KWA mara ya kwanza katika historia
ya miaka 15 tangu kianzishwe, Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino (SAUT)
kimehudhurisha wahitimu wawili wa Shahada ya Uzamivu katika sheria (Ph.D).
Wahitimu hao, mtanzania Mandopi
Kevin na mnaigeria Gbadebo Anthony Olagunju walitunukiwa shahada hizo juzi
katika mahafali ya sita ya Chuo Kikuu Kishiriki cha SAUT cha Ruaha (Ruco),
mjini Iringa.
Pamoja na madaktari hao wa sheria,
MKUU wa Chuo Kikuu cha SAUT, Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa aliwatunuku vyeti
wahitimu wengine 1,777 wa astashahada, stashahada, shahada na shahada ya
uzamili katika fani mbalimbali zinazotolewa Ruco.
Fani hizo ni katika sayansi za afya,
ufundi sanifu madawa, sayansi ya kompyuta, sheria, biashara na utawala, sayansi
ya ukutubi, elimu ya jamii na ualimu na sayansi ya lugha.
Kabla ya kuwatunuku vyeti hivyo,
Askofu Ngalalekumtwa alisema “ulimwengu wa asa katika fani ya elimu ni wa
ushindani mkubwa; haisaidii kulalamika kwamba elimu itolewayo katika vyuo vyetu
ni duni wakati sisi wadau wa elimu hatufanyi juhudi yoyote katika kujikwamua
kutoka katika hali hiyo.”
Alisema lipo tatizo la wahitimu wa
vyuo vikuu kudhani kuwa elimu wanayopata ni kamilifu kumbe ni tone dogo katika
bahari ya elimu na ni mwanzo wa njia ndefu ya kupambana na mazingira
yanayowazunguka.
“napenda kuwaasa wahitimu waibweteke
na kuridhika na kiwango cha alimu waliyopata; dunia ya sasa ni ya ushindani
mkubwa. Mjenge dhana ya kutaka kujiendeleza zaidi kwani elimu haina mwisho,”
alisema.
Kwa upande wake Mkuu wa chuo cha
Ruco, Dk Cephas Mgimwa alisema kutokana na mafanikio makubwa kinayozidi
kuyapata, chuo chao kiko katika mchakato wa kuwa chuo kinachojitegemea.
“Tunataka kuwa chuo kikuu
kinachojitegemea nje ya vyuo vya SAUT, naomba niwahakikishie mababa Askofu na
wadau wengine wote kwamba tumejidhatiti na tupo tayari kujitegemea,” alisema.
Alisema adidu za rejea katika
kufikia azma hiyo zinatekelezwa na kwamba hivisasa wanasubiri mamlaka
inayohusika (TCU) iwakague pamoja na kupitia machapisho ya sera za chuo,
kumbukumbu mbalimbali na miundombinu.
Alisema chuo hicho na vingine
vinavomilikiwa na makanisa havipendelewi bali vinapendwa kwasababu vinafanya
kazi kwa faida na maendeleo ya Taifa.
Habari hii kwa hisani ya BONGO LEAKS
=30=