoa wa Iringa umekuwa na Technolojia ya Habari, TV, Radio katika maeneo
yote ya Mkoa wa Iringa. Mawasiliano yameimarika na wananchi wanafurahia
maendeleo ya habari Mfano radio Ebony, Nuru, Country, Furaha, Ovecomers,
Qibraten N.k.
Ndugu Wananchi,
Pamoja na mafanikio
haya mkoa umepata changamoto mbalimbali ambazo ni pamoja na Mkoa wa
Iringa umeathirika kwa kiwango kikubwa sana na tatizo la UKIMWI (asilimia 15.7). Hivyo nawaasa kila mmoja wetu anapaswa kubadili tabia ili
kupunguza kiasi cha maambukizi.
Pia, naomba akibnababa msiwanyanyase akinamama na pia akinamama
msiwanyanyase akinababa. Muendelee kuishi kwa upendo, utulivu na amani katika
maisha yenu yote. Tupunguze kabisa unyanyasaji wa kijinsia.
Mungu Ibariki Tanzania, Mungu Ubariki Mkoa wetu wa Iringa.
Asanteni
kwa Kunisikiliza.