Tuesday, March 12, 2013

TANZANIA YAPUNGUZA VIFO VYA WATOTO




Tanzania imefanikiwa kupunguza idadi ya vifo vya watoto walio na umri chini ya miaka mitano kwa asilimia 45 kutokana na kuhimiza matumizi ya chanjo dhidi ya kujikinga na magonjwa mbalimbali nchini.

Hayo yamesemwa na mratibu wa chanjo kitaifa toka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Zebina Msumi wakati akiwasilisha mada juu ya hali ya chanjo nchini katika semina ya waandishi wa habari wa mikoa ya Iringa, Njombe na Ruvuma kuhusu kuanzishwa kwa chanjo mpya za pneumococcal na rotavirus iliyofanyika katika ukumbi wa chuo kikuu huria tawi la Iringa.

Zebina amesema kuwa Tanzania kama nchini nyingine zinazoendelea inafanya juhudi kubwa ili kufikia malengo ya milenia ya nne na tano ifikapo mwaka 2012. Amesema katika juhudi hizo, Tanzania imefanikiwa kupunguza vifo vya watoto walio na umri chini ya miaka mitano kutoka 147 mwaka 1999 hadi kufikia vifo 81 kwa kila watoto 1,000 waliozaliwa hai, hilo likiwa ni punguzo la asilimia 45. Aidha, vifo vya watoto chini ya mwaka mmoja vimepungua kutoka 99 hadi kufikia 51 ilikuwa ni punguzo la asilia 49. 

Amesema kuwa mafanikio hayo yanatokana na viwango vya chanjo kuendelea kupanda kutoka asilimia 50 miaka ya 60 hadi kupindukia asilimia 90 mwaka 2011.

Akielezea huduma ya chanjo nchini, mratibu huyo amesema kuwa imethibitika kitaalamu kuwa chanjo mkakati muafaka katika kutokomeza maradhi na kupunguza vifo vya watoto na kupunguza gharama kubwa ambazo familia na taifa kwa ujumla limetumia katika kutibu maradhi yatokanayo na magonjwa yanayozuilika kwa chanjo. Ameyataja magonjwa yanayokingwa kupitia mpango wa chanjo kuwa ni kifua kikuu, polia, dondakoo, pepopunda, kifaduro, homa ya ini, homa ya uti wa mgongo, surua na vichomi.

Kwa upande wa changamoto zilizopo, Zenina amezitaja kuwa ni vimelea vya  Streptococcus pneumoniae ni kisababishi kikuu cha maradhi na vifo vitokanavyo ugonjwa wa vichomi na homa ya uti wa mgongo. Ameongeza kuwa vimelea vya “rotavirus” kwa upande mwingine husababisha takribani asilimia 80 ya maradhi na vifo vitokanavyo na kuharisha kukali kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano duniani.

Ameitaja mikakati iliyopo kuwa ni chanjo ya “pneumococcal” (PCV13) kukinga maambukizi ya vichomi kwa asilimia 38 na homa ya uti wa mgongo kwa karibia asilimia 87 na chanjo ya “rotavirus” inayokinga kuharisha kukali kunakosababisha vifo vya watoto kwa asilimia 80; na kwa sehemu kubwa kukinga ugonjwa wa kuharisha unaosababishwa na vimelea vya aina nyingine pia.

Mikakati mingine ameitaja kuwa ni Serikali na Wadau wa maendeleo  kuhakikisha kuwa chanjo zinapatikana kwa walengwa wote na kwa muda unaotakiwa na miundombinu ya kuhifadhi na kusafirisha chanjo imeimarishwa  kuwezeshwa kutunza.

Vilevile, chanjo za PCV13 na Rotarix zimeshawasili nchini na zimesambazwa mikoa yote  na watumishi kupatiwa mafunzo ya jinsi ya kutoa chanjo hizi mpya.
Mtoa mada amewata wanahabari hao kuwahimiza akina mama kunyonyesha maziwa ya mama pekee kwa miezi sita na kuimarisha usafi wa mazingira na kunawa mikono kwa sabuni husaidia kupunguza mambukizo ya magonjwa ya kuhara.   

Vilevile, amesisitiza kuwa chanjo ya Rotarix itatolewa pamoja na chanjo zingine  zinazotolewa katika kliki na ratiba ya chanjo  inatolewa mtoto akiwa na wiki 6 na 10. Chanjo hii inatolewa bure katika vituo vinavyotoa huduma za chanjo nchini kama ilivyo kwa chanjo zingine.
=30=

SERIKALI YATHAMINI MCHANGO WA VYOMBO VYA HABARI



Serikali inatambua na kuthamini mchango wa vyombo vya habari nchini katika kuhabarisha na kuhamasisha jamii katika kufanikisha kampeni za afya kuanzia ngazi ya kijiji hadi Taifa.

Kauli hiyo imetolewa na Gloria Tesha alipokuwa akitoa mada juu ya majukumu ya vyombo vya habari katika huduma za chanjo nchini katika ukumbi wa Chuo kikuu Hurua tawi la Iringa.

Gloria amesema “vyombo vya habari vina uwezo na ushawishi mkubwa katika kuhamasisha jamii kupitia mfumo na uongozi uliopo kuanzia ngazi ya kijiji hadi Taifa katika mikakati yote ya maendeleo ya nchi ikiwemo huduma za afya”.

Amesema kuwa uwezo wa vyombo vya habari umejidhihirisha katika kutoa habari sahihi na muhimu kwa muda muafaka kwa jamii kwa lengo la kuelimisha, kuhabarisha na kuhamasisha wananchi kushiriki katika huduma na kampeni mbalimbali. “Habari zinaiwezesha jamii kufahamu mambo mbalimbali na kuwa na uwezo wa kufanya maamuzi sahihi” alisisitiza Gloria.

Akielezea mchango wa vyombo vya habari katika kufanikisha kampeni za afya, amesema kuwa ushiriki wa vyombo vya habari katika uanzishwaji wa chanjo mpya ni nyenzo muhimu katika mchakato mzima wa kuboresha afya ya watoto nchini na kufikia malengo ya milenia. Amesema dhana hii inakubalika kutokana na ukweli ulivyo kulingana na historia ya mchango wa vyombo vya habari ilivyo katika maendeleo ya Tanzania. Amesema Wizara inategemea kuwa vyombo vya habari vitawakilisha ujumbe kwa jamii katika uanzishwaji wa chanjo mpya; pamoja na lengo la nne la milenia linalolenga kupunguza vifo vya watoto chini ya miaka mitano kwa theluthi mbili ifikapo 2015.

Kuhusu ujumbe kwa jamii kupitia vyombo vya habari juu ya chanjo ya Rotavirus amesema magonjwa ya kuharisha husababishwa na vimelea vya aina mbalimbali lakini virusi vya Rota huchangia kwa kiwango kikubwa katika magonjwa ya kuharisha kwa watoto walio na umri wa chini ya miaka mitano. Amesema virusi vya Rota huenezwa kwa njia ya kula na /au kunywa maji yaliyochafuliwa na kinyesi chenye virusi hivyo.

Amesema kuwa dalili kuu za ugonjwa huo ni kutapika na kuharisha na mara nyingine huambatana na homa. Ameongeza kuharisha huchukua kati ya siku 4 hadi 7 sambamba na upungufu wa maji mwilini.

Mtoa mada huyo ameelezea njia za kujikinga kuwa ni kumnyoshesha mtoto maziwa ya mama pekee kwa miezi sita ya mwanzo tangu anapozaliwa bila kumpa kitu chochote kingine chochote yakiwemo maji. Kinga nyingine ameitaja kuwa ni usafi wa mazingira na kunawa mikono kwa maji safi na sabuni husaidia kupunguza maambukizo ya magonjwa ya kuharisha kwa ujumla. Aidha, amesisitiza kuwa wazazi na walezi ni vizuri wafuate ratiba ili watoto wasipitishe umri wa kupata dozi ya chanjo ya Rotavirus kwasababu umri ukizidi ataikosa chanjo hiyo na wazazi na walezi watapewa tarehe ya kurudi tena wiki nne baada ya dozi ya kwanza.

Akielezea mategemeo ya Wizara baada ya semina hiyo kwa waandishi wa habari, Gloria amesema kuwa anategemea kuwa waandishi wa habari wataweka habari za chanjo hiyo kuwa habari kuu kwa sababu inahusu kunusuru watoto na vifo vinavyozuilika. Amesema pia anategemea kupata habari nyingi katika makala, habari, majarida na vipindi vya kutosha vya kuelimisha jamii.
=30=


Friday, March 8, 2013

MKUU WA MKOA WA IRINGA AKEMEA VITENDO VYA DHULUMA KWA WANAWAKE



Jamii imetakiwa kubalidilika na kupinga vitendo vya dhuluma wanavyofanyiwa wanawake na watoto wa kike nchini kwa kuhimiza matumizi ya sheria na haki katika kuhamasisha usawa wa kijinsia.

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma katika hotuba yake ya maadhimisho ya siku ya wanawake duniani iliyofanyika kimkoa katika kijiji cha Ibangamoyo, Kata ya Ulanda Wilayani Iringa leo.

Dkt. Christine amesema kuwa ”napenda kutoa wito kwa jamii mzima kubadili mitazamo iliyopitwa na wakati dhidi ya wanawake kwa sababu haina nafasi kwa wakati tulionao sasa. Ni lazima sote kwa pamoja tufahamu kuwa kila mtu anaweza, awe mwanamke au mwanaume”. Amesema kuwa lazima vitendo vya dhuluma dhidi ya wanawake na watoto wa kike vikemewe vikali na kuhimiza matumizi ya sheria na haki katika kupinga unyanyasaji na dhuluma wanazofanyiwa wanawake. Amesema ”hapo nyuma wanawake waliachwa nyuma kwa mengi ya muhimu kama elimu, ajira, mitaji na katika kutoa maamuzi lakini sasa umefika wakati wa kutambua uwezo na mahitaji yao katika kuendeleza gurudumu la maendeleo katika jamii”.

Akiongelea nafasi ya Serikali katika kuhakikisha wanawake wanapatiwa haki katika masuala mbalimbali ya kijamii na kiuchumi amesema ”Serikali imeweka mikakati mizuri sana ya kuwawezesha wanawake katika masuala  ya elimu, ajira, nafasi za uongozi lakini tatizo limebaki katika ngazi ya familia, vijiji na Kata”. Aidha, ameshauri kuwekwa mfumo mzuri wa kushughulikia matatizo ya unyanyasaji wa kijinsia kwa wanawake na kuweka vizuri kumbukumbu za matukio hayo ili tuweze kuwa na kumbukumbu sahihi.

Katika kusisitiza hilo, ameziagiza Halmashauri za za Wilaya na Manispaa kuhakikisha matatizo yanayotokana na unyanyasaji na ukatili wa kijinsia yanashugulikiwa vizuri na kutunza kumbukumbu za matukio hayo kuanzia ngazi za vijiji, Kata hadi Halmashauri za Wilaya. Amewataka kuwa na rejesta inayoorodhesha matukio yote ya ukatili wa kijinsia na jinsi matukio hayo yalivyoshughulikiwa katika ngazi husika. Kwa kufanya hivyo itakuwa rahisi hata kuweza kufanya tafiti ili kujua ukubwa wa tatizo hilo katika ngazi ya Wilaya na Mkoa.

Dkt. Christine ameziagiza Halmashauri zote za Mkoa wa Iringa kuhakikisha elimu inatolewa mara kwa mara katika vijiji vyote ili kila mtu aelewe madhara ya ukatili wa kijinsia na pale itakapotokea mtu kufanya unyanyasaji huo achukuliwe hatua zinazostahili na wale wote wanaotendewa ukatili waweze kupata haki zao.

Mkuu wa Mkoa wa Iringa amesema kuwa Mkoa wa Iringa hauwezi kupiga hatua zaidi katika maendeleo iliwa wanawake hawatapewa nafasi katika nyanja za kiuchumi, kisiasa na kijamii. Amesema ”ili Mkoa wetu wa Iringa uweze kupiga hatua zaidi katika maendeleo ni lazima wanawake wapewe nafasi katika nyanja za Kuchumi, Kisiasa na Kijamii”. Aidha, amesisitiza elimu lazima iendelee kutolewa kwa wananchi wote na kwa muda wote siyo tu kusubiri katika kipindi cha maadhimisho hayo.

Maadhimisho ya siku ya wanawake duniani yanaongozwa na kaulimbiu isemayo ‘uelewa wa masuala ya jinsia; ongeza kasi’ kwa lengo la kuweka msisitizo kwa jamii kuona umuhimu wa kila mmoja wetu kuelewa maana ya usawa wa jinsia una umuhimu wake katika jamii.

Maadhimisho haya ni matokeo ya kumbukumbu ya kihistoria ya mwanaharakati mwanamke wa nchini Ujerumani Clara Serkin aliyejaliwa ujasiri na ushupavu wa kutetea wanawake dhidi ya  kandamizwaji, unyanyaswaji na dhuluma walizokuwa wakifanyiwa na wanaume katika nyanja za kiuchumi, kisiasa, kijamii na kiutamaduni.

Katika taarifa ya maendeleo ya shughuli za wanawake wa Wilaya ya Iringa iliyowasilishwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani Immaculate Senje amesema kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa imekuwa ikihamasisha wanawake kujiunga katika vikundi na kupatiwa elimu ya ujasiliamali na jinsi ya kubuni miradi ya maendeleo na jinsi ya kuiendesha. Amesema kuwa hadi sasa jumla ya vikundi 176 ambavyo kati  ya vikundi hivyo vikundi 100 ni vya kawaida na vikundi 66 ni benki za kijamii. Amesema kuwa vikundi hivyo vina jumla wanachama 2,021.

Amesema kuwa Halmashauri yake imekuwa ikihamasisha kuunda benki za kijamii vijijini (VICOBA), ambapo jumla ya VICOBA 66 vimeanzishwa vikiwa na wanachama 1361 na mtaji wa sh. 150,980,560. Aidha, amesema kuwa wanawake wamekuwa wakihamasishwa kujiunga na SACCOS katika maeneo yao kwa malengo ya kujijengea tabia ya kukopa na kuweka. Amesema jumla ya wanawake 1,527 sawa na asilimia 40 wamejiunga na SACCOS.

Akiongelea umiki wa ardhi, Immaculate amesema kuwa Halmashauri imeendelea na jitihada za kuwapa fursa wanawake ya kumiliki ardhi kwa sababu ndiyo rasilimali pekee inayoweza kumkomboa mwanamke kuondokana na umasikini. Amesema kuwa bado hakuna usawa katika umiliki wa ardhi kati ya wanawake na wanaume. Amesema kuwa kati ya watu 6,133 waliopata hati za kimila za kumiliki ardhi wanawake 2,006 wamepata hati za kumiliko ardhi.
=30=

WAANDISHI HABARI WA NYANDA ZA JUU WATAKIWA KUELIMISHA JUU YA CHANJO



Waandishi wa habari wa Mikoa ya Iringa, Njombe na Ruvuma wametakiwa kutoa elimu na hamasa kwa wananchi kwa lengo la kufanikisha zoezi la chanjo mpya zinazozuia magonjwa ya vichoni , uti wa mgongo na kuharisha nchini.

Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma katika hotuba yake kwenye ufunguzi wa semina ya waandishi wa habari wa mikoa ya Iringa, Njombe na Ruvuma kuhusu kuanzishwa kwa chanjo mpya za ‘pneumococcal’ na ‘rotavirus’ zinazozuia magonjwa ya vichomi, kuharisha na uti wa mgongo katika ukumbi wa chuo kikuu huria njini Iringa.

Dkt. Christine amesema “napenda kuwafahamisha rasmi kuwa mwaka huu 2013 Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imeanzisha chanjo mpya mbili za ‘pneumococcal’ na ‘rotavirus’.
Akielezea malengo ya Semina hiyo, Mkuu wa Mkoa amesema kuwa lengo kuu la semina hiyo ni kuwaelimisha wanahabari juu ya uanzishwaji wa chanjo hizo mpya. Amesema kuwa baada ya kuelewa vizuri uanzishwaji wa chanjo hizo watakuwa na jukumu la kuihabarisha jamii kuhusu chanjo mpya kwa kutoa hamasa na taarifa sahihi, muhimu na kwa muda muafaka kuhusu hizi chanjo.
Amesema kuwa vimelea vya ‘streptococcus pneumoniae’ ni kisababishi kikuu cha maradhi na vifo vitokanavyo na ugonjwa wa vichomi na homa ya uti wa mgongo kwa watoto katika nchi zinazoendelea. Amesema “vimelea vya “rotavirus” kwa upande mwingine husababisha karibia asilimia 80 ya maradhi na vifo vitokanavyo na kuharisha kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano duniani”.

Amesema “kwa mujibu wa rejea za kitaalamu zinaonesha kuwa chanjo ya ‘pneumococcal’ hukinga maambukizi ya vichomi kwa asilimia 38 na homa ya uti wa mgongo kwa karibia asilimia 87 wakati na chanjo ya ‘rotavirus’ hukinga kuharisha kunakosababisha vifo vya watoto kwa asilimia 80”.

Aidha, chanjo ya ‘rotavirus’ kwa sehemu kubwa hukinga ugonjwa wa kuharisha unaosababishwa na vimelea vya aina nyingine pia.
Dkt. Christine amewataja walengwa wa chanjo hizo kuwa ni watoto walio na umri chini ya miezi Kumi na Miwili. Aidha, amesema kuwa chanjo ya kukinga vichomi  na uti wa mgongo inatolewa mara tatu kuanzia umri wa wiki 6, 10 na 14. Chanjo ya kukinga kuhara inatolewa mara mbili kuanzia umri wa wiki 6 na 10. Amesisitiza kuwa ni vizuri mtoto apate kinga kamili ni lazima kukamilisha ratiba ya chanjo hizi mapema.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, amesema kuwa kutokana na umuhimu wa chanjo hizi na uwekezaji kwa Taifa, Serikali inatoa chanjo hizi bila malipo ili kila mtoto aweze kupata chanjo hizi. Aidha, Mkuu wa mkoa aliwahakikishia wanahabari wao kuwa chanjo hizo ni salama na zitatolewa na wataalamu wenye ujuzi na uzoefu wa kutosha.
Katika salamu za Mganga Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Robert Salim amewaomba wanahabari hao kuhakikisha wanapeleka ujumbe sahihi na kwa muda muafaka ili kuondoa dhana ambayo imekuwa ikijengeka mara zinapofanyika chanjo mbalimbali. Amesema ni vema wakawapinga wale wote wanaopotosha kuwa chanjo hizo zinalenga kuwafanya wasiweze kuzaa.
=30=