Waalimu Mkoani Iringa wameshauriwa kutenga dakika tano katika ratiba zao za vipindi ili kuzungumza suala mtambuka la ugonjwa wa UKIMWI ili kuinusuru jamii dhidi ya janga hilo .
Ushauri huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma alipokuwa akiongea na wafanyakazi wa shirika lisilo la kiserikali la SUMASESU lenye makao yake makuu Wilayani Makete pamoja na watumishi wa Serikali kuu, Halmashauri na taasisi za kidini.
Bw. Egnatio Mtawa, Mkurugenzi Mtendaji wa SUMASESU Makete akisoma taarifa yake kwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Dkt. Christine Ishengoma (hayupo pichani)
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Ishengoma amesema kuwa “tuendelee kutoa elimu shuleni ili kukabiliana na ugonjwa wa UKIMWI”, aidha, ameshauri “walimu wa Sekondari kutenga angalau dakika 5 hadi 10 kuzungumzia masuala ya ugonjwa wa UKIMWI”.
Kuhusiana na uhusiano wa mila na desturi dhidi ya maambukizi ya UKIMWI, Mkuu wa Mkoa amesema kuwa mila na desturi ni nzuri sana ila tatizo lipo katika zile zinazopotosha. Ameshauri kuwa mila na desturi zote zinazopotosha lazima ziwekwe kando ili jamii iwe salama.
Mkuu wa Mkoa amepongeza ushirikiano baina ya Serikali na SUMASESU katika sekta ya maendeleo ya jamii Wilayani Makete wenye lengo la kuijengea jamii uwezo na kuwa na maendeleo endelevu.
Katika taarifa fupi ya shirika la SUMASESU kwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa iliyotolewa na Mkurugenzi wa SUMASESU, Bw. Egnatio Mtawa amesema shirika lake linatekeleza miradi mikubwa miwili ambayo ni Mradi wa Ujana unaofadhiliwa na watu wa Marekani kupitia shirika la fhi 360 na mradi wa usalama wa chakula unaofadhiliwa na shirika la Mkate kwa Dunia la Ujerumani.
Amesema kuwa mradi wa ujana unashughulika na utoaji elimu kwa jamii ili kujikinga na maambukizi mapya ya VVU/UKIMWI, elimu ya afya ya uzazi na unyanyasaji wa kijinsia.
Nae Mkuu wa Wilaya ya Makete, Bibi. Zainabu Kwikwega amesema kuwa lengo la kutembelea shirika hilo la SUMASESU ni kumuelezea Mkuu wa Mkoa shughuli zinazofanywa na shirika hilo kwa wanamakete pamoja na kuwatia moyo ili waendelee na utoaji huo wa huduma kwa wakazi wa Makete.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Dkt. Christine Ishengoma (kulia) akisalimiana na viongozi wa Wilaya ya Makete alipofanya ziara ya kujitambulisha wilayani humo.