Wananchi na viongozi Mkoani Iringa wametakiwa
kuongeza uwajibikaji na uadilifu kwa kutanguliza mbele uzalendo na maslahi ya
Taifa katika shughuli zao za kila siku za kujiletea maendeleo yao na maendeleo ya
Taifa.
Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt.
Christine Ishengoma alipokuwa akiwahutubia wananchi wa Mkoa wa Iringa wakati wa
maadhimisho ya siku ya Uhuru wa Tanzania Bara yaliyofanyika kimkoa katika Tarafa
ya Mahenge Wilayani Kilolo.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma (katikati) akisaini kitabu cha wageni, kushoto ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo Josheph Muhumba na Helman Msua, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji halmashauri ya Wilaya ya Kilolo (kulia)
Dkt. Christine amesema “ni ukweli usiopingika
tukiwajibika ipasavyo, tukiwa waadilifu, na wazalendo kuanzia kwenye kaya hadi
Taifa tutalitumikia Taifa na kupata maendeleo yanayohitajika. Hivi vitu vitatu
ni msingi mkubwa sana wa maendeleo ya nchi yetu, hivyo kila mmoja inampasa
kutimiza kauli mbiu hii”.
Akiongelea mafanikio yaliyopatikana mkoani Iringa
tokea Uhuru, Mkuu wa Mkoa ameyataja kuwa ni pamoja na kuongezeka kwa pato la Mkoa
na pato la mkazi. Amesema mwaka 1961 pato la Mkoa lilikuwa ni shilingi
5,693,000 na wastani wa pato la mtu kwa mwaka lilikuwa shilingi 103. Amesema
kwa mwaka 2011 pato la Mkoa limekuwa na kufikia shilingi 1,985,708,000 wakati
pato la mkazi limeongezeka na kufikia shilingi 1,225,503.
Katika
ukusanyaji wa mapato ya Halmashauri, Mkoa wa Iringa, Mkuu wa Mkoa wa Iringa
amesema kuwa kumekuwapo na ongezeko kubwa la ukusanyaji wa mapato hayo kwa
mwaka 2011/2012 mapato ya Halmashauri yaliyokusanywa ni shilingi 9,357,013,391
kutoka vyanzo vya ndani, kukiwa na ongezeko la shilingi 9,355,366,502
yakilinganishwa na mapato ya mwaka 1961/1962 ya shilingi 1,646,889.
Kwa upande wa
kilimo ambacho ni shughuli kuu ya kiuchumi, Dkt. Christine amesema kuwa Mkoa wa
Iringa umefanikiwa kuongeza eneo linalolimwa kutoka Hekta 305,208.65 mwaka
1961/1962 hadi kufikia Hekta 411,116 mwaka 2011/2012. Amesema kuwa sambamba na
kuongeza eneo hilo, pia elimu juu ya kilimo bora imeendelea kutolewa kwa
wakulima na jumla ya mashamba darasa 1,603 yameanzishwa wakati wakulima 49,075
wamepatiwa mafunzo kwa vitendo kupitia mashamba hayo kwa kipindi cha kuanzia
mwaka 1961 hadi mwaka 2011. Amesema katika kuhakikisha kuwa elimu inawafikia
wakulima wengi, Mkoa umeanzisha vituo vya rasilimali watu wa kilimo katika kata
17.
Amesema kuwa
Serikali imeendelea kuhimiza matumizi ya mbolea katika kilimo ili kuwawezesha
wakulima kupata mazao mengi na bora. Amesema Mkoa wa Iringa umeweza kuongeza
matumizi ya mbolea toka tani 16,826 na tani 300 za mbegu hadi kufikisha tani
42,250 za mbolea na tani 3,142 za mbegu kwa mwaka 2011.
Akiwasilisha Taarifa fupi ya
maadhimisho ya miaka 51 ya Uhuru na maendeleo yaliyopatikana katika wilaya ya
Kilolo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Helman Msua,
amesema kuwa pamoja na Wilaya hiyo kuanzishwa mwaka 2002 bado imepiga hatua
sana katika nyanza mbalimbali. Akitolea mfano juhudi za kukuza kilimo kupitia
matumizi ya zana bora za kilimo, amesema mwaka 2002 Wilaya yake ilikuwa na
matrekta makubwa 41 na hadi kufikia mwaka 2002 matrekta hayo yameongezeka hadi
kufikia 52. Amesema kuwa vyama vya ushirika vimeongezeka toka 15 mwaka 2002
hadi kufikia 54 mwaka 2012.
Miaka 51 ya Uhuru wa Tanzania Bara inaadhimishwa
nchini kote ikiongozwa na kauli mbiu isemayo
“uwajibikaji, uadilifu na uzalendo ni nguzo ya maendeleo ya Taifa letu”.
=30=
No comments:
Post a Comment