HOTUBA YA MHESHIMIWA MIZENGO P. PINDA (MB), WAZIRI MKUU WA
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, WAKATI WA KUHITIMISHA SHUGHULI ZA MKUTANO WA
13 WA BUNGE LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA TAREHE 09 NOVEMBA, 2013
Waziri Mkuu wa Tanzania, Mizengo Pinda (Mb.)
I:
UTANGULIZI
a) Masuala ya Jumla
Mheshimiwa Spika,
1.
Leo tunahitimisha
shughuli za Mkutano wa Kumi na Tatu wa Bunge lako Tukufu. Ni jambo la
kumshukuru Mwenyezi Mungu mwenye wingi wa Rehema kwa kutufikisha salama siku ya
leo.
Mheshimiwa Spika,
2.
Mkutano huu
ulijumuisha kazi kubwa zifuatazo:
Kwanza: Kujadili Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo
wa Taifa kwa Mwaka 2014/2015;
Pili: Kujadili Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya
Sheria mbalimbali wa Mwaka 2013, [The Written Laws (Miscellaneous Amendments
(No. 3) Bill 2013];
Tatu: Kujadili Muswada wa Sheria ya Mfuko wa Akiba
wa GEPF wa Mafao ya Wastaafu wa Mwaka 2013 [The GEPF Retirement Benefit
Bill, 2013]; na
Nne: Kujadili Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya
Mabadiliko ya Katiba (The Constitutional Review Act) sura ya 83.
3.
Nitumie nafasi hii
kuwapongeza Waheshimiwa Wabunge wote kwa kushiriki katika Kamati ya Mipango
hapa Bungeni kwa kujadili kwa kina mapendekezo yaliyowasilishwa na Serikali
kuhusu Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2014/2015. Napenda
kuwahakikishia kuwa, maoni na ushauri kama yalivyotolewa na Waheshimiwa Wabunge
yatazingatiwa na Serikali kila moja kwa uzito wake wakati wa maandalizi ya
Bajeti ya 2014/2015. Vilevile niwashukuru kwa kujadili na kupitisha Muswada wa
Sheria ya Mfuko wa Akiba wa GEPF wa Mafao ya Wastaafu.
b)
Maswali
Mheshimiwa Spika,
4.
Pamoja na kukamilisha
kazi hizo muhimu, pia katika Mkutano huu, jumla ya maswali 120 ya msingi
na 305 ya nyongeza ya Waheshimiwa Wabunge yalijibiwa na Serikali.
Aidha, Maswali 6 ya msingi na 6 ya nyongeza yalijibiwa kwa
utaratibu wa Maswali ya Papo kwa Papo kwa Waziri Mkuu.
c) Kauli za Mawaziri/Maazimio
Mheshimiwa Spika,
5. Mkutano huu pamoja na kazi za msingi zilizopangwa, Waheshimiwa
Wabunge walipata
fursa ya kujadili
Azimio la Kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania kuhusu msimamo wake katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.
(d)
Hotuba ya Mheshimiwa Rais,
Mheshimiwa Spika,
6.
Katika Mkutano huu
pia, Waheshimiwa Wabunge walipata fursa ya kumsikiliza Mheshimiwa Dkt. Jakaya
Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akizungumza na Wananchi
kupitia Bunge lako Tukufu. Mtakubaliana nami kwamba hotuba ya Mheshimiwa
Rais ilikuwa nzito na yenye kuonesha umakini, umahiri na busara ambazo ni sifa
mojawapo za Rais wetu kati ya nyingi nzuri alizonazo. Tunachotakiwa ni kutumia
maelekezo ya Mheshimiwa Rais kwa kuyafikisha kwa Wananchi katika maeneo yetu
ili nao waweze kuelewa hali halisi ya yanayotokea katika Jumuiya yetu. Aidha,
Hotuba ya Rais imegusa maeneo mengine ambayo sisi Wabunge tunatakiwa
kushirikiana na Wananchi katika kujipanga vizuri namna ya kukabiliana na
matatizo yaliyojitokeza.
II: UTEKELEZAJI WA MPANGO NA
BAJETI YA MWAKA 2013/2014
(a) Mwenendo wa Mapato na
Matumizi ya Serikali katika Robo ya Kwanza ya Mwaka 2013/2014
Mheshimiwa Spika,
7.
Hotuba yangu kwa leo
imejikita zaidi kuelezea utekelezaji wa Mpango wa Bajeti ya Mwaka 2013/2014 na
maeneo machache katika Sekta ya Kilimo na Nishati. Lakini kabla ya kuelezea
mwenendo wa Mapato na Matumizi ya Serikali katika Robo ya Kwanza ya mwaka 2013/2014,
naomba kueleza kwa muhtasari kuhusu mwenendo wa baadhi ya viashiria muhimu vya
uchumi hususan Ukuaji wa Uchumi na Mfumuko wa Bei. Taarifa za awali
zilizotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu zinaonesha kwamba Ukuaji wa Pato la
Halisi la Taifa katika kipindi cha nusu ya kwanza ya mwaka 2013, ulikuwa
Asilimia 7.0 ikilinganishwa na ukuaji wa Asilimia 6.9 katika
kipindi kama hicho mwaka 2012. Sekta zilizoonesha kuwa na Viwango vikubwa
vya ukuaji ni pamoja na Sekta ya Mawasiliano na Usafirishaji ambayo imekua kwa
Asilimia 18.4, Sekta ya Fedha Asilimia 14.6 na Sekta ya Ujenzi
Asilimia 8.7.
Mheshimiwa Spika,
8.
Kwa upande wa Mfumuko
wa Bei, takwimu zinaonesha kuwa kasi ya upandaji bei imepungua kutoka Wastani
wa Asilimia 13.5 Mwezi Septemba, 2012 hadi Asilimia 6.1 Mwezi
Septemba, 2013. Kushuka kwa Mfumuko wa Bei kumechangiwa zaidi na upatikanaji wa
chakula cha kutosha ndani ya Nchi. Mwenendo huu mzuri wa viashiria vya uchumi
jumla unatupa matumaini makubwa kwamba jitihada za Serikali za kuimarisha
usimamizi wa Uchumi na kuleta Maendeleo endelevu ya Wananchi wetu zinaanza
kuzaa matunda.
Mheshimiwa Spika,
9.
Katika Robo ya Kwanza
ya mwaka 2013/2014 kuanzia Mwezi Julai hadi Septemba 2013, Mapato yote
yaliyokusanywa na Hazina yalifikia Shilingi Trilioni 3.08; sawa na
Asilimia 85.7 ya makadirio ya Shilingi Trilioni 3.59. Pamoja na
mwenendo huo wa ukusanyaji mapato, changamoto kubwa zinazokabili eneo la Mapato
ya Serikali ni kuchelewa kuanza kwa wakati kwa ukusanyaji wa Mapato katika
baadhi ya vyanzo vya mapato. Changamoto nyingine ni Miundombinu isiyokidhi
mahitaji ya usafirishaji endelevu hasa reli ya kati, bandari, usafiri wa Anga
na barabara. Miundombinu Bora ni muhimu katika kuchochea ukuaji wa Uchumi
na Kukuza Ajira; na hivyo kuiwezesha Serikali kukusanya mapato zaidi kutokana
na kuongezeka kwa shughuli za kiuchumi. Serikali inafanyia kazi changamoto hizo
ili kuzipatia ufumbuzi mapema.
Mheshimiwa Spika,
10.
Kwa upande wa matumizi,
hadi kufikia mwezi Septemba 2013; matumizi yalifikia Shilingi Bilioni 3,806.5,
sawa na Asilimia 98.5 ya lengo la kutumia Shilingi Bilioni 3,854.2. Kati
ya matumizi hayo, Shilingi Bilioni 3,058 ni Matumizi ya Kawaida na
Shilingi Bilioni 747.9 ni Matumizi ya Maendeleo. Katika kipindi
hiki, sehemu kubwa ya matumizi ya Serikali ya Kawaida na Maendeleo imeelekezwa
katika maeneo yenye kuleta ufanisi na tija kubwa kama vile kuboresha
miundombinu ya barabara, ambayo mgao wake ulikuwa Shilingi Bilioni 182.5
za Matumizi ya Kawaida na Maendeleo, Sekta ya Elimu Shilingi Bilioni 229.2;
Sekta ya Nishati, Shilingi Bilioni 159.9; Sekta ya Kilimo Shilingi
Bilioni 119.6 na Sekta ya Maji Shilingi Bilioni 51.3. Vilevile, Serikali
imelipa Mishahara ya Watumishi wa Umma kwa wakati. Changamoto kubwa iliyopo
kwenye matumizi ya Serikali ni kuwepo kwa mahitaji makubwa ya matumizi
yasiyowiana na mapato; jambo ambalo linailazimu Serikali kukopa kutoka Mabenki
ya Ndani. Serikali itaendelea kuoanisha Matumizi na ukusanyaji wa Mapato, hasa
yale ya ndani pamoja na kuzingatia viwango vya Matumizi vilivyoidhinishwa na
Bunge. Aidha, Serikali itaendelea kuweka msisitizo wa kuelekeza Matumizi kwenye
vipaumbele vilivyoainishwa katika Bajeti ya Serikali ambavyo ni vyanzo muhimu
vya kuongeza Mapato, Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini.
III:
UTEKELEZAJI WA MFUMO MPYA WA TEKELEZA KWA MATOKEO MAKUBWA SASA (BIG RESULTS
NOW - BRN)
(a) Muundo wa Mfumo
Mheshimiwa Spika,
11.
Waheshimiwa Wabunge watakumbuka kuwa Serikali ilianzisha Mfumo mpya wa “Tekeleza
kwa Matokeo Makubwa Sasa au Big Results Now (BRN) ili kuongeza
ufanisi katika usimamizi, ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa Mipango
yetu ya Maendeleo, hususan, Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2011/2012 -
2015/2016). Hatua hii ilichukuliwa baada ya kuona namna Mfumo kama
huo ulivyoziwezesha Nchi kadhaa, na hasa Nchi ya Malaysia, kupiga hatua kubwa za
kimaendeleo kiuchumi na kijamii katika kipindi kifupi. Kwa ukumbusho tu, Mfumo
huo unatekelezwa katika Maeneo Sita ya Matokeo muhimu Kitaifa (National Key
Results Areas) katika awamu yake ya kwanza, ambayo ni Nishati ya Umeme;
Uchukuzi; Kilimo; Elimu; Maji na Ukusanyaji wa Mapato;
Mheshimiwa Spika,
12.
Katika
Hotuba yangu ya kuahirisha Mkutano wa Kumi na Mbili wa Bunge, tarehe 6 Septemba
2013, nilitoa taarifa ya awali kuhusu utekelezaji wa Mfumo huu Mpya kwa kipindi
cha kuanzia mwezi Julai hadi Septemba, 2013. Katika taarifa hiyo, nilieleza
kuwa tumepiga hatua za kuridhisha katika uundaji wa Mfumo wa kuleta
matokeo ya haraka, ikiwa ni pamoja na kuanzisha na kuteua Uongozi wa juu wa
Taasisi Maalum yaani "President’s Delivery Bureau (PDB)” inayomsaidia
Mheshimiwa Rais kusimamia ipasavyo utekelezaji wa Miradi na Programu
zilizoainishwa. Hivi sasa zoezi la kuajiri Watumishi wa Taasisi ya "President’s
Delivery Bureau” na Vitengo vya Wizara vya Ufuatiliaji yaani Ministerial
Delivery Units (MDUs) watakaochukua nafasi za Watumishi walioazimwa kutoka
kwenye Wizara na Taasisi mbalimbali za Serikali, Sekta Binafsi, na Asasi Zisizo
za Kiserikali ambao walikuwepo katika hatua zake za maandalizi limeanza.
Ninapenda kutumia fursa hii kuwashukuru wote waliotumika katika chombo hiki
tangu kilipoundwa kwa uzalendo na weledi waliouonesha katika kipindi hiki cha
mwanzo na cha mpito;
Mheshimiwa Spika,
13.
Napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba hadi sasa vitengo vya
ufuatiliaji katika Wizara zote sita (6) zinazosimamia utekelezaji chini ya
Mfumo huu mpya vimeanzishwa na vinaandaa Taarifa za utekelezaji za kila wiki na
kila mwezi, na kuziwasilisha kwenye Chombo cha President’s Delivery Bureau.
Aidha, Kamati Maalum za kusimamia utekelezaji zinazoongozwa na Mawaziri husika
zinakutana kila mwezi kujadili mwenendo wa utekelezaji na kushughulikia
changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika utekelezaji. Baraza la Kusimamia
Mageuzi na Utekelezaji (Transformation and Delivery Council – (TDC))
limeundwa na lilikutana tarehe 11 Oktoba, 2013. Katika Kikao hicho, Baraza
lilipokea na kujadili muhtasari wa Taarifa ya utekelezaji wa Mfumo mpya wa
Kusimamia, Kufuatilia na Kutathmini Miradi ya Kipaumbele katika Maeneo Sita ya
Matokeo ya Kitaifa. Baraza liliridhika na hatua za awali za utekelezaji na
lilitoa mwongozo stahiki wa hatua za kuchukuliwa pale ilipohitajika. Baraza litaendelea
kukutana mara kwa mara ili kutathmini na kutoa mwelekeo wa utekelezaji wa
Mikakati iliyowekwa ya Mfumo huu mpya;
(b) Utekelezaji wa Mikakati
katika Maeneo Makuu Sita ya Matokeo Kitaifa;
Mheshimiwa Spika,
14.
Utekelezaji wa mikakati katika maeneo makuu sita ya matokeo kitaifa ulianza
mara baada ya uchambuzi wa maabara kukamilika. Mafanikio ya kuridhisha
yamepatikana katika kila moja ya maeneo yale sita, hasa ikizingatiwa kwamba
Mfumo huu ni mageuzi makubwa sana katika utendaji Serikalini. Katika kipindi
cha miezi mitatu ya mwanzo ya mwaka huu wa fedha, kuanzia mwezi Julai hadi
Septemba, 2013; baadhi ya matokeo yaliyopatikana ni pamoja na yafuatayo:
(a) Katika Sekta ya Kilimo, Serikali inatekeleza miradi 26 ya
umwagiliaji kwa Wakulima wadogo na pia imekarabati maghala 26 ya mpunga
kati ya 39 yanayotumiwa na wakulima katika maeneo yaliyopewa kipaumbele
hasa katika eneo la SAGCOT.
(b)
Katika Sekta ya Nishati ya Umeme, jumla ya Wateja wapya 27,494
wameunganishwa na kupatiwa umeme, ikiwa ni Asilimia 18.3 ya lengo la
kuunganisha wateja wapya 150,000 hadi mwisho wa mwaka 2013/2014. Aidha,
vipande vya Bomba la Gesi 20,491 vinavyotosheleza ujenzi
wa Kilomita 243.8 za Bomba la Gesi tayari vimewasili Nchini, na
uchomeleaji wa Bomba la Gesi Asilia kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam
umekamilika kwa Kilomita 124.3. Vilevile, Kilomita 447 za njia ya Bomba la Gesi
zimesafishwa;
(c)
Katika Sekta ya Elimu, Shule za msingi 5,916 zilipatiwa mitihani ya
marejeo na mazoezi, sawa na Asilimia 100 ya lengo la mwaka. Aidha, Mafunzo
Kazini kuhusu ufundishaji yametolewa kwa Walimu katika Shule 1,325 sawa
na Asilimia 65 ya lengo la Shule 2,048 kwa mwaka huu wa fedha;
(d)
Kwa upande wa huduma za maji, wananchi wapatao 752,000
waishio Vijijini wamepatiwa huduma ya maji. Mafanikio haya yanafanya
idadi ya Wananchi waishio Vijijini ambao wanapata majisafi na salama kufikia
takribani Milioni 15.9. Kasi hii ya upanuzi wa huduma za Maji Vijijini
imewezekana baada ya Wizara ya Maji kugatua madaraka ya usimamizi wa miradi
husika kwa Sekretarieti za Mikoa na Halmashauri za Wilaya, jambo ambalo
limewafanya Watendaji kuwajibika na kuharakisha utendaji wao wa kazi. Aidha,
hatua zilizochukuliwa zimeiwezesha Wizara ya Maji kuongeza ufanisi katika
masuala ya ununuzi wa huduma, ikiwemo ujenzi na vifaa vyake, kutoka wastani wa
siku 265 za hapo awali hadi siku 90 za sasa.
Mheshimiwa Spika,
15. Mafanikio haya na
mengine mengi ambayo sikuyataja hapa yameonyesha kuwa tukidhamiria, tunaweza
kubadilisha kabisa matokeo ya juhudi zetu na kuifikia dhamira yetu ya kuwa ni
Taifa la Kipato cha Kati ifikapo mwaka 2025;
Mheshimiwa Spika,
16.
Kufuatia mafunzo yaliyotolewa mapema mwezi Juni, 2013 kwa Watendaji wa
Wizara husika, Wakuu wa Mikoa wote, Makatibu Tawala wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya
zote Nchini, mnamo Mwezi Septemba 2013 nilikutana na Wakuu wa Mikoa na Makatibu
Tawala wa Mikoa yote Tanzania Bara ili kujadili kwa kina Taarifa za utekelezaji
wa Miradi ya kipaumbele chini ya Mfumo huu. Aidha, katika Vikao hivyo,
nimezielekeza Wizara, Mikoa na Halmashauri zote Nchini kufanya yafuatayo:-
(a) Kuchambua miradi
iliyopangwa kutekelezwa katika mwaka huu wa fedha ambayo ipo nje ya Mfumo
wa “Tekeleza kwa Matokeo Makubwa Sasa” kwa kutambua manufaa yanayotarajiwa
baada ya kukamilika na mahitaji halisi;
(b) Kuipanga miradi hiyo kwa kipaumbele ili
kuweka mkazo katika miradi itakayokamilika haraka na kuwa na manufaa makubwa
kwa Wananchi; na,
(c) Kuweka utaratibu wa
Kimfumo na Kitaasisi wa kufuatilia utekelezaji wa miradi ya kipaumbele.
Mheshimiwa Spika,
17.
Ninafurahi kutoa taarifa kuwa Wizara na Tawala za Mikoa na Mamlaka za
Serikali za Mitaa zimeupokea mfumo wa Tekeleza kwa Matokeo Makubwa Sasa kwa
hamasa kubwa. Ili kuhakikisha azma yao ya kutekeleza majukumu yao katika Mfumo
huu kikamilifu, iliamuliwa kuwa Viundwe Vitengo vya kusimamia utekelezaji
katika Ngazi ya Mkoa (Regional Delivery Units (RDUs), sambamba na vile
Vitengo vya ufuatiliaji vya Wizara ili utekelezaji katika Maeneo Makuu ya
Matokeo Kitaifa ufanyike kwa ufanisi na umakini stahiki. Hatua hii inazingatia
umuhimu wa kuhakikisha kuwa maeneo kama Elimu na Maji ambayo Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa zina mchango mkubwa katika utekelezaji yanapata msukumo wa
kutosha. Kazi hii imeshaanza, na taarifa zilizowasilishwa ni za kutia moyo
sana.
Mheshishimiwa Spika,
18. Kwa kuzingatia mafanikio ya awali
yaliyopatikana, Serikali imetoa maelekezo kwa Wizara, Idara na Taasisi ambazo
bado hazijaingia katika Mfumo wa Tekeleza kwa Matokeo Makubwa Sasa zisisubiri
hadi zitakapoingia rasmi bali zianze kujipanga na kutekeleza mipango, miradi na
program zao kwa kutumia mbinu ambazo zinatumika katika Mfumo huo pamoja na
Rasilimali fedha na Wataalam waliopo. Msisitizo ni kwamba Wizara zote na
Mikoa ijipange upya na kuongeza ubunifu na kufanya vizuri zaidi katika
kuimarisha usimamizi wa miradi ya maendeleo ili kuhakikisha kwamba Taifa letu
linafikia malengo ya maendeleo tuliyojiwekea katika Dira ya Maendeleo ya Taifa
2025. Aidha, napenda kutumia fursa hii kutoa wito kwa Wizara, Mikoa na Mamlaka
za Serikali za Mitaa kuimarisha usimamizi wa Watendaji wao kwa kuzingatia
taratibu za uwajibikaji zilizowekwa chini ya mfumo huu mpya ili kuleta ufanisi
na tija ya utendaji Serikalini pamoja na kupata matokeo makubwa tarajiwa ya
Kukuza Uchumi na kuondoa umaskini;
IV: MAPENDEKEZO YA MPANGO WA MAENDELEO YA
TAIFA WA MWAKA 2014/2015
Mheshimiwa Spika,
19. Mwanzoni mwa Mkutano huu
wa Bunge Serikali iliwasilisha Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo 2014/2015. Napenda kutumia fursa hii tena kuwapongeza
Waheshimiwa Wabunge kwa maoni na michango yao mizuri ambayo itatuwezesha
kuboresha Mpango na Bajeti ya Mwaka ujao wa Fedha 2014/2015. Aidha, namshukuru
Mheshimiwa Stephen Wasira (Mb.) pamoja na Waheshimiwa Mawaziri wa Kisekta
waliotoa maelezo fasaha ya ufafanuzi wa Hoja zilizojitokeza wakati wa Mjadala
wa Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo. Kwa kuzingatia michango mizuri na yenye
tija iliyotolewa na Waheshimiwa Wabunge na Waheshimiwa Mawaziri wakati wa
kujadili Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa wa mwaka 2014/2015, nami
naomba uniruhusu kusisitiza mambo machache kama ifuatavyo:
Mheshimiwa Spika,
20.
Kama Waheshimiwa
Wabunge watakavyokumbuka katika majadiliano yaliyokuwa yanaendelea,
moja ya jambo ambalo Waheshimiwa Wabunge wamelizungumzia kwa kina, ni juu ya
wingi wa vipaumbele vya Taifa. Aidha, imeonekana pia kuwa miradi ya
maendeleo ni mingi sana kiasi kinachosababisha miradi hiyo kutotekelezeka
kutokana na ufinyu wa rasilimali fedha. Napenda kulifahamisha Bunge lako Tukufu
kuwa Vipaumbele vilivyopendekezwa na Serikali vinategemeana na vinalenga
kutanzua vikwazo vikuu vya kiuchumi Nchini ili kufungua fursa za ukuaji wa
uchumi wa Taifa na kuharakisha maendeleo na ustawi wa Wananchi wa Tanzania.
Pendekezo la Serikali ni kuwa njia bora si kupunguza vipaumbele hivi sasa, bali
ni kupanga vizuri mtiririko wa utekelezaji wa miradi ndani ya kila kipengele
ili kuongeza jitihada za kuongeza Mapato, na kusimamia nidhamu ya matumizi.
Mheshimiwa Spika,
21.
Kwa
kuwa Mpango huu wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2011/2012 - 2015/2016) ni wa
kwanza unaojenga msingi wa mipango mingine ya maendeleo ya miaka mitano
itakayoandaliwa, ni dhahiri kuwa kasi ya utekelezaji wake itarahisisha
utengenezaji wa mipango mingine na kupunguza vipaumbele vya msingi katika
mipango ijayo. Hivyo, ninawaomba Waheshimiwa Wabunge washirikiane kwa karibu na
Serikali kuhakikisha kuwa miradi iliyopangwa katika ngazi zote
inatekelezwa kwa ufanisi ili Mpango huu wa mwanzo utekelezeke kama
ilivyokusudiwa.
Mheshimiwa Spika,
22.
Mjadala
na Hoja nyingine zilijielekeza katika changamoto za upatikanaji wa Ajira
kwa Vijana Nchini. Kulingana na Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012, Asilimia
34.7 ya nguvu kazi ya Tanzania ni Vijana wa umri wa kati ya miaka 15
- 35. Kundi hili la Vijana ndilo lenye kiwango kikubwa cha ukosefu wa ajira
cha Asilimia 13.4 hapa Nchini. Pamoja na kuwa Vijana hawa wamekuwa
wakipata kazi hususan katika Sekta za Ujenzi, Kilimo na Hoteli, ajira zao
nyingi zimekuwa za muda.
23.
Katika
kukabiliana na changamoto hii, Serikali imeandaa Programu ya Ajira kwa Vijana
itakayotekelezwa kwa kipindi cha miaka mitatu. Malengo ni kupatikana fursa za
ajira 840,000 kwa kuwezesha jumla ya Miradi 10,000 ya Wahitimu wa
Elimu ya Juu wapatao 30,000 kutoka Vyuo mbalimbali ambao watatoa
ajira za moja kwa moja kwa wahitimu wengine 270,000 na ajira zisizo za
moja kwa moja 540,000. Programu hii itajengea Vijana uwezo katika stadi
za kazi; ujasiriamali; na kuwapatia Vijana mitaji, nyenzo na vifaa vya kufanyia
kazi; na kuwapatia Vijana maeneo ya uzalishaji na biashara. Serikali inatarajia
kuelekeza fedha zaidi katika kipindi husika ili kuwezesha utekelezaji wa
Programu hiyo. Aidha, naipongeza Sekta Binafsi kwa mchango wao mkubwa katika
kukuza uchumi wa Nchi na kuongeza ajira kwa vijana.
Mheshimiwa Spika,
24.
Kilimo
ni moja ya maeneo ya kipaumbele katika Mpango wa mwaka 2014/2015. Hili ndilo
eneo kubwa kwa maana ya kuongeza fursa za ajira na kipato kwa Wananchi
wanaoishi Vijijini, kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi kwa namna ambayo ni
shirikishi ili kupunguza umaskini. Hivyo, ili kujibu matatizo ya msingi
ya umasikini wa kipato Mpango wa Maendeleo 2014/2015 utatoa kipaumbele
katika mambo muhimu yafuatayo:
(i)
Utafiti
wa kilimo cha mazao, hususan katika uzalishaji wa mbegu bora, mifugo na uvuvi;
(ii) Kuimarisha huduma za
ugani kwa kilimo, mifugo na uvuvi na kuimarisha upatikanaji na matumizi
ya mbolea kwa ajili ya kilimo;
(iii) Kuimarisha Ushirika wa
Wakulima na Wafugaji;
(iv) Kuongeza fursa za mikopo
kwa wakulima, wafugaji na wavuvi ikiwa ni pamoja na kukamilisha uanzishwaji wa
Benki ya Kilimo mwezi Januari 2014;
(v)
Kuwezesha
upatikanaji wa masoko ya mazao ya kilimo, na mifugo;
(vi)
Kujenga
na kukarabati skimu za umwagiliaji;
(vii)
Upatikanaji
wa ardhi kwa kilimo na mifugo kwa kuongeza kasi ya upimaji wa ardhi; na
(viii) Kuendeleza shughuli za kuongeza
thamani ya mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi;
Mheshimiwa Spika,
25.
Mpango
wa Maendeleo huandaliwa katika ngazi zote Tano za Utawala kulingana na majukumu
ya Serikali ambazo ni:
Moja:
Vijiji
na Mitaa;
Pili:
Kata;
Tatu:
Mamlaka za Serikali za Mitaa (Halmashauri);
Nne:
Mikoa; na
Tano:
Wizara, Idara zinazojitegemea, Taasisi na Wakala wa Serikali.
Mamlaka husika katika ngazi zote zinatakiwa kuandaa
Mipango yao kwa kuzingatia maeneo ya vipaumbele kama yalivyoainishwa katika
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2014/2015. Mipango lazima ilenge
katika maeneo yenye kuleta matokeo makubwa na ya haraka hususan katika
kuchochea maendeleo ya maeneo mengine na Programu nyingine katika ukuaji wa
uchumi na kupunguza umaskini.
Katika kila ngazi, Wadau wengine kama vile Sekta Binafsi,
Asasi Zisizo za Kiserikali, Mashirika ya Dini na Washirika wa Maendeleo
washirikishwe kikamilifu. Wizara, Idara zinazojitegemea, Taasisi na Wakala wa
Serikali ziandae Mpango na kuuwasilisha Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango Wiki ya
Nne ya mwezi Januari, Mwaka 2014.
Katika ngazi za Mikoa na Wilaya, uandaaji uanze katika
ngazi ya Kijiji na Mtaa, Kata, Halmashauri na hatimaye kwenye Mkoa. Mpango
uliopitishwa na Mkoa uwasilishwe Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa na Wizara ya Fedha, Wiki ya Nne ya Mwezi Januari, 2014.
Mpango wa Maendeleo wa Taifa utajadiliwa na Bunge kuanzia Mwezi Aprili hadi
Juni, 2014 na utekelezaji wake utaanza Mwezi Julai 2014 hadi Juni 2015;
Mheshimiwa Spika,
26.
Mapendekezo
ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2014/2015 ndiyo yatatumika katika utayarishaji
wa Mipango ya Maendeleo ya Wizara, Idara za Serikali zinazojitegemea, Taasisi
na Wakala wa Serikali, Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa ya mwaka ujao wa
fedha 2014/2015. Hivyo, nawaomba Waheshimiwa Wabunge kutumia taarifa zilizotolewa
hapa Bungeni kutoa ufafanuzi kwenye Vikao vya Baraza la Madiwani katika
Halmashauri zao wakati wa kujadili Mipango yao. Aidha, napenda kutumia
fursa hii kuzihimiza Mamlaka za Serikali za Mitaa kuainisha vipaumbele
vinavyolenga katika maeneo yenye kuleta matokeo makubwa na ya haraka ya
Kiuchumi na Kijamii; na pia yenye kuchochea maendeleo ya maeneo mengine.
Vilevile, vipaumbele vya Halmashauri vilenge kufungulia fursa za ajira,
kuongeza mapato ya ndani na kuvutia uwekezaji wa Sekta Binafsi katika maeneo
yao.
V:
SEKTA YA KILIMO
a)
Hali ya chakula Nchini
Mheshimiwa Spika,
27.
Kwa ujumla hali ya
upatikanaji wa Chakula Nchini hadi kufikia Mwezi Oktoba 2013 ni ya kuridhisha
kufuatia mavuno mazuri ya msimu wa kilimo wa 2012/2013 ambapo mazao yake
yanaendelea kuingia sokoni kutoka maeneo mbalimbali hapa Nchini. Tathmini ya
awali iliyofanyika mwezi Julai/Agosti, 2013 inaonesha kuwa uzalishaji wa mazao
ya chakula katika Msimu wa kilimo wa 2012/2013 utafikia Tani 14,383,845
za chakula zikiwemo Tani 7,613,221 za mazao ya nafaka na Tani
6,770,624 za mazao yasiyo ya nafaka. Kiasi hicho cha chakula
kilichozalishwa ni ongezeko la Tani 2,234,726 za chakula, ikilinganishwa
na mahitaji ya chakula kwa mwaka 2013/2014 ya Tani 12,149,120. Kiwango hicho
kinajumuisha Tani 354,015 za mahindi na Tani 466,821 za mchele.
Hivyo napenda kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge na Wananchi kwa ujumla kuwa
tutakuwa na chakula cha kutosha Nchini kwa Asilimia 118.
Mheshimiwa Spika,
28. Vilevile, tathmini hiyo inaonesha kuwa, pamoja
na kuwepo kwa chakula cha kutosha na cha ziada, Halmashauri 61 katika
Mikoa ya Manyara, Shinyanga, Simiyu, Arusha, Dodoma, Lindi, Tanga, Singida,
Mara, Morogoro, Kilimanjaro, Mwanza, Pwani, Mtwara, Kigoma na Tabora
zinatarajiwa kuwa na uhaba wa chakula.
29. Natoa wito kwa Halmashauri zinazohusika katika
Mikoa hiyo kufuatilia kwa karibu utaratibu wa kupata chakula kinachotolewa
kutoka maeneo yenye ziada na kuhakikisha kuwa kinafika mapema kwenye maeneo yao
kabla Wananchi wa maeneo hayo hawajaanza kulalamika.
(b) Mwenendo wa Bei za Vyakula Nchini
Mheshimiwa Spika,
30. Kutokana na hali ya upatikanaji wa chakula
kuwa nzuri, Bei za wastani za vyakula hasa mahindi na mchele katika Soko Nchini
zimeendelea kushuka. Kwa mfano, bei ya mahindi ilishuka kutoka Shilingi
774.30 kwa kilo mwezi Februari, 2013 hadi Shilingi 535.40 kwa Kilo
mwezi Septemba 2013. Kwa upande wa mchele, bei kwa kilo moja imeshuka kutoka Shilingi
1,825.45 mwezi Februari, 2013 hadi kufikia Shilingi 1,206.70 mwezi
Septemba 2013, na bei ya mchele imeshuka zaidi hadi kufikia Shilingi 1,146.70
katika mwezi Oktoba, 2013.
(c)
Hali
ya Ununuzi na Akiba ya Chakula ya Taifa
Mheshimiwa Spika,
31.
Serikali kupitia
Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula imepanga kununua Tani 250,000 za
nafaka katika msimu wa 2013/2014. Hadi kufikia tarehe 23 Oktoba, 2013, Wakala
alikuwa amekwishanunua kiasi cha Tani 218,412 za nafaka sawa na Asilimia
87.37 ya lengo lililowekwa ambapo Tani 217,919 kati ya hizo ni za
Mahindi na Tani 493 ni za mtama. Aidha, hadi kufikia tarehe 23 Oktoba
2013, maghala ya Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula yalikuwa na jumla ya Tani
232, 921 za nafaka, kati ya hizo Tani 232,419 ni za mahindi na Tani
493,103 ni za mtama. Kiasi hiki cha nafaka kinajumuisha albaki
ya Tani 25,452 za mahindi kutoka msimu uliopita wa 2012/2013.
Mheshimiwa Spika,
32. Serikali inaendelea na tathmini ya kina ya
hali ya chakula na lishe katika Halmashauri 61 zilizoainishwa kuwa na
hali tete ya chakula kwa lengo la kubainisha idadi ya watu wenye uhaba wa
chakula ili kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa tatizo hili. Nitumie fursa hii kwa
mara nyingine tena kuwaagiza Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuwahimiza Wakulima hasa
walioko katika maeneo yenye chakula cha ziada kuhifadhi Chakula cha kutosha kwa
mahitaji ya Kaya zao. Aidha, Wakala wa Taifa na Hifadhi ya Chakula wajipange
vizuri kuhamisha Chakula kutoka maeneo yenye ziada na kupeleka kwenye maeneo
yaliyoainishwa kuwa na hali tete mara taarifa ya upungufu itakapotolewa.
Mheshimiwa Spika,
33.
Pamoja na juhudi za Serikali za kuhakikisha kwamba kuna chakula cha
kutosha, natambua Changamoto zilizopo katika ununuzi wa Chakula kupitia Wakala
wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula. Natambua kuwepo kwa madeni yanayotukabili
kwenye ununuzi wa nafaka kwa ajili ya Wakala yaani NRFA. Hata hivyo,
Mikoa inayohusika na madeni hayo ni Arusha, Dodoma, Njombe, Shinyanga,
Ruvuma, Rukwa na Tanga. Serikali itahakikisha deni hilo hilo
linalipwa ndani ya mwaka huu wa fedha 2013/2014.
(d)
Mpango wa Pembejeo za
Ruzuku
Mheshimiwa Spika,
34. Kama nilivyoeleza katika Mkutano wa 12 wa
Bunge, katika msimu wa 2013/2014 Serikali imetenga jumla ya Shilingi Bilioni
112.564 kwa ajili ya ruzuku ya mbolea, na pembejeo. Aidha, nilielezea
kuhusu utaratibu mpya wa kutoa ruzuku utakaohusisha uwiano wa Asilimia
80 kwa Vocha na Asilimia 20 mikopo. Ili kuhakikisha Mfumo huu mpya
unatekelezwa kikamilifu na kuleta matokeo yaliyotarajiwa, Serikali imetoa
mafunzo ya utoaji pembejeo kwa njia ya mikopo kwa Washauri wa Kilimo wa Mikoa,
Maafisa Ushirika wa Mikoa na Wilaya na Maafisa Kilimo wa Wilaya kwa awamu
mbili. Awamu ya kwanza ikihusisha Mikoa ya Shinyanga, Geita na Manyara; na
Awamu ya Pili inahusu Mikoa ya Ruvuma, Njombe, Mbeya na Iringa. Aidha,
uchambuzi wa takwimu za Vyama vya Ushirika na Vikundi vya Wakulima
watakaokopeshwa pembejeo za Kilimo mwaka 2013/2014 umefanyika katika Mikoa ya
Iringa, Ruvuma, Shinyanga, Njombe, Mbeya, Geita na Manyara. Takwimu
zinaonesha kuna SACCOS 214, AMCOS 163 na Vikundi vingine 51
vyenye Wakulima 88,290 watakopeshwa pembejeo za Kilimo. Natoa Wito kwa
Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika kuendeleza mafunzo haya kwa Mikoa
iliyobaki.
(e) Hali ya Usambazaji wa Vocha za Pembejeo
Mheshimiwa Spika,
35. Kuhusu hali ya Usambazaji wa Vocha za Pembejeo
katika Msimu wa 2013/2014 napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba, jumla ya
Vocha 2,796,300 kwa ajili ya Kaya 932,100 zikiwemo Vocha 932,100
za mbolea ya kupandia, 932,100 za mbolea ya kukuzia, Vocha 441,100
za mbegu za mahindi chotara; Vocha 432,000 za mahindi ya OPV na Vocha 60,000
za mbegu za mpunga zilisambazwa katika Mikoa yote hapa Nchini. Nitoe wito kwa
Viongozi wa Mikoa na Wilaya kwa kushirikiana na Waheshimiwa Madiwani na
Viongozi wengine kuhakikisha kuwa Wananchi wanapata na wanatumia Vocha hizi
kupata pembejeo kama ilivyokusudiwa. Aidha, tushirikiane kuhakikisha kuwa wale
watakaokwenda kinyume na utaratibu huu wa usambazaji wa Vocha hizo
wanashughulikiwa kwa mujibu wa Sheria.
(f)
Changamoto za Mbolea
ya Minjingu
Mheshimiwa Spika,
36.
Juhudi
za Serikali katika kuhakikisha upatikanaji wa Pembejeo za ruzuku ziko dhahiri.
Hata hivyo, imebainika kwamba katika mahitaji ya mbolea, kilio kikubwa
cha Wakulima ni kupatiwa mbolea kwa wakati. Aidha, wapo Wananchi
wanaolalamikia mbolea ya Minjingu Mazao ambayo ni kweli hapo awali ilikuwa na
matatizo. Lakini sasa, mbolea hii imeboreshwa kwa kiwango kikubwa kwa
kuongezewa virutubisho.
Mheshimiwa Spika,
37. Mbolea ya Minjingu ya awali ilikuwa na
virutubisho vya udongo viwili tu vya Kalisiumu na Fosfeti. Mbolea ya
Minjingu Mazao imeboreshwa kwa kuongezwa virutubisho vinne zaidi na kufanya
virutubisho hivyo kuwa sita yaani Kalisiumu, Fosfeti, Naitrojeni, Salfa,
Boroni na Zinki.
38. Kwa msingi huo, Mbolea ya Minjingu mazao
inaweza kutumika katika aina mbalimbali za udongo tofauti na ilivyokuwa awali.
Aidha, Mbolea ya Minjingu Mazao ni ya chengachenga (granulated) tofauti
na ya awali ambayo ilikuwa katika mfumo wa unga (dust) ambapo pengine
matumizi yake hayakuwa rafiki kwa mkulima. Baada ya kuboreshwa, kwa sasa Mbolea
hii ya Minjingu inatumika kwa mazao mengi hususan mahindi, mpunga na alizeti
katika sehemu mbalimbali na aina mbalimbali za udongo.
Mheshimiwa
Spika
39. Mkulima anahitaji kutumia mifuko miwili ya
mbolea ya Minjingu Mazao ya kilo 50 kila mmoja kwa wakati mmoja
ikilinganishwa na mfuko mmoja wa kilo 50 wa mbolea ya DAP. Hata
hivyo, ukilinganisha na mbolea ya DAP, mkulima anayetumia Minjingu Mazao
anawezesha shamba lake kupata virutubisho zaidi. Kwa hiyo, Mbolea ya Minjingu
Mazao ni nafuu ikilinganishwa na Mbolea ya DAP.
40. Bei ya mbolea ya Minjingu Mazao
kwa mfuko mmoja ni Shilingi 32,500/= hivyo kwa mifuko miwili ni Shilingi
65,000 katika Wilaya zote Nchini ikilinganishwa na bei ya wastani ya Shilingi 75,000/=
ya mfuko mmoja wa DAP. Aidha, kwa aina zote mbili za mbolea zinapotumika
kupandia, lazima mkulima aweke mbolea nyingine ya kukuzia ambayo ina
virutubisho vingi vya Naitrogeni kama CAN au UREA.
41. Majaribio ya kutumia Mbolea ya Minjingu
yalianza mwaka 1977 kuendelea hadi mwaka 2006 ikiwa katika hali ya unga. Mwaka
2007 Mbolea hiyo iliboreshwa kwa kuiweka katika hali ya chenga chenga (granulation)
ingawa virutubisho havikuboreshwa. Mbolea hiyo iliendelea kutumika katika hali
hiyo hadi mwaka 2009. Hivyo, mwaka 2010 Mbolea hiyo iliboreshwa kwa kuongezea
virutubisho ambavyo baada ya utafiti wa kuihakiki (validation)
iliingizwa Sokoni mwaka 2012.
42. Kwa sasa, Mbolea ya Minjingu Mazao inatumika
katika Mikoa ya Iringa, Ruvuma, Rukwa, Mbeya, Njombe, Katavi, Kigoma na
Morogoro. Aidha, kuna mikoa mingine ambako mbolea hii imepelekwa pamoja na
mbolea nyingine kwa ajili ya Wakulima wenyewe kufanya maamuzi ya kuchagua.
Mheshimiwa Spika
43. Matumizi ya Mbolea ya Minjingu Mazao katika
mwaka 2012/2013 yamewezesha kuongezeka kwa uzalishaji wa mahindi, mpunga na
alizeti kwa ekari hususan katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini. Changamoto
kubwa ni elimu juu ya matumizi sahihi ya Mbolea hiyo kwenye baadhi ya maeneo.
44. Katika kutatua changamoto hii, Wizara
inashirikiana na Mmiliki wa Kiwanda cha Mbolea cha Minjingu kuendesha mashamba
darasa katika Wilaya mbalimbali Nchini. Vilevile, Wizara ya Kilimo kwa
kushirikiana na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo, inaendelea kufanya utafiti
katika maeneno mbalimbali ya Nchi ili kuboresha matumizi sahihi ya Mbolea hiyo
katika aina mbalimbali za udongo (site specific validation trials).
45. Changamoto zinazohusiana na Mbolea ya Minjingu
katika Wilaya ya Mbozi zitaangaliwa kwa namna yake. Kitendo hicho ni cha
udanganyifu kwani Mbolea ya aina nyingine ni bei kubwa ikilinganishwa na ya
Minjingu Mazao. Kutokana na kitendo hicho kuwa kinyume na Sheria ya Mbolea ya
2009, Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea kwa kushirikiana na Wakaguzi wa mbolea wa
Wilaya ya Mbozi ilimkamata Wakala husika na kumchukulia hatua za kisheria.
Naagiza Viongozi wa Mikoa na Wilaya kuchunguza mbolea inayopelekwa katika
maeneo yao isije ikachakachuliwa.
Mheshimiwa Spika,
46.
Kwa kuzingatia Changamoto zilizojitokeza katika matumizi ya mbolea ya
Minjingu katika maeneo mbalimbali Nchini Serikali itaendelea kuzitafutia
ufumbuzi kwa kuchukua hatua zifuatazo:
(a)
Kutoa elimu kwa Wakulima kuhusu namna bora ya kutumia Mbolea ya Minjingu
Mazao kuongeza uzalishaji wa mazao kwa kuzingatia ushauri wa kitaalam kuhusu
aina ya udongo na mazao yanayofaa kwa mbolea hiyo. Vilevile, kuwaelimisha
Wananchi kuhusu ubora wa Mbolea ya Minjingu Mazao ikilinganishwa na Mbolea za
aina nyingine hasa kutokana na virutubisho vilivyoongezwa katika mbolea.
(b)
Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea imeagizwa kufuatilia na kufanya uchunguzi wa
madai ya Wakulima kuhusu changamoto za matumizi ya mbolea ya Minjingu Mazao
hasa katika Wilaya ya Mbozi na sehemu nyingine zenye matatizo ya matumizi ya
mbolea hiyo Nchini.
(c)
Naomba kuiagiza Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika kuendelea
kushirikiana na Wadau kufanya utafiti katika maeneo mbalimbali Nchini. Kutokana
na utafiti huo itoe ushauri na mwongozo kwa Wakulima wote Nchini kuhusu njia
sahihi za kutumia Mbolea ya Minjingu Mazao katika aina mbalimbali za udongo na
mazao yanayofaa kulimwa. Lengo ni kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao ya
kilimo kwa eneo. Kwa Wilaya ya Mbozi Wizara itoe mwongozo kuhusu nini
kifanyike kwa sasa wakati hatua za utafiti na uchunguzi wa matumizi sahihi ya
Mbolea hiyo zinaendelea.
(g)
Uzalishaji na Ununuzi wa Mazao ya Biashara
Mheshimiwa Spika,
47. Katika miaka ya hivi karibuni kumekuwa na
Changamoto mbalimbali za uzalishaji na ununuzi wa baadhi ya mazao ya biashara
hapa Nchini ikiwemo Kilimo cha zao la Pamba, Korosho, Tumbaku na Kahawa. Kwa
kuzingatia ufinyu wa muda, leo naomba mniruhusu nizungumzie kidogo kuhusu
kilimo cha mazao mawili ya Pamba na Korosho.
(h) Uzalishaji na Ununuzi wa Zao la Pamba
Mheshimiwa Spika,
48. Serikali inaendelea na
jitihada za kuhakikisha kuwa Wakulima wa Pamba wanazalisha kwa tija kwa
kutumia mbegu bora, utumiaji wa pembejeo (Viuadudu na Mbegu), kutoa
huduma za ugani kupitia Maafisa wa Kilimo katika Halmashauri za
Wilaya na pia kuhamasisha Kilimo cha pamba kwa kushirikiana kwa karibu na Wadau
mbalimbali ikiwemo Sekta Binafsi.
49. Katika kilimo hiki cha
Pamba, Zana za kilimo zinazotumika kwa sasa ni majembe ya kukokotwa na wanyama
kazi kwa ajili ya kulima nah ii ni dhahiri haiwezi kuongeza tija. Ttahakikisha
tunatumia Zana za Kisasa.
(i)
Mkakati
wa Wizara kupata masoko ya uhakika ya pamba
50.
Serikali
pia inaendelea kuhakikisha kwamba pamba inaongezwa thamani hapa Nchini kwa
kuhamasisha uwekezaji katika ujenzi wa viwanda vya nyuzi na nguo. Uwekezaji
mpya unafanyika kwa kujenga kiwanda cha nyuzi na nguo cha Dahong Mkoani
Shinyanga na pia Mradi mkubwa wa kuzalisha pamba, kuchambua, kutengeneza nyuzi,
kutengeneza vitambaa na nguo unaotarajiwa kutekelezwa na Kampuni ya
Kijapani (NITORI) katika Wilaya ya Handeni. Kwa sasa mradi huo uko katika hatua
ya umilikishwaji wa Ardhi.
51.
Vilevile,
Serikali imeanzisha mafunzo ya Uhandisi na Ubunifu katika Viwanda vya Nyuzi na
Nguo. Pia tumeanzisha kozi ya ubunifu wa mitindo katika mitaala ya VETA na
Mafunzo ya Shahada ya uzamili katika “Textile” katika Chuo Kikuu cha Dar
es Salaam. Lengo ni kuhakikisha kuwa kuna watalaamu wa kutosha katika mchakato
wa kuongeza thamani ya pamba.
(j)
Tofauti
za ubora wa mbegu za pamba manyoya na De – linted
Mheshimiwa Spika,
52. Sina shaka Watanzania
wameshasikia kuwa kwa sasa tunazo aina mbili za mbegu za Pamba zinazotumika
hapa Nchini. Tunayo mbegu yetu ya asili ya Pamba Manyoya na Mbegu mpya na
ya kisasa ya Pamba isiyo na manyoya (De-linted). Aina hizi zinatofautiana
sana kwa ubora na bei. Mbegu ya manyoa ina uotaji wa chini ya Asilimia 50
wakati ile ya De –linted ni zaidi ya Asilimia 90. Mbegu ya manyoya hutumika
nyingi kwa eneo (kilo 25 kwa Ekari), wakati De – linted ni kilo 6 tu kwa
Ekari, sawa na Shilingi 7,200 kwa Ekari kwa bei ya Shilingi 1,200
kwa kilo. Mbegu ya manyoya ina tija ndogo (inazalisha kati ya kilo 250
na 300 kwa Ekari) ikilinganishwa ya mbegu ya De-linted inayozalisha Kilo 450 –
1200 kwa Ekari. Mbegu ya manyoya ina uwiano mdogo wa pamba nyuzi (Asilimia 33)
ikilinganishwa na mbegu De-linted ambayo uwiano wake ni Asilimia 36.
(k)
Jitihada
za Wizara kupunguza bei ya mbegu bora
Mheshimiwa Spika,
53. Ili kuwawezesha
Wakulima kutumia mbegu bora (de-linted) Serikali imetoa ruzuku ya Shilingi
Billioni 4.8 ili kufanya mbegu hiyo ipatikane kwa Shilingi 600
kwa kilo kwa mkulima badala ya Shilingi 1,200 kwa kilo iliyotumika mwaka
2012/2013.
54. Serikali pia
inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kutoa elimu kwa wakulima wa pamba
kuhusu mbegu bora. Kwa mfano, Viongozi wa maeneo yanayolima pamba (Wakuu wa
Mikoa, Wakuu wa Wilaya na baadhi ya Madiwani) wamepelekwa katika kiwanda
cha kuchakata mbegu bora za Pamba cha Kampuni ya Quton ili kupata
maelezo na kujionea hali ya utendaji wa mbegu bora katika kilimo.
55. Kupitia programu ya
kuendeleza zao la pamba wakulima wawezeshaji (Lead Farmers) 3000 wa
vikundi vya Kilimo cha Mkataba wanaendelea kupewa mafunzo ya kilimo bora na
matumizi ya mbegu bora ili watumike kupeleka elimu hii kwa wakulima wenzao.
Mheshimiwa Spika,
56. Katika msimu huu wa
Kilimo wa 2013/14, Serikali imejipanga kusimamia utekelezaji wa Kilimo cha
Mkataba kwa lengo la kuleta ufanisi katika Kilimo cha Pamba Nchini. Hatua hii
inahusisha pia kutoa elimu ya kutosha na kushirikisha kwa
karibu Wadau katika kuzipatia ufumbuzi changamoto zilizopo kwenye
utaratibu mzima wa kilimo hicho ambacho kina manufaa makubwa iwapo kitaeleweka
na kutekelezwa vyema kwa misingi ya haki miongoni wa wadau. Baadhi ya manufaa
hayo ni:
(i)
Uhakika
wa upatikanaji wa pembejeo kwa mkulima kwa mkopo.
(ii) Kuongeza tija kutokana na
kupata pembejeo na huduma za ugani.
(iii) Kuongeza ubora wa pamba
kutokana na matumizi makubwa ya pembejeo na huduma za ugani pamoja
na vikundi kutumika kama Mawakala wa kununua Pamba ya wanachama wake hivyo
kusimamia ubora
(iv) Uhakika wa soko la
pamba ya mkulima
(v) Kupunguza wizi kupitia
mizani ya mawakala
(vi)
Wakulima
kupata teknolojia kupitia uwekezaji
(vii) Kujenga na kuimarisha
mfumo wa Ushirika kupitia vikundi vya wakulima.
(l)
Elimu
ya kilimo cha mkataba kwa wakulima
Mheshimiwa Spika,
57. Kupitia programu
ya kuendeleza zao la pamba, wakulima Wawezeshaji zaidi ya 3,000
wamekwisha pokea mafunzo ya kilimo cha Mkataba wanao tumika kupeleka elimu hii
kwa vikundi vya wakulima. Wagani wa Halmashauri wapatao 560 wameshapata
mafunzo haya. Chini ya Mpango huu kila mgani anaweza kuhudumia vikundi
hadi 20.
58. Napenda kuwaagiza Viongozi na
Wataalamu wa Kilimo waendelee kutoa elimu ya matumizi na faida ya mbegu bora za
De-linted au mbegu zisizokuwa na manyoya kwa Wakulima wa Pamba Nchini. Aidha,
mashamba darasa yatumike ipasavyo kuonesha tija inayotokana na aina hiyo ya
mbegu za Pamba inapolinganishwa na mbegu zenye manyoya. Vilevile,
Viongozi na Wataalamu wa Kilimo waendelee kuwakumbusha Wakulima wa Pamba na
Watanzania kuwa utaratibu mpya wa Kilimo cha Mkataba una manufaa mengi na
makubwa. Tuendelee kuwashawishi Wakulima kujiunga na Kilimo cha Mkataba
bila kuwashurutisha isipokuwa tuwape elimu hasa kupitia mashamba darasa.
Wale watakaoshawishika kuingia katika utaratibu huu wasaidiwe kwa kila hali ili
wanufaike na kilimo hicho huku wakisaidia kutoa elimu kwa Wakulima wengine ili
wajiunge na aina hii ya kilimo. Ni matumaini yangu ndani ya muda mfupi Wakulima
watafahamu faida ya kilimo cha mkataba.
(m)
Zao la Korosho
Mheshimiwa Spika,
59. Kuhusu Zao la Korosho, azma ya Serikali ni
kuimarisha Viwanda vya Korosho na kufufua vile vilivyopobinafsishwa ili viweze
kusaidia kukuza Soko kwa wakulima wa Korosho. Ili kutekeleza azma hiyo,
Serikali imefanya tathmini na kubaini kuwa Wawekezaji wengi katika Viwanda vya
Korosho vilivyobinafsishwa wameshindwa kutekeleza Mikataba ya Ubinafsishaji wa
viwanda hivyo kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo ukosefu wa fedha za
uendeshaji, ukosefu wa nishati ya uhakika na Viwanda kutumia teknolojia
zilizopitwa na wakati. Ili kukabiliana na hali hiyo, Wizara ya Kilimo, Chakula
na Ushirika kwa kushirikiana na Shirika Hodhi la Mali za Mashirika ya Umma
(CHC) pamoja na Wadau wengine inaandaa mapendekezo ya hatua za kuchukua dhidi
ya Wawekezaji walioshindwa kuendeleza viwanda hivyo. Dhamira ya Serikali ni
kwamba Mwekezaji ambaye ameshindwa kuendeleza kiwanda alichonunua kwa
kuzingatia Makubaliano ya ununuzi na Serikali, mali hiyo irudishwe Serikalini
na ifanyiwe tathmini na itangazwe upya ili kupata Wawekezaji mahiri na wenye
nia thabiti ya kuendeleza Viwanda husika.
Mheshimiwa Spika,
60. Sambamba na hatua hiyo, Bodi ya Korosho
Tanzania imeandaa Mpango wa Ubanguaji wa miaka mitatu kuanzia mwaka 2012/2013
ambao umelenga kuwasaidia wabanguaji wadogo na wa kati kuendesha shughuli za
ubanguaji kwa ufanisi kwa kuwapatia mafunzo, vifaa vya kubangulia, na
kuwatafutia masoko ya ndani, masoko ya kanda na masoko ya nje;
61. Hatua iliyofikiwa kwa sasa ni kwamba, Mfuko wa
Wakfu wa Kuendeleza Zao la Korosho kwa kushirikiana na Bodi ya Korosho Tanzania
umetenga fedha kwa ajili ya kujenga viwanda vitatu katika Mikoa ya Ruvuma,
Mtwara, na Pwani kwa ajili ya kuwawezesha Wabanguaji wadogo na wa kati
kumalizia baadhi ya hatua za ubanguaji katika viwanda hivyo kwa ajili ya
kukidhi matakwa ya masoko makubwa ya korosho duniani.
Mheshimiwa Spika,
62. Ili kuboresha kilimo cha Korosho, katika mwaka
2013/2014, Serikali itaendelea kutoa ruzuku ya madawa kutoa huduma za ugani na
kuhamasisha wakulima wahudumie mikorosho na kupuliza madawa mapema.
Mheshimiwa Spika,
63. Kuhusu ununuzi wa Korosho, katika msimu huu wa
2013/2014 ununuzi wa Korosho utaendelea kwa kutumia mfumo wa Stakabadhi za
mazao Ghalani. Ukusanyaji wa Korosho kutoka kwa wakulima umeanza katika maeneo
mbalimbali Nchini. Kwa mfano, katika Mkoa wa Mtwara, mnada wa kwanza wa Korosho
ulianza tarehe 25 Oktoba, 2013 ambapo ulihusisha Vyama vya Msingi vya Mkoa wa
Mtwara. Korosho zote zilizokuwa zimekusanywa na kutangazwa katika kila mnada
zilinunuliwa. Bei ya Korosho katika Mnada wa kwanza ilikuwa kati ya Shilingi 1,402/=
na 1,520/= kwa kilo ikilinganishwa na bei dira ya Shilingi 1,000/=
kwa kilo. Mnada uliofuatia bei ziliongezeka na kuwa kati ya Shilingi 1,481/=
na 1,570/= kwa kilo.
Mheshimiwa Spika,
64. Kwa upande wa Mkoa wa Lindi, Vyama vya Msingi
vilivyobaki chini ya ILULU vilifanya Mnada wa kwanza tarehe 2 Novemba, 2013
ambapo jumla ya Tani 783.593 ziliuzwa. Vyama vingine 51 vya kutoka
Wilaya ya Ruangwa, Nachingwea na Liwale ambavyo vilijiondoa kutoka usimamizi wa
Chama Kikuu cha ILULU vitafanya mnada baada ya taratibu za kupata Kamati
itakayowasimamia zitakapokamilika. Vyama hivyo vimeomba kufanyiwa Minada yake
katika Wilaya ya Nachingwea ambako ndiko walikoweka Ofisi yao.
Mheshimiwa Spika,
65. Kwa upande wa Wilaya ya Tunduru, bado
haijapata mkopo mpaka sasa na juhudi za kufuatilia zinaendelea. Taarifa kutoka
Benki ya NMB inaonyesha kuwa kuna uwezekano mkubwa wa Vyama vya Msingi vya
TAMCU kupata mkopo msimu huu kwani deni ambalo TAMCU walikuwa wanadaiwa na
Benki hiyo ya NMB limelipwa na Serikali.
Mheshimiwa Spika,
66. Kwa upande wa Mkoa wa Pwani, uwezekano wa
Vyama vilivyo chini ya Chama Kikuu cha Coast Region Cooperative Union (CORECU)
kupata Mkopo ni mdogo kutokana na kudaiwa fedha nyingi zaidi ya Shilingi Bilioni
7 za msimu wa mwaka 2010/2011. Serikali imefanya Ukaguzi Maalum katika
Vyama hivyo na kubaini kwamba madeni hayo kwa kiwango kikubwa yamesababishwa na
ubadhirifu wa Viongozi na Watendaji wa Vyama hivyo. Hivyo, kupitia Ofisi ya
Mrajis wa Vyama vya Ushirika hatua za kisheria zimechukuliwa ikiwa ni pamoja na
kuwataka wahusika wa ubadhirifu huo kufidia hasara hiyo. Kwa upande mwingine,
Wahusika wamekata rufaa, lakini Mamlaka yenye dhamana imezitupilia mbali rufaa
hizo zote 434, na kuwataka Wahusika walipe kiasi cha fedha kinachodaiwa
na Vyama vyao. Kutokana na hali hiyo, Wakulima wa Mkoa wa Pwani wanashauriwa
kupeleka mavuno ya Korosho katika maghala yaliyoteuliwa. Minada ya Korosho
itafanyika katika maghala hayo na wakulima watalipwa mara moja baada ya minada
kufanyika.
Mheshimiwa Spika,
67. Kutokana na jitihada za Serikali zinazoendelea
natoa wito kwa Bodi ya Korosho na Wakuu wa Mikoa husika kuendelea kusimamia
kikamilifu taratibu wa ununuzi wa Korosho ili kuhakikisha kwamba Wakulima
wanauza Korosho zao walizovuna na kulipwa malipo yao halali kwa wakati.
(n) Hali ya mwenendo wa Mvua za vuli mwaka 2013 na
athari kwa mazao ya vuli
Mheshimiwa Spika,
68. Taarifa ya utabiri wa mwelekeo wa hali ya hewa
hususan mvua katika kipindi cha Oktoba hadi Disemba 2013 iliyotolewa na Mamlaka
ya Hali ya Hewa Nchini inaonesha kuwa mvua za vuli zinatarajiwa kuwa chini ya
wastani katika Mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Tanga, Kaskazini mwa Morogoro,
Kilimanjaro, Arusha, Manyara na baadhi ya maeneo katika mikoa ya Mwanza,
Simiyu, Shinyanga Kagera, Geita na Mara. Pamoja na kwamba mvua za msimu wa vuli
zimechelewa kuanza katika maeneo mengi ambayo yalitarajiwa kupata mvua za vuli,
mvua hizi hazitarajiwi kuwa na mtawanyiko wa kuridhisha.
(o)
Athari za mvua za vuli
zinazonyesha chini ya Wastani
Mheshimiwa Spika,
69. Kutokana na utabiri huo wa Hali ya Hewa, tathmini ya awali
iliyofanyika katika maeneo yaliyotarajiwa kupata mvua za vuli inaonesha kuwa:
i. Hali ya mazao hasa katika
Nyanda za juu Kaskazini na ukanda wa Pwani Kaskazini si ya kuridhisha,
ii. Mategemeo ya mavuno ya
vuli ni kidogo isipokuwa katika baadhi ya maeneo ya ukanda wa Ziwa Viktoria
hususan katika Mikoa ya Kagera na Geita ambayo yamepata mvua za wastani hadi
chini ya wastani,
iii. Mchango wa mavuno ya vuli
ambao ni kati ya Asilimia 28-30 ya Chakula kinachozalishwa katika maeneo
yanayopata mvua hizo au Asilimia 18 Kitaifa hauwezi kufikiwa katika hali
hii ya mvua.
iv. Hali hii inaashiria kuwa
kutakuwepo na upungufu wa Chakula katika maeneo hayo niliyotaja hapo juu.
Mheshimiwa Spika,
70. Kutokana na hali hii, natoa wito kwa Wakulima
katika maeneo haya kuzingatia ushauri wa kupanda mazao yanayostahimili ukame na
yanayokomaa kwa muda mfupi. Wakuu wa Mikoa na Wilaya katika Halmashauri husika
wasimamie suala hili kwa ukamilifu; ili kuepusha upungufu wa Chakula
unaotarajiwa.
VI:
NISHATI
(a)
Kuongezeka kwa upatikanaji wa Nishati Vijijni (Miradi ya REA) na hali
iliyofikiwa
Mheshimiwa Spika,
71.
Wakati wa Kuhitimisha
Mkutano wa 12 wa Bunge nilieleza Mikakati ya Serikali katika kueneza umeme
Vijijini na matarajio ya baadaye. Napenda kulieleza Bunge lako Tukufu kwamba
tumeweza kupiga hatua katika baadhi ya maeneo katika kuelekea kwenye malengo
tuliyojiwekea. Tayari Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ulitangaza zabuni
mwezi Desemba 2012 kwa ajili ya kuwapata Wakandarasi wa kupeleka umeme Vijijini
na kujenga vituo vya kupoozea umeme. Baada ya tathmini kufanyika, zabuni 15 za
kupeleka umeme Vijijini zilipata Wakandarasi. Mikoa ambayo ilipata
Wakandarasi katika awamu hiyo ni pamoja na Arusha,
Dodoma, Iringa, Katavi, Kilimanjaro, Mara, Mtwara, Mwanza, Njombe,
Ruvuma, Shinyanga, Simiyu, Singida na Tabora. Aidha
Wakandarasi kwa ajili ya ujenzi wa
vituo vya kupozea umeme vya msongo wa Kilovoti 11 na 33 vya Ngara,
Kibondo, Kasulu, Kigoma, Tunduru na Mbinga
walipatikana. Kwa sasa Wakala unaendelea na kulipa malipo ya awali (advance
payments) na Wakandarasi wanaendelea na ukamilishaji wa taratibu za kuanza
kazi. Miradi
hii yenye thamani ya Shilingi Bilioni 430.82 inatarajiwa kukamilika
mwezi Juni, 2015.
Mheshimiwa Spika,
72. Mwezi Mei, 2013 zabuni
nyingine 10 ya Miradi yenye thamani ya Shilingi Bilioni
450 zilitangazwa kwa ajili yakuwapata Wakandarasi
wa kupeleka umeme Vijijini katika Mikoa ya Geita,
Kagera, Kigoma, Lindi, Manyara, Mbeya, Morogoro, Pwani, Rukwa
na Tanga. Kwa sasa tathmini ya zabuni hizo inaendelea. Inatarajiwa
kwamba Wakandarasi kutokana na Tathmini hiyo watajulikana ifikapo tarehe 15
Novemba, 2013.
(b) Suala la Fidia, Sera; na
Miongozo ya usambazaji Umeme Vijijini:
Mheshimiwa Spika
73. Ili kuharakisha maendeleo ya upatikanaji wa
Nishati Vijijini, suala la Wananchi kuchangia nguvu kazi na kutoa njia na
maeneo ya kupitisha nyaya za umeme bila fidia pale
inapowezekana limekuwa likisititizwa na Serikali kutokana na ufinyu wa bajeti.
Upo ukweli kwamba, Miradi mingi imechelewa kutekelezwa kutokana na Wananchi
kudai fidia ya miti na mazao ya msimu yanayokutwa kwenye njia ya umeme.
Kwa mfano miradi ya Awamu ya Kwanza katika Mkoa wa Pwani imechelewa kuanza na
kukamilishwa kutokana na Wananchi kudai fidia ilipwe kwanza ndio ujenzi
uendelee. Pia, kwa sasa ujenzi umesimama katika maeneo ya Bungu-Nyamisati na
Kisiwa cha Mafia kutokana na Wananchi kudai fidia kwanza.
Mheshimiwa Spika,
74. Ni kweli kwamba kulingana na Sheria zilizopo
kama katika njia ya kupitisha umeme yapo mazao yanayostahili kulipwa fidia.
Hata hivyo kutokana na bajeti finyu Wakala wa Nishati Vijijni unashindwa kutoa
fidia inayohitajika na kuona ni bora wale wanaojitolea maeneo yao wapelekewe
umeme haraka kuliko kusubiri bajeti kwa ajili ya fidia. Serikali inatoa rai kwa
Viongozi na Wananchi kuona umuhimu wa kujitolea maeneo yao ili waweze kupata
huduma hii muhimu mapema. Nawaomba Waheshimiwa Wabunge tushirikiane katika
kuwahamasisha Wananchi katika maeneo yetu kuhusu umuhimu wa kupata umeme mapema
kwa maendeleo ya maeneo yetu.
(c) Utekelezaji wa Ujenzi wa Bomba la Gesi Asilia
kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam
Mheshimiwa Spika,
75.
Shughuli za ujenzi wa
Bomba la Gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam zinaendelea vizuri. Mpaka sasa usafishaji wa
njia ya kulaza bomba unaendelea na tayari Kilometa 484.17 kati ya
Kilometa 517 zimekamilika. Aidha jumla ya mabomba 20,491
yanayotosheleza kulazwa umbali wa Kilometa 243.8 yamekwishawasili
Nchini. Kazi ya kuchimba mtaro, kuyapanga mabomba katika mstari mmoja kwenye
mkuza na kuyaunganisha pamoja kwa kuchomelea inaendelea na hadi sasa Kilometa 124.3
zimeshaunganishwa. Kazi zinazoendelea ni ujenzi wa kambi, nyumba za wafanyakazi
katika maeneo ya Songo Songo na Madimba, pamoja na maandalizi ya ujenzi wa
mitambo ya kusafirishia Gesi Asilia. Tutaendelea kutoa taarifa ya hatua
iliyofikiwa ya utekelezaji wa Mradi huu muhimu kwa Taifa letu.
76.
Aidha,
katika kuhakikisha kwamba miradi hii inatekelezwa na kuleta manufaa katika Nchi
yetu, ninayo furaha kulijulisha Bunge lako Tukufu kuwa, Serikali ilipitisha
Sera ya Gesi Asilia tangu tarehe 10 Oktoba 2013, Utaratibu wa kuichapisha sera
hiyo katika lugha ya Kiswahili na Kiingereza unaendelea. Vilevile Serikali
kupitia Wizara ya Nishati na Madini imeandaa Mpango Mkakati wa Miaka Mitano wa
Utekelezaji wa Sera ya Gesi na imeanza kutayarisha Rasimu ya Sheria ya Gesi. Ni
matumaini yangu kwamba vitu vyote hivi vikikamilika Sekta ya Gesi Asilia
itaimarika.
VII: MIFUGO
(a) Operesheni Ondoa Mifugo
Katika Maeneo Mbalimbali Nchini
Mheshimiwa Spika,
77.
Kwa muda mrefu sasa
maeneo mbalimbali hapa Nchini yamekuwa yakikumbwa na migogoro inayotokana na
matumizi ya Ardhi hususan kwa Wafugaji wanaohama kutoka maeneo yaliyokatazwa
kisheria kwenda eneo lingine pasipo na maandalizi ya kutosha ya kuwapokea. Utafiti unaonesha kuwa,
migogoro ya ardhi hapa Nchini ina sura nne:
Moja:
Migogoro kati ya Wakulima na Wafugaji,
Pili:
Migogoro kati ya Wananchi na Wawekezaji,
Tatu:
Migogoro kati ya Wananchi na Serikali, na
Nne:
Migogoro kati ya Mamlaka moja na Mamlaka nyingine ndani ya Serikali inayotokana
na migongano ya kimaslahi.
Mheshimiwa Spika,
78.
Kuna ukweli kwamba,
kuongezeka kwa idadi ya Watu na kuongezeka kwa matumizi ya ardhi kutaendelea
kuongeza kasi na vipaumbele katika kugawa maeneo yaliyoko wazi. Hali hii imeanza
kuonekana katika maeneo ya Wafugaji ambayo yameendelea kupungua siku hadi siku.
Aidha, shughuli za kilimo, maendeleo ya makazi, na matumizi mengine ikiwa ni
pamoja na kuongezeka kwa Vijiji kunakotokana na ongezeko la idadi ya watu
kumeendelea kupunguza eneo la malisho.
Mheshimiwa Spika,
79. Kuna ukweli pia kwamba, mabadiliko ya
tabianchi na kuongezeka kwa mifugo katika maeneo ya Nchi kwa ajili ya kutafuta
malisho na maji kumeendelea kuchangia migogoro mingi kati ya wafugaji na
watumiaji wengine wa ardhi. Kati ya mwaka 2005 na sasa, tumeshuhudia uhamiaji
wa mifugo kutoka mikoa ya Kaskazini na Kanda ya Ziwa kwenda katika Mikoa ya
Kusini na Mashariki mwa Nchi. Uhamiaji huo licha ya kusababisha migogoro kati
ya watumiaji wengine pia imesababisha uharibifu mkubwa wa mazingira kwenye
maeneo ya vyanzo vya maji na hifadhi za Taifa. Baadhi ya maeneo hayo ni pamoja
na hifadhi za Wanyama pori za Burigi, Maswa na Meatu, Bonde la Usangu na Bonde
la Kilombero.
Mheshimiwa Spika,
80. Ni matumaini yangu kwamba, maadam suala hili
limepewa umuhimu na Bunge lako Tukufu na hivyo kuunda Kamati ya kufuatilia
migogoro hii, ni dhahiri tutapata ufumbuzi wa kudumu katika tatizo hili.
Niwaombe Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote kwa ujumla wanaotoka katika
maeneo yenye migogoro inayotokana na Wafugaji na Wakulima kutoa ushirikiano
katika kutoa taarifa muhimu kwa Kamati iliyoundwa ili kulisaidia Taifa katika
kutatua migogoro hii.
VIII: HALI YA ULINZI NA
USALAMA NCHINI.
Mheshimiwa Spika,
81.
Kwa ujumla hali ya
Ulinzi na Usalama Nchini imeendelea kuwa shwari, isipokuwa katika maeneo
machache ambako kulijitokeza vitendo vinavyoashiria kuwepo kwa vikundi vya
uhalifu na ujambazi. Serikali kupitia Jeshi la Polisi imeendelea
kujipanga kukabiliana na matishio mbalimbali ya kiusalama ikiwemo ugaidi. Tukio
lililotokea Nchini Kenya hivi karibuni na matukio ya kukamatwa kwa Vijana 12
kule Mtwara na lile lililotokea Wilaya ya Kilindi Mkoani Tanga ambapo zaidi ya
watuhumiwa 46 wamefikishwa mahakamani kwa makosa mbalimbali yanaashiria
kwamba ugaidi hauna mipaka unaweza kutokea katika Nchi yoyote.
Mheshimiwa Spika
82.
Katika
kuhakikisha kuwa amani na utulivu vinaendelea kudumu Nchini, Serikali
imejipanga katika maeneo hayo kama ifuatavyo:
(i) Kuhakikisha Vikao vya
Kamati za Ulinzi na Usalama vya Mitaa, Vijiji na Vitongoji vinafanyika mara kwa
mara kwa mujibu wa Sheria na Kanuni za Serikali za Mitaa katika kila
Kata/Shehia kwa kuwashirikisha madiwani ili kujadili na kubaini kero mbalimbali
na kuzitafutia ufumbuzi.
(ii) Kufufua mpango wa Daftari
la Wakazi na Wageni katika kila Mtaa/Kitongoji kwa Tanzania Bara na Zanzibar
ili kila Kiongozi wa Mtaa, Kijiji na Kitongoji ajue Watu wanaoishi katika
himaya yake. Zoezi hili litasaidia kuepuka tatizo la wageni wasiojulikana au
wahamiaji haramu. Aidha kamati za Ulinzi na Usalama za Serikali za Mitaa na
Vijiji zinahimizwa kutekeleza mkakati wa Halmashauri wa kuzuia uhalifu kwa
kuimarisha vikundi vya ulinzi shirikishi/ulinzi jirani, kwa kuzingatia Sheria
ya Serikali za Mitaa na Sheria Ndogo zilizotungwa ili kuimarisha usalama katika
Halmashauri husika.
(iii) Kuhimiza wafanyabiashara
wasaidiane na vikundi vya ulinzi shirikishi/ulinzi jirani vilivyo kwenye maeneo
jirani na biashara zao kama sehemu ya kuimarisha usalama wa maeneo yao ya
biashara. Pia, kwa wafanyabishara wenye biashara kubwa zenye mikusanyiko ya
Watu wengi wanaagizwa kufunga “CCTV Camera” na kuziunganisha kimtandao na “Control
Room” ya Polisi ili kutoa msaada wa kuzuia na kutanzua mapema uhalifu
wowote utakaojitokeza.
(iv) Kuendelea kuunda Zonal
Task Force za Jeshi la Polisi katika kila Tarafa/Jimbo ili kukusanya
taarifa za uhalifu na kufanya operesheni za kuzuia uhalifu katika kila Kata au
Shehia zilizo ndani ya Tarafa husika. Kwa kufanya hiovyo tutaokoa maisha ya watu wengi.
(v) Kuendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu mbinu
mbalimbali za kuzuia na kupambana na uhalifu kwa kutumia vyombo mbalimbali vya
habari, mihadhara, mikutano, maonesho na usambazaji wa machapisho na
vipeperushi.
Mheshimiwa Spika,
83.
Jukumu
la kuhakikisha Ulinzi na Usalama katika Nchi yetu ni letu sote. Kila
Mwananchi popote alipo anawajibika kushiriki kwa vitendo kwa kubaini vitendo
vyovyote vya uhalifu katika sehemu za kazi, biashara na maeneo
tunamoishi. Wito wangu kwa Waheshimiwa Wabunge wote, ni kuwaomba
tuwahimize Wananchi kushiriki kikamilifu katika kuhakikisha Nchi yetu inadumu
katika hali ya Amani na Utulivu.
IX:
HITIMISHO
Mheshimiwa Spika,
84. Kwa kuhitimisha, naomba nitumie nafasi hii ya
mwisho kuwashukuru wote waliosaidia kufanikisha Mkutano huu. Kipekee
nikushukuru wewe Mheshimiwa Spika, pamoja na Naibu Spika kwa kutuongoza
vizuri. Niwashukuru Wenyeviti wa Bunge kwa kazi nzuri ya kuongoza vikao
vya Bunge lako Tukufu. Aidha, niwashukuru tena Waheshimiwa Wabunge kwa
kazi nzuri na kwa michango mbalimbali wakati wa Mkutano huu. Namshukuru Katibu
wa Bunge na Wasaidizi wake wote pamoja na Wataalam wote wa Serikali na Taasisi
zake ikijumuisha Taasisi za Sekta Binafsi, kwa misaada ya Kitaalam na huduma
mbalimbali za kufanikisha Mkutano huu. Niwashukuru pia Waandishi wa Habari kwa
kazi nzuri walizofanya kuhakikisha kuwa taarifa za majadiliano na maamuzi
mbalimbali ya hapa Bungeni zinawafikia Wananchi. Niwashukuru Madereva kwa
kazi nzuri waliofanya ya kuwasafirisha kwa usalama Waheshimiwa Wabunge,Viongozi
mbalimbali, Wataalam na Wasaidizi wote walioshiriki katika Mkutano huu.
Mheshimiwa Spika,
85. Nimalizie kwa kuwatakia wote safari njema
mnaporejea kwenye maeneo yenu ya kazi na katika majimbo yenu. Baada ya
kusema hayo, naomba sasa kutoa hoja kwamba, Bunge lako Tukufu liahirishwe hadi
tarehe 3 Desemba, 2013 saa 3:00 Asubuhi litakapokutana katika Mkutano wa
14 kwenye Ukumbi huu hapa Dodoma.
Mheshimiwa Spika,
86. Naomba kutoa hoja.
@kwa hisani ya Blog ya Michuzi