Vyombo vya habari vya Mkoa wa Iringa vimepongezwa kwa jitihada kubwa vinazozifanya za kuhamasisha michezo Mkoani hapa hususani mpira wa miguu.
Pongezi hizo zimetolewa na Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Bibi. Gertrude Mpaka wakati akipokea shilingi 1,500,000 fedha taslimu zikiwa ni ufadhili wa kampuni ya bia Tanzania (TBL) kwa timu ya Mkoa wa Iringa katika mashindano ya Kili Taifa Cup mwaka 2011 katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa leo.
Mwakilisi wa TBL Mkoani Iringa, Masumbuko John Changwe (katikati) akimkabidhi
Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Gertrude Mpaka (kulia) Tshs. 1,500,000 za ufadhili
wa timu ya Mkoa wa Iringa, kushoto ni Afisa Michezo Mkoa Keneth Komba
akishuhudia tukio hilo .
Akitoa shukrani hizo Bibi. Mpaka amesema “nawashukuru sana kampuni ya bia Tanzania kwa mchango wenu wa fedha na vyombo vya habari kwa jitihada kubwa za kuhamasisha michezo na kuutangaza Mkoa wa Iringa”.
Katibu Tawala Mkoa wa Iringa ambaye ndie Mwenyekiti wa Kamati ya Michezo ya Mkoa amewaasa wanamichezo wanaouwakilisha Mkoa wa Iringa katika mashindano ya Kili Taifa Cup kuzingatia nidhamu ya hali ya juu ili waweze kuuletea Mkoa ushindi na heshima kubwa.
Bibi. Mpaka amesema kuwa Serikali inathamini sana michezo na kukuza vipaji vya wanamichezo nchini na kutokana na umuhimu huo ndio maana Serikali imerudisha michezo ya UMITASHUMTA na UMISETA shuleni.
Awali akitoa maelezo kabla ya kukabidhi fedha za ufadhili wa TBL, mwakilishi wa TBL Mkoani Iringa, Masumbuko John Changwe amesema kuwa kampuni ya bia nchini inamalengo ya kuinua vipaji vya wanamichezo vijana nchini na kuwapatia ajira kupitia michezo.
Aidha, amekemea vikali vitendo visivyo vya kimichezo vya kuwapiga waamuzi na matumizi ya lugha ya matusi kwa wanamichezo. Vilevile amesisitiza kuwepo kwa mfumo mzuri wa kupata timu ya Mkoa iliyo bora kwa kuwashirikisha wadau wote ili timu ya Mkoa iwe na sura ya kimkoa.
Nae Katibu wa chama cha mpira wa miguu mkoani hapa Eliud Mvella amesemakuwa changamoto iliyopo ni udhamini ambapo amesema kuwa chama chake kipo mbioni kufanya maongezi na kampuni ya bia Tanzania ili waongeze wigo wa fedha katika udhamini wao.
Timu ya mpira wa miguu ya Mkoa wa Iringa itaondoka kesho tarehe 5 Mkoani hapa kuelekea kuelekea Mkoani Mbeya ambapo inajiwinda kufungua dimba na timu ya Mkoa wa Mbeya hapo tarehe 7 Mei, 2011.
No comments:
Post a Comment