Friday, March 8, 2013

MKUU WA MKOA WA IRINGA AKEMEA VITENDO VYA DHULUMA KWA WANAWAKE



Jamii imetakiwa kubalidilika na kupinga vitendo vya dhuluma wanavyofanyiwa wanawake na watoto wa kike nchini kwa kuhimiza matumizi ya sheria na haki katika kuhamasisha usawa wa kijinsia.

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma katika hotuba yake ya maadhimisho ya siku ya wanawake duniani iliyofanyika kimkoa katika kijiji cha Ibangamoyo, Kata ya Ulanda Wilayani Iringa leo.

Dkt. Christine amesema kuwa ”napenda kutoa wito kwa jamii mzima kubadili mitazamo iliyopitwa na wakati dhidi ya wanawake kwa sababu haina nafasi kwa wakati tulionao sasa. Ni lazima sote kwa pamoja tufahamu kuwa kila mtu anaweza, awe mwanamke au mwanaume”. Amesema kuwa lazima vitendo vya dhuluma dhidi ya wanawake na watoto wa kike vikemewe vikali na kuhimiza matumizi ya sheria na haki katika kupinga unyanyasaji na dhuluma wanazofanyiwa wanawake. Amesema ”hapo nyuma wanawake waliachwa nyuma kwa mengi ya muhimu kama elimu, ajira, mitaji na katika kutoa maamuzi lakini sasa umefika wakati wa kutambua uwezo na mahitaji yao katika kuendeleza gurudumu la maendeleo katika jamii”.

Akiongelea nafasi ya Serikali katika kuhakikisha wanawake wanapatiwa haki katika masuala mbalimbali ya kijamii na kiuchumi amesema ”Serikali imeweka mikakati mizuri sana ya kuwawezesha wanawake katika masuala  ya elimu, ajira, nafasi za uongozi lakini tatizo limebaki katika ngazi ya familia, vijiji na Kata”. Aidha, ameshauri kuwekwa mfumo mzuri wa kushughulikia matatizo ya unyanyasaji wa kijinsia kwa wanawake na kuweka vizuri kumbukumbu za matukio hayo ili tuweze kuwa na kumbukumbu sahihi.

Katika kusisitiza hilo, ameziagiza Halmashauri za za Wilaya na Manispaa kuhakikisha matatizo yanayotokana na unyanyasaji na ukatili wa kijinsia yanashugulikiwa vizuri na kutunza kumbukumbu za matukio hayo kuanzia ngazi za vijiji, Kata hadi Halmashauri za Wilaya. Amewataka kuwa na rejesta inayoorodhesha matukio yote ya ukatili wa kijinsia na jinsi matukio hayo yalivyoshughulikiwa katika ngazi husika. Kwa kufanya hivyo itakuwa rahisi hata kuweza kufanya tafiti ili kujua ukubwa wa tatizo hilo katika ngazi ya Wilaya na Mkoa.

Dkt. Christine ameziagiza Halmashauri zote za Mkoa wa Iringa kuhakikisha elimu inatolewa mara kwa mara katika vijiji vyote ili kila mtu aelewe madhara ya ukatili wa kijinsia na pale itakapotokea mtu kufanya unyanyasaji huo achukuliwe hatua zinazostahili na wale wote wanaotendewa ukatili waweze kupata haki zao.

Mkuu wa Mkoa wa Iringa amesema kuwa Mkoa wa Iringa hauwezi kupiga hatua zaidi katika maendeleo iliwa wanawake hawatapewa nafasi katika nyanja za kiuchumi, kisiasa na kijamii. Amesema ”ili Mkoa wetu wa Iringa uweze kupiga hatua zaidi katika maendeleo ni lazima wanawake wapewe nafasi katika nyanja za Kuchumi, Kisiasa na Kijamii”. Aidha, amesisitiza elimu lazima iendelee kutolewa kwa wananchi wote na kwa muda wote siyo tu kusubiri katika kipindi cha maadhimisho hayo.

Maadhimisho ya siku ya wanawake duniani yanaongozwa na kaulimbiu isemayo ‘uelewa wa masuala ya jinsia; ongeza kasi’ kwa lengo la kuweka msisitizo kwa jamii kuona umuhimu wa kila mmoja wetu kuelewa maana ya usawa wa jinsia una umuhimu wake katika jamii.

Maadhimisho haya ni matokeo ya kumbukumbu ya kihistoria ya mwanaharakati mwanamke wa nchini Ujerumani Clara Serkin aliyejaliwa ujasiri na ushupavu wa kutetea wanawake dhidi ya  kandamizwaji, unyanyaswaji na dhuluma walizokuwa wakifanyiwa na wanaume katika nyanja za kiuchumi, kisiasa, kijamii na kiutamaduni.

Katika taarifa ya maendeleo ya shughuli za wanawake wa Wilaya ya Iringa iliyowasilishwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani Immaculate Senje amesema kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa imekuwa ikihamasisha wanawake kujiunga katika vikundi na kupatiwa elimu ya ujasiliamali na jinsi ya kubuni miradi ya maendeleo na jinsi ya kuiendesha. Amesema kuwa hadi sasa jumla ya vikundi 176 ambavyo kati  ya vikundi hivyo vikundi 100 ni vya kawaida na vikundi 66 ni benki za kijamii. Amesema kuwa vikundi hivyo vina jumla wanachama 2,021.

Amesema kuwa Halmashauri yake imekuwa ikihamasisha kuunda benki za kijamii vijijini (VICOBA), ambapo jumla ya VICOBA 66 vimeanzishwa vikiwa na wanachama 1361 na mtaji wa sh. 150,980,560. Aidha, amesema kuwa wanawake wamekuwa wakihamasishwa kujiunga na SACCOS katika maeneo yao kwa malengo ya kujijengea tabia ya kukopa na kuweka. Amesema jumla ya wanawake 1,527 sawa na asilimia 40 wamejiunga na SACCOS.

Akiongelea umiki wa ardhi, Immaculate amesema kuwa Halmashauri imeendelea na jitihada za kuwapa fursa wanawake ya kumiliki ardhi kwa sababu ndiyo rasilimali pekee inayoweza kumkomboa mwanamke kuondokana na umasikini. Amesema kuwa bado hakuna usawa katika umiliki wa ardhi kati ya wanawake na wanaume. Amesema kuwa kati ya watu 6,133 waliopata hati za kimila za kumiliki ardhi wanawake 2,006 wamepata hati za kumiliko ardhi.
=30=

WAANDISHI HABARI WA NYANDA ZA JUU WATAKIWA KUELIMISHA JUU YA CHANJO



Waandishi wa habari wa Mikoa ya Iringa, Njombe na Ruvuma wametakiwa kutoa elimu na hamasa kwa wananchi kwa lengo la kufanikisha zoezi la chanjo mpya zinazozuia magonjwa ya vichoni , uti wa mgongo na kuharisha nchini.

Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma katika hotuba yake kwenye ufunguzi wa semina ya waandishi wa habari wa mikoa ya Iringa, Njombe na Ruvuma kuhusu kuanzishwa kwa chanjo mpya za ‘pneumococcal’ na ‘rotavirus’ zinazozuia magonjwa ya vichomi, kuharisha na uti wa mgongo katika ukumbi wa chuo kikuu huria njini Iringa.

Dkt. Christine amesema “napenda kuwafahamisha rasmi kuwa mwaka huu 2013 Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imeanzisha chanjo mpya mbili za ‘pneumococcal’ na ‘rotavirus’.
Akielezea malengo ya Semina hiyo, Mkuu wa Mkoa amesema kuwa lengo kuu la semina hiyo ni kuwaelimisha wanahabari juu ya uanzishwaji wa chanjo hizo mpya. Amesema kuwa baada ya kuelewa vizuri uanzishwaji wa chanjo hizo watakuwa na jukumu la kuihabarisha jamii kuhusu chanjo mpya kwa kutoa hamasa na taarifa sahihi, muhimu na kwa muda muafaka kuhusu hizi chanjo.
Amesema kuwa vimelea vya ‘streptococcus pneumoniae’ ni kisababishi kikuu cha maradhi na vifo vitokanavyo na ugonjwa wa vichomi na homa ya uti wa mgongo kwa watoto katika nchi zinazoendelea. Amesema “vimelea vya “rotavirus” kwa upande mwingine husababisha karibia asilimia 80 ya maradhi na vifo vitokanavyo na kuharisha kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano duniani”.

Amesema “kwa mujibu wa rejea za kitaalamu zinaonesha kuwa chanjo ya ‘pneumococcal’ hukinga maambukizi ya vichomi kwa asilimia 38 na homa ya uti wa mgongo kwa karibia asilimia 87 wakati na chanjo ya ‘rotavirus’ hukinga kuharisha kunakosababisha vifo vya watoto kwa asilimia 80”.

Aidha, chanjo ya ‘rotavirus’ kwa sehemu kubwa hukinga ugonjwa wa kuharisha unaosababishwa na vimelea vya aina nyingine pia.
Dkt. Christine amewataja walengwa wa chanjo hizo kuwa ni watoto walio na umri chini ya miezi Kumi na Miwili. Aidha, amesema kuwa chanjo ya kukinga vichomi  na uti wa mgongo inatolewa mara tatu kuanzia umri wa wiki 6, 10 na 14. Chanjo ya kukinga kuhara inatolewa mara mbili kuanzia umri wa wiki 6 na 10. Amesisitiza kuwa ni vizuri mtoto apate kinga kamili ni lazima kukamilisha ratiba ya chanjo hizi mapema.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, amesema kuwa kutokana na umuhimu wa chanjo hizi na uwekezaji kwa Taifa, Serikali inatoa chanjo hizi bila malipo ili kila mtoto aweze kupata chanjo hizi. Aidha, Mkuu wa mkoa aliwahakikishia wanahabari wao kuwa chanjo hizo ni salama na zitatolewa na wataalamu wenye ujuzi na uzoefu wa kutosha.
Katika salamu za Mganga Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Robert Salim amewaomba wanahabari hao kuhakikisha wanapeleka ujumbe sahihi na kwa muda muafaka ili kuondoa dhana ambayo imekuwa ikijengeka mara zinapofanyika chanjo mbalimbali. Amesema ni vema wakawapinga wale wote wanaopotosha kuwa chanjo hizo zinalenga kuwafanya wasiweze kuzaa.
=30=