Wednesday, July 27, 2011

WATUMISHI WA RAS IRINGA WAPEWA SOMO LA RUSHWA 

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa ilianzisha Mkakati wa kudhibiti Rushwa mahali pa kazi ili Ofisi hiyo iwe ni eneo salama kutolea huduma kwa wananchi.
Paulos Lekamoi, Mwanasheria wa Sekretarieti ya Mkoa wa Iringa


Hayo yamesemwa na Mwanansheria wa Ofisi hiyo, Paulos Lekamoi wakati akiwasilisha mada juu ya Sheria ya Rushwa na Wajibu wa Watumishi wa Umma katika kudhibiti vitendo vya rushwa katika ukumbi wa Chuo kikuu Huria Tanzania tawi la Iringa katika Manispaa ya Iringa.

Lekamoi amesema “katika kuhakikisha rushwa mahali pa kazi haina nafasi ilianzisha mkakati wa kudhibiti rushwa katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa”.

Amesema mkakati huo umezingatia mkakati wa kitaifa wa kudhibiti rushwa ambapo lengo kuu ni kuimarisha njia za kupambana na rushwa, kuweka mifumo ya uadilifu, uwajibikaji na uwazi katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa pamoja na uzingatiaji wa Sheria ya Rushwa ya mwaka 2007.

Lekamoi amesema katika sehemu ya III ya Sheria Na. 11 imeleta mabadiliko makubwa sana yanayoenda sambamba na Azimio la Umoja wa Mataifa la Mwaka 2005. Amesema Sheria hii imeongeza makosa yaliyopo kwenye Sura ya 329 ya Sheria kama ilivyorekebishwa Mwaka 2000 na kuyataja baadhi ya makosa kuwa ni mchakato wa rushwa (kifungu cha 4), kutumia nyaraka mbalimbali kumpotosha msimamizi (kifungu cha 6), Maafisa wa Serikali kutumia madaraka yao kujinufaisha (kifungu cha 7), kupatikana na mali yoyote ambayo imepatikana kwa njia ya Rushwa (kifungu cha 10).

Amesema kifungu cha 15 (i) (a) na (b) cha Sheria Na. 11, 2007 kinazungunzia makosa yanayohusu upokeaji wa rushwa ambapo Mtumishi wa Umma anaweza kujikuta amejiingiza aidha kwa kujua au kwa kutojua.

Ameyataja makosa hayo kuwa ni kushirikiana na mtu mwingine au mtumishi mwenyewe kushawishi kupokea au kukubalikupokea chochote kwa manufaa yake ili kutekeleza lengo lolote ambalo kimsingi anatakiwa alifanye katika shughuli zake za kila siku.

Vilevile, kifungu Na. 15 (a) kinamtia hatiani mtu yeyote atakaetoa ahadi ya kumpendelea mtu yeyote.


Zaidi ya asilimia 70 ya matumizi ya kawaida ya Serikali ni kwa ununuzi wa bidhaa, huduma na malipo kwa kazi za ujenzi wa miundombinu.

Akiwasilisha mada juu ya Sheria ya Manunuzi ya mwaka 2004, Uwezo wa Bajeti katika kufanikisha Manunuzi na Udhibiti wa Rushwa katika Manunuzi, Afisa Ugavi Msaidizi Mkoa wa Iringa, Janeth Kitinye amesema kuwa eneo la Manunuzi ya Umma ni muhimu sana kwa sababu hutumia sehemu kubwa ya fedha za walipa kodi wa Tanzania.

Bi. Janeth Kitinye, Afisa Ugavi Msaidizi Sekretarieti ya Mkoa wa Iringa akiwasilisha mada

Aidha, ufanisi katika eneo hili ni chachu ya kufikia baadhi ya malengo makubwa ya kiuchumi na kijamii ya Taifa.

Amesema kuwa ukiondoa mishahara ya watumishi wa Serikali, karibu asilimia 70 ya Matumizi ya kawaida ya Serikali ni Ununuzi wa bidhaa, huduma na malipo kwa kazi mbalimbali. Vilevile, amesema karibu asilimia 100 ya matumizi ya Maendeleo ni kwa ajili ya ununuzi wa bidhaa, huduma na malipo kwa ajili ya kazi za ujenzi wa miudombinu na miradi mingine ya Maendeleo.

Amewataka watumishi wa Umma kuona kuwa wanalo jukumu kubwa la kuhakikisha Manunuzi wanayoyafanya yanawawezesha kupata bidhaa na huduma zenye Ubora kulingana na thamani ya fedha zilizotumika.

Kitinye amesema Sheria ya Manunuzi ya Umma ya Mwaka 2004, na Kanuni zake za Mwaka 2005 kwa pamoja zinaweka misingi na taratibu za kweza kufikia adhima hiyo.

Ameongoza kuwa Vitengo vya Manunuzi Vinajukumu la msingi la kuhakikisha kuwa huduma muhimu zinawafikia watumishi wa Umma na Wahitaji wengine katika muda uliopangwa na katika ubora unaokubalika. Sharia ya Manunuzi ya Mwaka 2004 na Kanuni zake za Mwaka 2005 zinawapngoza Watumishi wa Umma katika misingi ya Utawala Bora na uwajibikaji kwa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.