Friday, March 8, 2013

WAANDISHI HABARI WA NYANDA ZA JUU WATAKIWA KUELIMISHA JUU YA CHANJO



Waandishi wa habari wa Mikoa ya Iringa, Njombe na Ruvuma wametakiwa kutoa elimu na hamasa kwa wananchi kwa lengo la kufanikisha zoezi la chanjo mpya zinazozuia magonjwa ya vichoni , uti wa mgongo na kuharisha nchini.

Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma katika hotuba yake kwenye ufunguzi wa semina ya waandishi wa habari wa mikoa ya Iringa, Njombe na Ruvuma kuhusu kuanzishwa kwa chanjo mpya za ‘pneumococcal’ na ‘rotavirus’ zinazozuia magonjwa ya vichomi, kuharisha na uti wa mgongo katika ukumbi wa chuo kikuu huria njini Iringa.

Dkt. Christine amesema “napenda kuwafahamisha rasmi kuwa mwaka huu 2013 Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imeanzisha chanjo mpya mbili za ‘pneumococcal’ na ‘rotavirus’.
Akielezea malengo ya Semina hiyo, Mkuu wa Mkoa amesema kuwa lengo kuu la semina hiyo ni kuwaelimisha wanahabari juu ya uanzishwaji wa chanjo hizo mpya. Amesema kuwa baada ya kuelewa vizuri uanzishwaji wa chanjo hizo watakuwa na jukumu la kuihabarisha jamii kuhusu chanjo mpya kwa kutoa hamasa na taarifa sahihi, muhimu na kwa muda muafaka kuhusu hizi chanjo.
Amesema kuwa vimelea vya ‘streptococcus pneumoniae’ ni kisababishi kikuu cha maradhi na vifo vitokanavyo na ugonjwa wa vichomi na homa ya uti wa mgongo kwa watoto katika nchi zinazoendelea. Amesema “vimelea vya “rotavirus” kwa upande mwingine husababisha karibia asilimia 80 ya maradhi na vifo vitokanavyo na kuharisha kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano duniani”.

Amesema “kwa mujibu wa rejea za kitaalamu zinaonesha kuwa chanjo ya ‘pneumococcal’ hukinga maambukizi ya vichomi kwa asilimia 38 na homa ya uti wa mgongo kwa karibia asilimia 87 wakati na chanjo ya ‘rotavirus’ hukinga kuharisha kunakosababisha vifo vya watoto kwa asilimia 80”.

Aidha, chanjo ya ‘rotavirus’ kwa sehemu kubwa hukinga ugonjwa wa kuharisha unaosababishwa na vimelea vya aina nyingine pia.
Dkt. Christine amewataja walengwa wa chanjo hizo kuwa ni watoto walio na umri chini ya miezi Kumi na Miwili. Aidha, amesema kuwa chanjo ya kukinga vichomi  na uti wa mgongo inatolewa mara tatu kuanzia umri wa wiki 6, 10 na 14. Chanjo ya kukinga kuhara inatolewa mara mbili kuanzia umri wa wiki 6 na 10. Amesisitiza kuwa ni vizuri mtoto apate kinga kamili ni lazima kukamilisha ratiba ya chanjo hizi mapema.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, amesema kuwa kutokana na umuhimu wa chanjo hizi na uwekezaji kwa Taifa, Serikali inatoa chanjo hizi bila malipo ili kila mtoto aweze kupata chanjo hizi. Aidha, Mkuu wa mkoa aliwahakikishia wanahabari wao kuwa chanjo hizo ni salama na zitatolewa na wataalamu wenye ujuzi na uzoefu wa kutosha.
Katika salamu za Mganga Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Robert Salim amewaomba wanahabari hao kuhakikisha wanapeleka ujumbe sahihi na kwa muda muafaka ili kuondoa dhana ambayo imekuwa ikijengeka mara zinapofanyika chanjo mbalimbali. Amesema ni vema wakawapinga wale wote wanaopotosha kuwa chanjo hizo zinalenga kuwafanya wasiweze kuzaa.
=30=


No comments:

Post a Comment