Friday, September 21, 2012

WANANCHI LINDENI MIUNDOMBINU YA ELIMU



 Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma amesema kuwa jukumu la ulinzi wa miundombinu ya elimu kama majengo ni jukumu la jamii nzima na sijukumu la jeshi la polisi wala shule husika pekee. 

Kauli hiyo ameitoa alipokuwa akiongea na wananchi wa kata ya Ifunda iliyopo wilayani Iringa kuhusu nafasi ya jamii katika ulinzi wa miundombinu ya elimu hasa baada ya shule ya sekondari ya St. Mary’s Ulete kuungua kwa baadhi ya mabweni na kusababisha uharibifu wa mali za shule na wanafunzi alipokwenda kukagua shule hiyo.

Amesema “tufanye kazi moja muhimu nayo ni kulinda shule na sehemu nyingine ili moto usitokee tena na kila mmoja lazima awe na uchungu kuona moto ukitokea na kuteketeza mali za shule na wanafunzi” alisisitiza Dkt. Ishengoma. Amesema kuwa shule hizo pamoja na kumilikiwa na serikali na taasisi bado zinawahudumia wananchi wote hivyo usalama ni jukumu la jamii nzima. Amesema kuwa pindi shule zinapoathiriwa na majanga ya moto husababisha wanafunzi kufunga shule na kurudi nyumbani. Amesema kuwa jambo hilo limekuwa likisababisha ufumbufu mkubwa kwa wanafunzi ikiwa ni pamoja na kupoteza muda wa masomo. 

Aidha, Mkuu wa Mkoa wa Iringa ameagiza kufanyika kwa mafunzo ya mgambo katika kata ya Ifunda ili kuwafanya wananchi wawe wakakamavu na kujihakikishia ulinzi na usalama katika eneo lao. Amesema kuwa mafunzo ya mgambo ni mafunzo muhimu sana na hufanyika kwa muda mfupi lakini huwa na matokea chanya katika jamii.
Katika taarifa fupi ya shule iliyosomwa na Mkuu wa Shule, Matholinus Kibuga amesema kuwa shule hiyo inakabiliwa na tatizo la moto wa mara kwa mara katika eneo la mabweni. Amesema kuwa ndani ya miezi miwili shule hiyo imekumbwa na majanga ya moto mara mbili na kusababisha hasara kubwa. Amesema kuwa tarehe 20 Julai, 2012 moto ulisababisha uharibifu wa mali za shule na wanafunzi zenye thamani ya shilingi milioni 9. Amesema moto wa tarehe 15 Septemba, 2012 ulisababisha hasara ya mali zenye thamani ya shilingi milioni 80, 400,000. 

Amesema kuwa shule hiyo inakabiliwa na tatizo la wizi wa mali za shule na ukosefu wa nishati ya kudumu kwa ajili ya mwanga na matumizi mengine. Changamoto nyingine ameitaja kuwa ni ukosefu wa uzio kwa ajili ya kusaidia ulinzi na usalama kwa wanafunzi na mali za shule. 

Akielezea hatua zilizochukuliwa katika kukabiliana na changamoto hizo, Mkuu wa shule hiyo amesema kuwa shule yake imeajiri walinzi kutoka kampuni ya ulinzi ya Mwazuma iliyopo mjini Iringa kwa lengo la kukabiliana tatizo la wizi na moto wa mara kwa mara shuleni hapo. Amesema kuwa majadiliano yanafanyika ili kuhakikisha uzio wa shule hiyo unajengwa haraka. Kuhusu changamoto ya nishati, amesema kuwa katika kipindi hiki shule yake inatumia jenereta dogo na kwa dharura kama chanzo cha nishati ya mwanga na kuiomba serikali kufanya juhudi za makusudi za kufikisha nishati ya umeme katika shule hiyo.
Akielezea nafasi ya kanisa katika kuihudumia jamii, Paroko msaidizi wa Parokia ya Ulete, Padre Augustine Kamunyuka ambaye parokia yake ndio wamiliki wa shule hiyo ya sekondari, amesema kuwa lengo la msingi la kanisa ni kumlea mwanadamu kiroho na kimaadili. Amesema kwa msingi huo ili kufanikisha jukumu hilo kanisa pia linahudumia pia mwili pamoja na mambo mengine. 

Amesema katika kufanikisha hilo, kanisa limekuwa likiendesha shule ya ufundi ya ushonaji, ujenzi na uselemala. Amesema pia kanisa katika parokia hiyo limekuwa likiendesha shule ya sekondari, zahanati, shule ya chekechea na kutoa huduma za maji kwa jamii. Amesema kanisa limekuwa likitoa huduma hizo pasipo kufikiria kujipatia faida bali kwa kutekeleza wito wao.

Shule ya sekondari St. Mary’s ilianzishwa mwaka 2006 ikiwa na wanafunzi wa kidato cha kwanza 35. Kwa sasa shule hiyo inawanafunzi 376 wakiwa ni wasichana 160 na wavulana 216. Kati ya mwaka 2010-2011 wanafunzi wote walifauli wa kidato cha nne katika mitihani ya kitaifa.
=30= 

No comments:

Post a Comment