Monday, December 16, 2013




Halmashauri za Mkoa wa Iringa zimepongezwa kwa kazi nzuri katika sekta ya elimu hadi kufanikisha kuvuka lengo la Matokeo Makubwa Sasa (BRN) na kuuwezesha Mkoa kushika nafasi ya tatu kitaifa katika Mtihani wa darasa la saba kitaifa. 

Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi wanafunzi wa kujunga na kidato cha kwanza Mkoa wa Iringa, Bibi. Wamoja Ayubu katika hotuba yake ya ufunguzi wa kikao cha Kamati ya Uchaguzi wanafunzi wa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2013 Mkoa wa Iringa kilchofanyika katika ukumbi wa Siasa ni Kilimo mjini Iringa.

Bibi. Ayubu amesema “kiwango cha ufaulu ni kizuri sana na Mkoa wa Iringa umeshika nafasi ya tatu kati ya mikoa 25 ya Tanzania bara. Pia kiwango cha ufaulu kimepanda kwa Halmashauri zote. Kwa hiyo, nachukua nasafi hii kuzipongeza Halamshauri zote kwa kuvuka lengo la matokeo makubwa sasa ambalo ni asilimia 60 kwa mwaka 2013”.

Akiwasilisha taarifa ya mwelekeo wa matokeo ya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi mwaka 2013 Mkoa wa Irnga, Afsa Elimu Mkoa wa Iringa, Mwalimu Joseph Mnyikambi amesema kuwa mtihani wa kumaliza elimu ya msingi ulifanyika tarehe 11-12 Septemba, 2013. Amesema kuwa shule za msingi 449 kati ya shule 482 ndizo likukuwa na watahiniwa wa mtihani wa kumaliza elimu ya msingi. 

Akiongelea mahudhurio siku za mitihani, Mwalimu Mnyikambi amesema kuwa mahudhurio yameongezeka kutoka asilimia 98.3 ya mwaka 2012 hadi kufikia asilimia 99 mwaka 2013 likiwa ni ongezeko la asilimia 0.7. Amesema kuwa kiwango cha kumaliza elimu ya msingi kimeongezeka kutoka asilimia 82 (2012) hadi kufikia asilimia 84 (2013) likiwa ni ongezeko la asilimia 2. Aidha, wanafunzi ambao hawakufanya mtihani mwaka 2013 ni asilimia 1 ukilinganisha na asilimia 1.2 mwaka 2012 kutokana na sababu za utoro, vifo, ugonjwa na mimba.

Akiongelea hali ya ufaulu kwa kila Halmashauri katika Mkoa wa Iringa, Afisa Elimu Mkoa amesema kuwa Iringa Manispaa asilimia 81.9 (1), Mufindi asilimia 63.9 (2), Iringa asilimia 62.2 (3) na Kilolo asilimia 60.3 (4).

Amezitaja shule 10 bora katika Mkoa wa Iringa kuwa ni Sipto (1), Ummu Salaama (2), Ukombozi (3), St. Dominic Savio  (4), Star (5), Wilolesi (6), St. Charles (7) zote za Manispaa ya Iringa. Nyingine ni Brooke Bond (8), Southern Highland (9) Mufindi na Mapinduzi (10) Manispaa ya Iringa.
=30=

KINAMAMA WA KIKUNDI CHA SONGAMBELE WAONESHA MFANO MZURI KWA KUHUDUMIA WATOTO YATIMA




Jamii imetakiwa kutenga muda wa kuwasaidia watoto walio katika mazingira magumu ili kuwatia moyo na kuwasaidia kufikia malengo yao.


          Mkuu wa Kituo cha Amani, Mama Erica Mwakalebela 



Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa kituo cha kulelea watoto yatima cha Amani kilichopo wilayani Kilolo Erica Mwakalebela alipokuwa akiwasilisha taarifa fupi ya kituo kwa akina mama wa kikundi cha Songambele chenye makazi yake Manispaa ya Iringa walipotembelea kituo hicho kuongea na watoto na kuwapatia zawadi mbalimbali.

Erica amesema kuwa watoto yatima wanahitaji kusaidiwa kwa hali na mali. Amesema “hatuwezi kuwa wakamilifu kama hatutatoa muda wetu kuwasaidia watoto yatima. Watoto hawa ni wetu hivyo jukumu la kuwahudumia ni letu sote”. Ametoa rai kwa jamii mzima kutenga muda na rasilimali kuwahudumia watoto yatina na watoto walio katika mazingira magumu. Amesema kuwa watoto yatima kama walivyo watoto wengine wanamalengo mbalimbali katika maisha yao ambayo ili waweze kuyatimiza ni lazima jamii iweze kuwasaidia kuyafikia. Amesema kuwa kuwawezesha kuyafikia malengo hayo kutawasaidia kutimiza jukumu lao katika ujenzi wa familia zao na Taifa kwa ujumla. 


Akiongelea mafanikio ya kituo hicho, mkuu wa kituo hicho ameyataja kuwa ni kuwalea na kuwasomesha watoto katika hatua mbalimbali kuanzia shule ya msingi, sekondari, vyuo vya ufundi, utalii hadi chuo kikuu. Ameyataja mafanikio mengine kuwa ni kuwasaidia watoto katika kituo hicho hadi kupata ajira kwa wale waliokamilisha masomo yao. Aidha, amesema kuwa kituo hicho kimekuwa kikiajiri pia watoto wanaofanya vizuri katika masomo yao na fani mbalimbali katika miradi inayoendeshwa kituoni hapo.


Erica amezitaja baadhi ya changamoto zinazokikabili kituo chake kuwa ni elimu, chakula na ajira kwa watoto hao. Aidha, ametoa wito kwa wafadhili na wadau wengine kujitokeza na kukisaidia kituo hicho katika kukabiliana na changamoto hizo.


Mwenyekiti wa Kikundi cha Songambele, Mama Rehema Dunga
Akitoa nasaha zake kwa watoto yatima wa kituo cha Amani, Mwenyekiti wa kikundi cha kinamama cha Songambele, Rehema Dunga amewataka watoto hao kutokukata tamaa katika maisha yao na kusongambele. Akielezea lengo la kutembelea kituo hicho, Mwenyekiti wa Songambele amesema kuwa lengo ni kukutana na kuzungumza na watoto hao ili kuwasaidia kusongambele. 

Amewataka watoto hao kuwa wasikivu na wenye kujituma katika kile wanachofundishwa ili waweze kufanikiwa. “Wakinamama wa Songambele tumekuja hapa kuwaonesha upendo na kuwatia moyo msirudi nyuma bali msongembele katika kila jambo mnalolifanya katika maisha yenu” alisisitiza Rehema. 


Katika ziara ya kikundi hicho kwa kituo cha kulelea watoto yatima Amani, kinamama wa Songambele walipika chakula cha mchana kwa watoto hao zaidi ya 100. Aidha, walipeleka zawadi mbalimbali kama sabuni, madaftari, kalamu, mafuta, maji, juisi, dawa za meno, miswaki pamoja na vitu vingine vyote vikiwa na thamani ya zaidi ya Tshs. 650,000/=


 Miongoni mwa zawadi zilizotolewa na kinamama wa Songambele kwa kituo cha Amani

Kikundi cha kinamama cha Songambele kilianzishwa miaka miwili iliyopita kwa lengo la kuwawezesha kina mama na familia zao kusonga mbele kimaendeleo. Kikundi kina wanachama 24 kikiwa na makao makuu eneo la Lugalo, Manispaa ya Iringa. 

                                                      Kinamama wa Songambele


       Kinamama wa Songambele wakiwa katika Pozi la pamoja
=30=