...WATOTO WALELEWE KWA MOYO WA UPENDO NA HURUMA
Uongozi wa makao ya kulelea watoto ya Tosamaganga wametakiwa kuwalea watoto kwa moyo wa upendo na huruma ili kuwaonesha mapenzi ya kweli na kuwafanya watoto hao wasijisikie wapweke.
Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Iringa Bibi. Wamoja
Ayubu (wa tatu kulia) akimkabidhi zawadi za Iddi El Haji
Mkuu wa Kituo cha Makao ya Watoto Tosamaganga
Sista. Hellena Kihwele (wa kwanza kushoto)
Ayubu amesema kuwa watoto wanahitaji malezi bora yenye upendo wa dhati na huruma ili kuondoa upweke unaoweza kuwakabili na kuathiri makuzi yao .
Akiongelea madhumuni ya safari hiyo amesema “nimekuja hapa kufanya mambo makubwa mawili: jambo la kwanza ni kuwafikishia salamu za Iddi Eli Haji kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania , Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Mhe Rais anawatakia Heri na Fanaka katika Iddi Eli Haji”. Ameongeza kuwa “Rais amefarijika sana kushiriki nanyi kusherehekea sikukuu hii na alipenda kuwa nanyi hapa ila kutokana na majukumu kuwa mengi ametuma salamu za kuwatakia heri na fanaka katika sikukuu hii”.
Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Iringa amelitaja jambo la pili kuwa ni kukabidhi zawadi kutoka kwa Mhe. Rais ili watoto hao waweze kusherehekea pamoja nae kwa furaha. Zawadi alizozitoa Mhe. Rais kwa kituo hicho ni mchele kg. 100, mbuzi wawili na mafuta ya chakula lita 40, vyote vikiwa na thamani ya zaidi ya shilingi 380,000/ za kitanzania.
Akipokea zawahi hizo mkuu wa makazi hayo ya kulea watoto ya Tosamaganga Sista Hellena Kihwele amemshukuru Rais Kikwete kwa upendo wake wa kuwajali watoto na hasa wanaolelewa katika vituo mbalimbali na kusema kuwa walezi pamoja na watoto wamefarijika sana na msaada huo.
Nae Afisa Ustawi wa Jamii wa Mkoa wa Iringa, Samwel Seti Nyagawa amesema kuwa watoto wanaolelewa katika vituo vya makao ya kulelea watoto na wale wanaoishi katika mazingira hatarishi hujisikia faraja sana pindi wanapotembelewa na kupatiwa misaada mbalimbali hasa na viongozi. Aidha alichukuwa fursa hivyo kuwaomba wafadhali na watu mbalimbali wenye mapenzi mema kuiga mfano huo wa Rais Kikwete wa kuwasaidia na kuwatembelea watoto katika sehemu mbalimbali.
Mhe. Rais ametoa zawadi mbalimbali kwa vituo vya kulelea watoto vya Tosamaganga (Iringa), Bulongwa (Makete) na Mafinga vyote vikiwa mkoani Iringa.
Kituo cha makao ya watoto Tosamaganga kilianzishwa mwaka 1969 chini ya shirika la Mtakatifu Theresia la Mtoto Yesu katika kuhudumia wagonjwa wa hospitali ya Tosamaganga na kilianza kwa kumpokea mtoto mmoja ambaye alifiwa mama yake. Aidha kituo kinawatoto wapatao 250.