Na. Ofisi ya
Mkuu wa Mkoa, Iringa
Wanaushirika mkoani Iringa wametakiwa kulipa
madeni kwa wakati ili kuepuka riba kubwa inayotokana na kuchelewa kulipa mkopo
kutoka taasisi za kifedha.
Kauli hiyo ilitolewa na mkuu wa mkoa wa Iringa, Amina
Masenza alipokuwa akifungua jukwaa la ushirika mkoa wa Iringa lililofanyika
katika ukumbi wa mikutano wa Siasa ni Kilimo mjini Iringa hivi karibuni.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza |
Masenza alisema kuwa wanaushirika wamenufaika na
mikopo inayotolewa na taasisi mbalimbali mkoani Iringa. Alisema kuwa pamoja na
manufaa hayo, changamoto kubwa imebaki kurejesha mikopo hiyo kwa wakati.
Aliwaasa wanaushirika kulipa kwa muda mikopo wanayokopeshwa.
“Nawaasa wanaushirika wenye mikopo kulipa
madeni yao kwa wakati ili kuepukana na riba inayoendela kupanda. Tukifanya
hivyo tutasaidia kujua hali ya uzalishaji hivyo kuvutia wanunuzi wengi zaidi
katika Mkoa wetu” alisema Masenza.
Akiongelea
sekta ya ushirika katika maendeleo ya wananchi, mkuu wa mkoa alisema kuwa
ushirika ni nguzo muhimu katika kuwasaidia wananchi kupata huduma za ushirika
kwa urahisi na gharama nafuu.
“Mwaka huu
vyama vya ushirika vya kilimo sita vimepata mikopo ya pembejeo toka benki ya maendeleo
ya kilimo wenye thamani ya Tsh. 277,905,600/= kwa lengo la kuendeleza Kilimo
kwenye maeneo yao kupitia udhamini wa chama kikuu cha ushirika -IFCU (1993)
LTD. Napenda kutoa wito kwa vyama hivyo vilivyopata mikopo ya kilimo kukusanya
mazao yao kwa pamoja katika maghala ili waweze kuuza kwa pamoja na kupata soko
zuri” alisema Masenza.
Jukwaa la ushirika mkoa wa Iringa ni la pili na
lilihudhuriwa na Katibu Tawala Mkoa, wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa mamlaka za
serikali za mitaa, taasisi za fedha na wanaushirika.
=30=
No comments:
Post a Comment