Na Magdalena Nkulu,Ofisi ya Mkuu wa Mkoa- SHINYANGA
Tume ya watu 18 imeundwa
kuchunguza chanzo cha mgogoro wa kugombea ardhi kati ya wakulima na
wafugaji wa wilaya za Kishapu mkoani Shinyanga na Igunga mkoani Tabora
kufuatia matukio ya mauaji ya watu watano na uharibifu wa makazi.
Hatua
hiyo imeazimiwa na kikao cha kamati za ulinzi na usalama za mikoa ya
Shinyanga na Tabora kilichofanyika jana katika kijiji cha Magogo ambako
vurugu hizo zimetokea.
Wakitoa
taarifa baada ya kikao hicho, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Ally N.
Rufunga na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Bi. Fatuma Mwasa wamesema pamoja na
kuundwa tume hiyo kikao kimeazimia kuwa, wafugaji walioko katika kijiji
cha Magalata wilayani Kishapu mkoa wa Shinyanga wabaki kwenye eneo lao
na wasivuke mto Manonga kulisha ng'ombe wao..
Pia,
wakulima walioko katika vijiji vya Magogo na Isakamaliwa wilaya ya
Igunga mkoani Tabora wabaki huko na wasivuke mto Manonga.
Aidha,wakulima
walioharibiwa makazi waendelee na shughuli zao kama kawaida katika
vijiji vya Magogo na Isakamaliwa mkoani Tabora aidha,ulinzi wa wananchi
wa vijiji vya
Magogo na Isakamaliwa unaimarishwa, askari polisi wameongezwa ili
kuhakikisha usalama wa eneo hilo
Kikao pia kimeazimia waharibifu wa makazi ya watu na wauaji wakamatwe ndani ya siku saba.
Azimio
lingine ni kamati zote mbili kutoa Elimu kwa wananchi wa vijiji vya
Magalata wilaya ya Kishapu na Magogo na Isakamaliwa wilaya ya Igunga,
vilevile Halmashauri
zote mbili za Igunga na Kishapu zihakikishe zinaboresha sheria ndogo
ili kuwaadhibu wanaokiuka utaratibu wa mipaka.
Kwa
pamoja, Mhe.Rufunga na Mhe. Mwasa wamesema serikali imelaani vikali
vitendo hivyo vilivyofanywa na wafugaji wa jamii ya Kitaturu na kusema
ni vitendo visivyovumilika kwani siyo desturi ya Watanzania hivyo
serikali imetoa salamu za pole kwa wafiwa na itahakikisha majeruhi mmoja
anahudumiwa na pia watuhumiwa lazima wakamatwe.
=30=