Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Iringa
Mkoa
wa Iringa unaendelea kuweka mikakati ya kuendeleza mazao ya korosho, pamba na
kahawai ili yachangie katika kukuza uchumi wa wakulima na mkoa kwa ujumla.
Kauli
hiyo ilitolewa na mkuu wa mkoa wa Iringa, Amina Masenza alipokuwa akifungua
jukwaa la ushirika mkoa wa Iringa kililofanyika katika ukumbi wa Siasa ni Kilimo
hivi karibuni.
Masenza
alisema kuwa serikali inatambua mazao matano ya kimkakati na kuyataja kuwa ni
korosho, kahawa, tumbaku, pamba na chai.
“Mkoa wetu wa Iringa una hali ya hewa nzuri
inayofaa kwa kilimo cha mazao yote. Kumekuwa na maendeleo mazuri katika kilimo
cha chai ambapo uzalishaji umefikia kiasi cha tani 18,930 kwa mwaka 2016/2017,
kwa mazao ya korosho, pamba na kahawa mkoa wetu unaendelea kuweka mikakati thabiti
wa kuyaendeleza” alisema Masenza.
Halmashauri zimeanza kuweka jitihada za
kuhamasisha kulima mazao hayo alisema. “Kupitia
jukwaa hili nawaagiza wakurugenzi wa halmashauri kukaa chini na vyama vya ushirika
kuandaa mpango wa miaka mitano wa kuendeleza mazao hayo” aliagiza Masenza.
Alisema kuwa wananchi wakihamasishwa kuzalisha
mazao hayo kwa wingi, kutawaongezea wanaushirika kushiriki shughuli za
uzalishaji mazao ya kibiashara na kuongeza kipato cha wanaushirika na wananchi
kwa ujumla.
Akiongelea zao la tumbaku, mkuu wa mkoa alisema
kuwa mkoa wa Iringa umekuwa ukizalisha tumbaku kwa zaidi ya miaka 50 lakini zao
hili halijatoa mchango mkubwa kiuchumi kwa wananchi.
“Napenda kutoa rai kuwa tunatakiwa kujipanga upya ili kuendeleza
uzalishaji wa zao hili. Uzalishaji wa zao la tumbaku umekumbwa na changamoto
mbalimbali zikiwemo ukosefu wa soko na uwepo wa madeni makubwa katika vyama vya
msingi ambayo yanasababishwa na wanachama kutouza kupitia vyama vyao. Nachukua
fursa hii kuwaasa wakulima wa zao hili kuzingatia taratibu za kilimo hicho hasa
kutowatumia watoto, kupanda miti na kuuza kwa uaminifu kupitia vyama vya
ushirika” alisisitiza Masenza.
Jukwaa la ushirika ni jukwaa la pili kufanyika
ngazi ya mkoa, likishirikisha Katibu Tawala Mkoa, wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi
wa mamlaka za serikali za mitaa, wadau wa taasisi za kifedha na wanaushirika.
=30=
No comments:
Post a Comment