Watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa wametakiwa kupima afya
zao ili kujitambua na kuchukua hatua dhidi ya maambukizi ya VVU na ukimwi kwa
lengo la kuwa na afya njema na kuongeza ufanisi wa kazi.
Katibu Tawala Msaidizi, Sehemu ya Utawala, Scolastica Mlawi
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa
wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma katika hotuba yake iliyosomwa kwa niaba
yake na Katibu Tawala Msaidizi, Sehemu ya Utawala na Rasilimali watu,
Scolastica Mlawi wakati wa kufungua semina ya siku ya familia na mapambano
dhidi ya ukimwi mahala pa kazi kwa watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa
iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Siasa ni Kilimo wilayani Iringa.
Dkt. Christine amesema “ni vema kila mtumishi apime afya yake ili
ajitambue na kuchukua hatua zinazostahili kwa kuwa huduma za kuzuia maambukizi
mapya kwa watu ambao hawana maambukizi pia wale wenye maambukizi wasipate
maambukizi mengine zinatolewa katika zahanati, vituo vya afya na hospitali za
serikali, taasisi na mashirika binafsi”. Amesema kuwa wateja wanaotembelea
vituo vya kutolea huduma za afya wakiwa wanaumwa magonjwa mengine aukusindikiza
wagonjwa wanashauriwa kupima VVU. Amesema kuwa huduma hiyo imesaidia sana
kuwafanya watu wengi kujua hali za afya zao kuhusiana na maambukizi ya VVU na
kuchukua hatua.
Mkuu wa Mkoa wa
Iringa amesema kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inawajali sana
watumishi wake hasa wanaoishi na VVU. Amesema “serikali ya Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania katika kuwajali watumishi wake inatekeleza Waraka Na. 6 wa Mwaka
2006 kutoka Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma ambao unamtaka kila
mwajiri katika Wizara, Taasisi, Mashirika na Idara za Serikali kuwasaidia watumishi wanaoishi na V.V.U. kwa
kuwapa fedha kidogo kwa ajili chakula na nauli wakati wa kwenda kupata huduma
za matibabu”.
Ameendelea kusema
kuwa watumishi wamekuwa wakishauriwa kupima afya zao na kutoa elimu ya kuzuia
maambukizi mapya. Katika kuonesha msisitizo, ametoa rai tena kwa watumishi
kupima afya zao ili wanapogundulika kuwa na maambukizi ya V.V.U. waweze kupata
huduma ya ushauri, vipimo, dawa, matibabu kwa magonjwa nyemelezi na mlo kamili.
Akiongelea
malengo ya semina hiyo kwa watumishi, Afisa Tawala mwandamizi katika ofisi ya
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Neema Mwaipopo amesema kuwa lengo ni kuelimishana na
kukumbushana kujikinga na maambukizi mapya ya ukimwi kwa ambao bado hawajapata
na kwa ambao wamepata kujikinga na maambukizi mapya. Amesema kuwa lengo jingine
ni kuwahamasisha watumishi kwenda kupima na watakaokutwa wameathirika watoe
taarifa kwa mwajiri ili waweze kunufaika na msaada wa huduma kwa mujibu wa
Waraka Na. 6 wa Mwaka 2006 kutoka Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa
Umma ambao unamtaka kila mwajiri kuwasaidia watumishi wanaoishi na V.V.U.
Neema amesema
kuwa suala la unyanyapaa halipo kutokana na watumishi kupatiwa elimu ya mara
kwa mara. Amesema kuwa utaratibu wa kutoa elimu kupitia semina, vikao na
mikutano mbalimbali ni endelevu katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa.
Siku ya familia
na mapambano dhidi ya ukumwi katika ofisi ya mkuu wa mkoa imeongozwa na
kaulimbiu isemayo Iringa bila maambukizi mapya,
unyanyapaa na vifo vitokanavyo na ukimwi inawezekana.
=30=