Wednesday, May 4, 2011

...Zingatieni kanuni za kazi
Waajiri wametakiwa kuzingatia misingi na kanuni za kazi ili kuweza kuondoa migogoro inayoweza kujitokeza kwa kukiukwaji huo mahala pa kazi.

Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, katika hotuba yake iliyosomwa kwa niaba yake na Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Evarista Kalalu katika maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani- Mei Mosi iliyofanyika kimkoa Wilayani Mufindi leo.


Kaimu Mwenyekiti wa TUCTA Mkoa (kushoto), Mgeni rasmi Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Iringa katika maadhimisho ya Meimosi, Evarista Kalalu (katikati) na kuu wa Wilaya ya Ludewa, Georgina Budala (kulia)

Kaimu Mwenyekiti wa TUCTA Mkoa (kushoto), Mgeni rasmi Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Iringa katika maadhimisho ya Meimosi, Evarista Kalalu (katikati) na kuu wa Wilaya ya Ludewa, Georgina Budala (kulia)

Kalalu amesema “ili kupunguza migogoro isiyo ya lazima mahala pa kazi waajiri wote wafanye kazi kwa kufuata misingi ya Sheria na Kanuni za kazi”. Mfanyakazi anawajibu wa kuipenda kazi yake lakini kero za kikazi zinapokuwa nyingi humfanya mfanyakazi kuichukia na ufanisi wa kazi yake kupungua. “Naomba sana tujitahidi kupunguza kero kwa wafanyakazi wetu na ikibidi tuwape motisha ambazo zitawafanya wafanye kazi kwa bidii” amesisitiza Kalalu.

Mkuu huyo wa Wilaya ya Mufindi amewata waajiri kuwa makini wanaposhughulikia utatuzi wa kezo za wananchi kuzingatia makundi yote husika. Amesema kutokufanya hivyo kunaweza kujenga mianya ya kutengeneza makundi baina ya wafanyakazi na badala ya kutatua kezo husika kujikuta wanatengeneza kero na migogoro mingine ambayo ingeweza kuepukika.
  
Aidha, amewataka waajiri kutenga  muda wa kukaa na waajiriwa wao ili kujadili masuala mbalimbali ya kazi na matatizo yanayojitokeza ili yamalizwe kwa njia ya mazungumzo.

Awali akisoma risala ya wafanyakazi wa Mkoa wa Iringa, Mratibu wa TUCTA Mkoa, Khatibu Juma Baweni amesema kuwa wafanyakazi wanawajibu wa kufanya kazi kwa bidii na kuongeza tija katika jitihada za kuongeza pato la taifa. Amesema “kila mtu akitimiza wajbu wake hapatakuwa na malalamiko baina ya wafanyakazi na waajiri” amesisitiza Baweni. Aidha, amesisitiza kilio cha wafanyakazi dhidi ya kupanda kwa bei ya umeme, mafuta na bidhaa nyingine jambo lisiloenda sanjali na upandaji wa mishahara ya wafanyakazi jambo linalomdidimiza mfanyakazi kiuchumi.

Maadhimisho haya ya siku ya wafanyakazi duniani maarufu kama Mei Mosi ni kumbukumbu ya mapambano ya wafanyakazi ya kujikomboa yaliyoanzia Ulaya na Marekani ya Kaskazini katika karne ya 18 na 19 kutoka katika ukandamizaji na unyonyaji wa waajili kutokana na ukuaji wa viwanda.   







No comments:

Post a Comment