Friday, October 11, 2013

WIKI YA VIJANA IHAMASISHE USAWA



Maadhimisho ya wiki ya vijana yanalenga kuendeleza fikra za Mwalimu Julius Nyerere za kuhamasisha amani na usawa katika jamii ili wananchi wajiletee maendeleo yao.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu- Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Sihaba Nkinga, akitoa maelezo mafupi kuhusu wiki ya vijana kitaifa mkoani Iringa, yaliyosomwa kwa niaba yake na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya vijana-Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, James Kajugusi katika uwanja wa shule ya msingi Mlandege. 

 Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya vijana-Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, James Kajugusi

Sihaba amesema kuwa serikali iliamua kuziunganisha shughuli za vijana na madhimisho ya kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru pamoja na kumbukumbu ya kifo cha Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere mwaka 1999. Amesema “maamuzi ya Serikali yalizingatia haja ya  kuendelea kuenzi  fikra za Baba wa Taifa za kuutumia Mwenge wa Uhuru kama chombo maalum cha kuhamasisha amani na umoja, kuondoa dhuluma, kukuza moyo wa kujitolea hasa kwa Vijana, na kuleta maendeleo ya watu katika nchi yetu na nje ya mipaka yetu”.

Akiongelea fursa watakazopata vijana katika wiki hiyo ya maonesho, Katibu Mkuu amesema kuwa vijana watapata fursa ya kukutana, kuonyesha shughuli wanazozifanya na kutathimini mchango wao katika kulijenga Taifa la Tanzania. Amesema kuwa vijana wataweza kutumia wiki hiyo kutengeneza mitandao na kubadilishana uzoefu katika masuala mbalimbali yanayohusu maisha yao ya kila siku.

Akielezea shughuli za wiki ya vijana kitaifa, Sihaba amesema kuwa shughuli hizo zimegawanyika katika sehemu tatu. Amezitaja sehemu hizo kuwa ni maonesho ya shughuli mbalimbali zinazofanywa na vijana ambayo yatakuwa kwenye mabanda maalum. Shughuli nyingine ni midahalo ya vijana, ambapo vijana watapata fursa ya kujadili na kujifunza mambo mengi kupitia mada mbalimbali. 

Mada hizo ni Ujue Mkoa wa Iringa, Maudhui ya Wiki ya Vijana, Fursa za ajira kwa Vijana, Ushiriki na ushirikishwaji wa Vijana katika maendeleo, Huduma ya hifadhi ya Jamii kwa Vijana na Wajibu wa Vijana katika kutunza amani ya nchi. Shughuli ya mwisho ni huduma ya kupima virusi vya ukimwi kwa hiyari itakayotolewa bure.

Washiriki wa maonesho hayo ni vijana kutoka mikoa yote ya Tanznia Bara na Visiwani kupitia kwenye vikundi vyao vya uzalishaji mali, makampuni na taasisi za vijana, mashirika na idara za Serikali pamoja wadau mbalimbali wa maendeleo ya vijana hapa nchini.
=30=