Friday, October 16, 2015
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU MWENENDO WA MAANDALIZI YA UCHAGUZI MKUU WA RAIS, WABUNGE NA MADIWANI ILIYOTOLEWA NA MKUU WA MKOA WA IRINGA MHESHIMIWA AMINA MASENZA TAREHE 16/10/2015
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU
MWENENDO WA MAANDALIZI YA UCHAGUZI MKUU WA RAIS, WABUNGE NA MADIWANI
ILIYOTOLEWA NA MKUU WA MKOA WA IRINGA MHESHIMIWA AMINA MASENZA TAREHE
16/10/2015
1.0 Utangulizi
Mkoa
wa Iringa unaendelea na maandalizi mbalimbali kwa ajili ya kufanikisha Uchaguzi
Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani utakaofanyika tarehe 25/10/2015. Maandalizi
hayo ni pamoja na Wagombea kuendelea na kampeni kunadi sera zao, mafunzo kwa
watendaji, maandalizi ya vituo vya kupigia kura, uhakiki wa taarifa zilizomo
kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na mapokezi ya vifaa.
2.0 Hali ya Kampeni za Uchaguzi
Kampeni
za uchaguzi zilianza rasmi tarehe 22/08/2015 na zitaendelea hadi tarehe
24/10/2015. Ratiba za kampeni zimeandaliwa na Wasimamizi wa Uchaguzi na Wasimamizi
Wasaidizi wa Uchaguzi kwa kuvishirikisha vyama vya siasa. Kwa ujumla Kampeni
hizo katika mkoa wa Iringa zinaendelea kwa hali ya amani na utulivu.
3.0 Kamati za Maadili
Wasimamizi
wote wa Uchaguzi wa Majimbo ya Uchaguzi wameunda Kamati za Maadili katika ngazi
ya Jimbo. Kamati hizo pia zimeundwa katika ngazi ya Kata kwa Kata zote za Mkoa
wa Iringa. Lengo la kuundwa kwa Kamati hizi ni kusimamia utekelezaji wa maadili
ya Uchaguzi ya mwaka 2015.
4.0 Mafunzo kwa Wasimamizi wa Uchaguzi
Mafunzo
tayari yametolewa kwa Wasimamizi wa uchaguzi na Tume ya Taifa ya Uchaguzi.
Mafunzo hayo yalitolewa kwa Waratibu wa Uchaguzi wa Mikoa, Wasimamizi wa
Uchaguzi na Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi katika ngazi ya Jimbo. Aidha, Halmashauri
zimeendesha mafunzo pia kwa Wasimamizi Wasaidizi ngazi ya Kata zote za Mkoa wa
Iringa kuanzia tarehe 3/10/2015 hadi 13/10/2015.
5.0 Utangazaji wa nafasi za Wasimamizi
wa Vituo, Wasimamizi Wasaidizi wa Vituo,
na Makarani waongozaji
Matangazo
hayo yalitolewa katika Halmashauri zote 5 za Mkoa wa Iringa tarehe 1/10/2015
hadi 5/10/2015. Zoezi linaloendelea ni kufanya uchambuzi wa walioomba nafasi
hizo ili kupata wenye sifa stahiki.
6.0 Vituo vya Kupigia Kura
Awali
Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilitoa orodha ya vituo 1,641 vitakavyotumika katika
zoezi la upigaji kura kwa Mkoa wa Iringa kwa Halmashauri zote 5. Idadi hiyo
imepungua kufikia vituo 1,601 baada ya uhakiki wa wapiga kura kwenye Daftari la
Kudumu la Wapiga Kura unaoendelea kufanywa na Wasimamizi wa Uchaguzi.
7.0 Mapokezi ya Vifaa
Halmashauri
zimepokea vifaa kama masanduku, mifuniko, Tshirts, kofia, Vituturi, na fomu mbalimbali kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu.
Aidha,
Wasimamizi wanaendelea kufanya tathmini ili kujiridhisha endapo
vifaa vilivyopokelewa vinakidhi mahitaji.
8.0 Daftari la Kudumu la Wapiga Kura
Tayari
Tume ya Taifa ya Uchaguzi imetoa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa
Halmashauri zote. Kazi inayoendelea hivi
sasa ni uhakiki wa idadi ya wapiga kura kwa kila kituo.
9.0 Mambo Muhimu ya Kuzingatiwa na
Wapiga Kura na Wananchi
(a) Sifa
za Mpiga Kura
- Mpiga kura ni raia yeyote wa Tanzania,
- Aliyefikisha umri wa miaka 18,
- Aliyeandikishwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura,
- Mwenye kadi ya kupigia kura iliyotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi.
- Lazima awe Mkazi wa eneo analotaka kupiga kura na jina lake limeorodheshwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura au Orodha iliyobandikwa katika Kituo cha Kupigia Kura.
- Orodha ya Wananchi wanaoshahili kupiga kura itabandikwa kwenye Vituo husika siku 8 kabla ya Uchaguzi hivyo wananchi wapitie Orodha hiyo mapema ili wajue vituo watakavyopigia kura.
- Vituo vyote vya kupigia kura havitawekwa katika nyumba za watu binafsi, vituo vidogo vya Polisi wala nyumba za Ibada kwa lengo la kuwapa nafasi na uhuru wapiga kura.
- Katika zoezi la Kupiga Kura kipaumbele kitatolewa kwa watu wenye Ulemavu, Wanawake Wajawazito na wale wenye Watoto Wachanga, Wagonjwa na Wazee ili wasikae muda mrefu kwenye mistari.
- Wapiga kura wasioweza kupiga kura wao wenyewe, wasioona au wasiojua kusoma watasaidiwa na watu watakao wateua wao wenyewe. Aidha, Tume imeandaa kifaa (Tactile Ballot Folder) kitakachowasaidia wapiga kura wasioona ili waweze kupiga kura zao wao wenyewe.
- Vituo vya kupigia kura vitafunguliwa saa 1:00 asubuhi na vitafungwa saa 10.00 Jioni, iwapo kutakuwa na wapiga kura katika mistari muda huo, wapiga kura hao wataruhusiwa kupiga kura. Aidha, wapiga kura watakaofika baada ya muda huo hawataruhusiwa kupiga kura.
10.0 Makosa ya Uchaguzi (Makosa ya
Jinai kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi Sura 343 na Sheria ya Uchaguzi wa
Serikali za Mitaa Sura 292)
- Kujaribu kupiga kura wakati muda wa kupiga kura umekwisha,
- Kujaribu kupiga kura wakati hauruhusiwi kisheria kupiga kura,
- Kujaribu kupiga kura zaidi ya mara katika uchaguzi,
- Kujaribu kupiga kura kwa kutumia kadi ya mtu mwingine,
- Kuweka kitu kingine zaidi ya karatasi ya kupigia kura katika sanduku la kuhifadhia kura.
- Kuchana orodha ya wapiga kura au mabango yoyote ya elimu kwa mpiga kura.
- Kughushi au kuharibu karatasi ya kura,
- Kuchapisha na kusambaza karatasi za kura bila mamlaka kisheria,
- Kupokea au kutoa rushwa kabla na wakati wa uchaguzi,
- Kumzuia mtu kupiga kura yake kwa uhuru na amani,
- Kutoa siri ya mpiga kura mwenzio kuwa anakwenda kumpigia kura Fulani au amempigia mtu Fulani.
- Kuvaa au kuonesha alama yoyote ya chama wakati wa zoezi la upigaji kura.
- Kuchukua kadi za Wapiga Kura ili wasiweze kupiga Kura.
- Kutumia vitisho na nguvu kuwashawishi wapiga kura ili wakupigie kura.
11.0 Ulinzi na Usalama
Mkoa
wa Iringa umejipanga vizuri kuhakikisha amani na usalama kwa kipindi chote cha
kampeni za Uchaguzi na wakati wa zoezi la kupiga kura vyote vinafanyika vizuri
kwa mujibu wa ratiba na kwa kuzingatia sheria za nchi ili Wananchi waendelee
kuwa salama na kutekeleza majukumu yao.
Napenda
kutoa rai kwa wananchi wote wa Mkoa wa Iringa kufahamu na kukubaliana kuwa yapo
maisha na yataendelea kuwepo hata baada ya Uchaguzi Mkuu hapo tarehe 25 Oktoba,
2015. Hivyo, kila mmoja wetu lazima atimize wajibu wake katika kuhakikisha
amani na utulivu vinaendelea kuwepo katika kipindi hiki chote ili tumalize
zoezi hili tukiwa wamoja na wenye mshikamano mkubwa.
Katika
kuhakikisha mkoa unakuwa na utulivu kwa kipindi chote, nimekutana na makundi
mbalimbali kujadili suala la amani kuelekea Uchaguzi Mkuu. Makundi hayo ni
viongozi wa vyama vya siasa, viongozi wa madhehebu ya dini, wazee na watu wenye
ushawishi katika jamii na waandishi wa habari.
Lengo
ni kupata maoni yao na ushauri wa jinsi ya kufanikisha Uchaguzi Mkuu kwa amani
na utulivu.
Napenda
kuchukua nafasi hii kuwathibitishia Wananchi wa Mkoa wa Irirnga kuwa, ulinzi
utakuwepo wa kutosha katika kipindi chote cha kampeni na siku ya kupiga kura
tarehe 25/10/2015.
Jeshi
la Polisi limejipanga vizuri kuwalinda wananchi wote, hivyo, rai yangu kwa Wananchi
ni kuwa jitokezeni kwa wingi siku ya kupiga kura mapema na baada ya kupiga kura
rudini kwenye maeneo yenu kuendelea na shughuli nyingine. Wananchi wasibaki
kwenye vituo vya kupigia kura baada ya kupiga kura.
Asanteni kwa kunisikiliza
Subscribe to:
Posts (Atom)