Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPL Board) imefungia viwanja saba
vilivyokuwa vikitumiwa na timu za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) na Ligi Daraja la
Kwanza (FDL) hadi vitakapofanyiwa marekebisho ili kukidhi mahitaji ya mechi za
mpira wa miguu.
Uamuzi huo umefikiwa na TPL Board katika kikao chake cha kwanza
kilichofanyika juzi (Novemba 10 mwaka huu) jijini Dar es Salaam ambapo pamoja
na mambo mengine kilipitia ripoti za mechi za VPL na FDL katika mzunguko wa
kwanza.
Boniface Wambura
Viwanja vilivyofungiwa na marekebisho yanayotakiwa kufanyika
kwanza ili viruhusiwe kutumika tena ni Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba (majukwaa
yake yamechakaa, hivyo kuhatarisha usalama wa watazamaji), na Uwanja wa CCM
Mkwakwani jijini Tanga (vyumba vya wachezaji kubadilishia nguo (dressing rooms)
havina hadhi).
Uwanja wa Kumbukumbu ya
Sokoine jijini Mbeya (sehemu ya kuchezea- pitch ni mbovu), Uwanja wa Kumbukumbu
ya Sheikh Kaluta Amri Abeid jijini Arusha (pitch ni mbovu), Uwanja wa Ali
Hassan Mwinyi (vyumba vya kubadilishia kutumika kwa ajili ya shule ya awali),
Uwanja wa Majimaji mjini Songea (pitch ni mbovu) na Uwanja wa Jamhuri mjini
Morogoro (pitch ni mbovu).
Klabu ambazo timu zake
zinatumia viwanja hivyo zimeshaarifiwa rasmi juu ya uamuzi huo ambapo ama
vinatakiwa kuwasiliana na wamiliki wa viwanja hivyo ili wafanye marekebisho au
kutafuta viwanja vingine vya kuchezea mechi zao.
Kwa upande wa ripoti za
mechi za VPL; Mbeya City imepigwa faini ya sh. 500,000 na kupewa onyo kali kwa
timu yake ya U20 kutocheza mechi ya utangulizi walipocheza na Yanga. Pia
wanatakiwa kulipa gharama za uharibifu baada ya washabiki wao kuvunja kioo cha
basi la Yanga baada ya gharama hizo kuthibitishwa na Bodi ya Ligi.
Pia Mbeya City imepigwa
faini ya sh. 500,000 kwa washabiki wake kushambulia basi la wachezaji wa
Tanzania Prisons baada ya mechi dhidi yao, na kulipa gharama za uharibifu baada
ya kuthibitisha na Bodi ya Ligi.
Coastal Union imepigwa
faini ya sh. 500,000 kutokana na vurugu za washabiki wake ilipocheza na Azam
kwenye Uwanja wa Mkwakwani ambapo mwamuzi msaidizi Hassan Zani alishambuliwa
kwa mawe na kujeruhiwa mkononi na kichwa, tukio lililosababisha mchezo kusimama
kwa dakika tatu.
Beki wa Coastal Union,
Hamad Khamis wa Coastal Union amepigwa faini ya sh. 500,000 kwa kumpiga kichwa
kwa makusudi Kipre Tchetche wa Azam. Kitendo hicho kilisababisha refa amtoe nje
kwa kadi nyekundu, hivyo atakosa mechi tatu zinazofuata za timu yake.
Mchezaji Cosmas Lewis wa
Ruvu Shooting alifanya kitendo cha utovu wa nidhamu kwa kupiga kelele wakati
mgeni rasmi akisalimia timu na kukataa kupeana mkono na kamishna kwenye mechi
dhidi ya Rhino Rangers, hivyo amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya sh.
500,000.
Mtunza vifaa (Kit Man)
wa JKT Ruvu, Selemani Oga aliondolewa kwenye benchi la ufundi wakati wa mechi
yao dhidi ya Mbeya City kwa kosa la kutoa lugha chafu kwa refa, hivyo suala
lake litapelekwa katika Kamati ya Maadili.
Kocha Msaidizi wa Oljoro
JKT, Fikiri Elias amepigwa faini ya sh. 500,000 na kufungiwa mechi tatu kwa
kumshambulia kwa matusi refa wakati wa mechi yao dhidi ya Ashanti United. Naye
mtunza vifaa wa timu hiyo Elas Justin amepelekwa Kamati ya Maadili kwa
kumshambulia refa kwa matusi ya nguoni.
Simba wamepigwa faini ya
sh. 500,000 kutokana na vurugu za washabiki wake wakati wa mechi dhidi ya
Kagera Sugar.
Katika FDL, mchezaji
Ally Mtoni wa Villa Squad amepigwa faini y ash. 200,000 na kufungiwa mechi
tano. Kosa lake ni kujisaidia haja ndogo golini wakti wa mechi dhidi ya Ndanda
FC iliyochezwa mjini Mtwara.
Kamishna Paul Opiyo wa
mechi ya FDL kati ya Villa Squad na Transit Camp kwa kutokuwa makini. Katika
ripoti yake ameeleza kuwa Transit Camp ilichelewa kufika uwanjani, lakini
hakusema ilichelewa kwa muda gani.
Kocha wa Polisi Dar es
Salaam, Ngelo Nyanjabha na Meneja wa timu hiyo Mrimi Masi wamepigwa faini ya
sh. 200,000 na kufungiwa mechi tatu kila mmoja kwa kuongoza kundi la washabiki
kumvamia refa wa mechi yao dhidi ya Villa Squad iliyochezwa Dar es Salaam.
Pia Bodi ya Ligi
imeagiza Polisi waandikiwe barua ya onyo kwa vile wakati waamuzi wanapigwa
walikuwepo lakini hawakutoa msaada kwa wakati.
Kocha wa Friends
Rangers, Kheri Mzozo amepigwa faini ya sh. 200,000 na kufungiwa mechi sita kwa
kosa la kumtukana refa na kutishia kuhamamisha washabiki waingie uwanjani
kufanya fujo kwenye mechi dhidi ya Villa Squad.
Naye Kocha msaidizi wa
timu ya Transit Camp, Haji Amiri amepigwa faini ya sh. 200,000 na kufungiwa
mechi sita kwa kutoa lugha ya matusi kwa mwamuzi wa akida wakati wa mechi dhidi
ya Friends Rangers.
Adhabu zote zimetolewa
kwa mujibu wa kanuni. Pia Bodi ya Ligi imeahirisha kufanya uamuzi wa mechi kati
ya Stand United na Kanembwa JKT iliyochezwa Uwanja wa Kambarage ili kukusanya
taarifa zaidi. Mechi hiyo haikumalizika. Bodi ya Ligi itakutana tena Jumapili
(Novemba 17 mwaka huu).
FUTURE TAIFA STARS vs
TAIFA STARS UWANJANI KARUME
Timu za Taifa za Future
Taifa Stars na Taifa Stars zinacheza kesho (Novemba 13 mwaka huu). Mechi hiyo
ya kirafiki itafanyika Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume jijini Dar es Salaam
kuanzia saa 10 kamili jioni.
Mechi hiyo ni maalumu
kwa Benchi la Ufundi la Taifa Stars linaloongozwa na Kim Poulsen kuangalia
wachezaji kumi kutoka Future Taifa Stars watakaoongezwa katika Taifa Stars
tayari kwa mechi ya kirafiki ya kimataifa itakayochezwa Novemba 19 mwaka huu
jijini Arusha.
Watazamaji 300 tu
wataruhusiwa kushuhudia mechi hiyo kwa kiingilio cha sh. 5,000.
Taifa Stars
inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager imeingia kambini leo (Novemba 12
mwaka huu). Miongoni mwa wachezaji wanaotarajia kuripoti ni kipa Ivo Mapunda wa
Gor Mahia.
Boniface Wambura
Kaimu Katibu Mkuu
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)