Wiki ya
nenda kwa uslama barabrani inalenga kuwakumbusha madereva na watumiaji wa
barabara juu ya sheria na taratibu za matumizi mazuri ya barabara kwa usalama
wa watumiaji na vyombo vya moto nchini.
Kauli hiyo
imetolewa na Mkaguzi wa Polisi, Abel Baetazal Swai kutoka Makao Makuu ya Kikosi
cha Usalama Barabarani, Kitengo cha Elimu alipokuwa aliwaelimisha wananchi wa
Manispaa ya Iringa katika Banda la Polisi lililopo katika uwanja wa maonesho ya
wiki ya nenda kwa usalama barabarani yanayoendelea mjini Iringa.
Mkaguzi
Swai amesema kuwa maana halisi ya wiki ya nenda kwa usalama barabarani n
kufanya marejeo kwa madareva ambao wamepitia mafunzo ya udereva kuweza
kukumbushwa sheria na taratibu pindi wanapokuwa barabarani. Amesema kuwa polisi
wanakuwa wanatoa elimu kwa makundi mbalimbali yanayotumia vyombo vya moto kwa
namna moja na ambayo hayatumii vyombo hivyo kwa namna nyingine. Amesema kuwa
katika kipindi hicho kazi nyingine zinazofanyika ni pamoja na kukagua magari
bure.
Akielezea
tathmini yake juu ya hali ya usalama barabarani Mkaguzi wa Polisi Swai amesema
kuwa hali si mbaya kwa sababu elimu inayotolewa imekuwa ikiwasaidia sana
madereva na watumiaji wengine wa barabara kurejea katika sheria na taratibu za
usalama barabarani. Amesema kuwa elimu
hiyo imekuwa ikitolewa katika shule na mikusanyiko mbalimbali, na majaribio ya
tathmini yaliyofanyika katika mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro na Pwani
inaonesha kupungua kwa ajali za barabarani.
Mkaguzi wa
Polisi Swai amesema kuwa elimu hiyo imekuwa ikitolewa kwa shule za msingi na
sekondari na kupitia vipindi mbalimbali vya redio na vyombo vingine vya habari.
Akielezea
vyanzo vya ajali, Swai amevitaja vyanzo hivyo kuwa ni miundombinu duni, makosa
ya kibinadamu na vyombo vyenyewe. Amesema mkusanyiko wa vyanzo hivi ndiyo
huchangia sana katika ajali za barabarani.
Wakati
huohuo, Afisa wa Polisi, Makao Makuu ya Jeshi la Polisi, Kitengo cha kuzuia
Uhalifu, Mariam Mruma wakati akifafanua juu dhana ya kuzuia uhalifu katika
makazi na vyombo vya moto amesema kuwa ni vema wananchi kuwa makini na kuchukua
tahadhari zote dhidi ya uhalifu katika maeneo yao. Amesema Jeshi la Polisi
linatumia maadhimisho ya wiki ya nenda kwa usalama barabarani kutoa elimu kwa
jamii dhidi ya kuzuia uhalifu katika makazi na vyombo vya moto. Amesema katika
magari ni vizuri wananchi kukokuacha vitu vya thamani ndani ya magari kwa
sababu vitu hivyo vinawashawishi wahalifu kutenda kosa na kushauri pia
wanapoyapaki magari yao kuyapati katika maeneo yaliyo wazi na yenye mwanga si
maeneo ya vificho.
Mruma
amesema kuwa katika makazi si vizuri kuwakaribisha nyumbani watu wasio fahamika
vizuri kwa sababu wanaweza kutumia nafasi hiyo kusoma mazingira ya nyumbani
hapo na hatimae kufanya uhalifu. Amesema ni vizuri kwa serikali za mitaa
kufahamishwa juu ya ugeni wowote unaofika katika maeneo yao na majirani kwa
tahadhali ya kiusalama. Aidha, ametoa wito kwa wazazi kuwaelimisha mtoto wao
juu ya kuchukua tahadhari dhidi ya vitendovya udhalilishaji na pindi vinapotokea
waweze kutoa taarifa kwao au kwa walimu kwa wale wao shule.
=30=