Monday, December 4, 2017

MUFINDI YABAINI WATEJA 31 WALIOJIUNGANISHIA UMEME KINYUME NA TARATIBU



Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Wilaya ya Mufindi imefanikiwa kuwabaini wateja 31 waliojiunganishia umeme kinyume na taratibu na kuchukuliwa hatua za kisheria katika jitihada za kudhibiti upotevu wa umeme na mapato ya serikali.

Kauli hiyo ilitolewa na Katibu Tawala Wilaya ya Mufindi, Allan Benard alipokuwa akisoma taarifa fupi ya Wilaya ya Mufindi kwa waziri wa Nishati aliyefanya ziara ya kukagua viwanda vya kuzalisha nguzo wilayani Mufindi hivi karibuni.

Benard alisema kuwa jumla ya wateja 9,382 walihakikiwa na kukaguliwa na kati yao, wateja 31 walibainika kuwa wamejiunganishia umeme kinyume na taratibu. Alisema kuwa wateja hao wamechukuliwa hatua za kisheria kwa kulisababishia shirika la ugavi wa umeme kukosa mapato. 

Alisema kuwa Wilaya ya Mufindi imefanikiwa kubadilisha mita zote za kawaida za umeme (convection) na kufunga mita la Luku ambazo zimesaidia kuongeza wigo wa ukusanyaji mapato.

Akiongelea viwanda wilayani Mufindi, Benard alisema kuwa Wilaya hiyo ina fursa mbalimbali za uwezeshaji wananchi kiuchumi. Alivitaja viwanda vilivyopo kwa mchanganuo kuwa, viwanda vikubwa 14, viwanda vya kati 27 na viwanda vidogo 43. Alisema kuwa viwanda hivyo vimetoa ajira kwa watu 9,171. Aliongeza kuwa kati ya hivyo, viwanda vitano vinazalisha nguzo. Alivitaja kuwa ni Sao Hill Industries, Qwihaya General Enterprises, Sheda General Supply, Leshea na Mufindi Wood Poles and Timber.

Wilaya ya Mufindi ina ukubwa wa eneo la kimometa za mraba 7,123, halmashauri mbili na majimbo matatu ya uchaguzi.    
=30=

UMEME WAKWMISHA UJENZI WA VIWANDA



Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Upungufu wa upatikanaji wa umeme umekuwa kikwazo katika juhudi za uanzishaji wa miradi ya kiuchumi na ujenzi wa viwanda mkoani Iringa.

Kauli hiyo ilitolewa na mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza alipokuwa akiwasilisha taarifa fupi ya Mkoa wa Iringa kwa waziri wa Nishati ofisini kwake jana.

Masenza alisema “mheshimiwa waziri, pamoja na utekelezaji huu wa kusukuma maendeleo ya wananchi, kumekuwa na changamoto kadhaa zinazochelewesha juhudi hizi. Baada ya wananchi kuitikia wito wa uanzishaji miradi ya kiuchumi ikiwemo ujenzi wa viwanda, pamekuwa na upungufu katika kupatikana kwa umeme wa uhakika. Maeneo yanayokumbwa na tatizo hili ni pamoja na Iringa mjini na wilaya ya Mufindi”. 

Changamoto nyingine ni miradi mikubwa ya kufua umeme inahitaji uwekezaji mkubwa na fedha nyingi, hivyo kuwa kikwazo kwa wananchi wazalendo na kushauri serikali kuwa na udhamini kwa miradi hiyo. 

Mkuu wa Mkoa alisema kuwa Mkoa utaendelea kukabiliana na changamoto hizo kwa kushirikiana na wadau kwa kuwa na ramani itakayoonesha maeneo ya viwanda. “Ramani hii ikikamilika itawasilishwa kwenye mamlaka zinazosimamia miundombinu kama umeme, maji, barabara ili kuhakikisha Mkoa unakuwa na mazingira bora na wezeshi kwa ujenzi na uendelezaji wa viwanda” alisema mkuu wa Mkoa.

Waziri wa Nishati alifanya ziara ya siku moja kukagua viwanda vinavyozalisha nguzo mkoani Iringa ili kujiridhisha na uwezo wa viwanda hivyo kuzalisha nguzo nchini.
=30=

VIWANDA 209 KUCHANGIA PATO LA MKOA IRINGA



Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Mkoa wa Iringa una viwanda 209 vinavyotoa ajira kwa zaidi ya wakazi 7,000 na kuchangia katika pato la Mkoa na Taifa.

Kauli hiyo ilitolewa na mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza ofisini kwake alipokuwa akiwasilisha taarifa fupi ya Mkoa wa Iringa kwa waziri wa Nishati, Dr Medard Kalemani wakati wa ziara yake mkoani Iringa jana.

Masenza alisema “Mkoa wa Iringa una viwanda 209 vinavyotoa ajira ya watu 7,470. Mchanganuo unaonesha viwanda 184 vilianzishwa kabla ya serikali ya awamu ya tano kuingia madarakani na viwanda 25 vilianzishwa baada yake”. 

Akiongelea viwanda hivyo kisekta, alisema kuwa Mkoa una viwanda 12 vinavyojishughulisha na uongezaji thamani katika sekta ya Nishati. Aliongeza kuwa viwanda hivyo vinazalisha umeme, nguzo za umeme, kutumia vumbi la mbao kuzalisha mkaa unaotumika viwandani na majumbani.

Mkuu wa Mkoa alisema kuwa kutokana na kuongezeka matumizi ya mazao ya miti, Mkoa kwa kushirikiana na wadau umeanzisha chuo kinachotoa mafunzo yanayohusu stadi za kilimo bora cha miti. Mafunzo yanayotolewa katika kiwanda hicho aliyataja kuwa ni jinsi ya kuchakata na kupunguza upotevu mwingi wa mazao ya miti wakati wa kuchakata, jinsi ya kupanda na kutunza miti. Mafunzo mengine aliyataja kuwa ni uandaaji wa vitalu vya miche ya miti kitaalam na kuandaa shamba la miti.

Waziri wa Nishati alifanya ziara ya siku moja kukagua viwanda vinavyozalisha nguzo mkoani Iringa ili kujiridhisha na uwezo wa viwanda hivyo kuzalisha nguzo nchini.
=30=

MAAFISA MAENDELEO WATAKIWA KUHAMASISHA UJENZI WA VYOO IRINGA



Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa-Iringa
Maafisa maendeleo ya jamii wa halmashauri watakiwa kushiriki katika kuhamasisha kampeni ya ujenzi wa vyoo ili kuwa na jamii yenye vyoo bora na isiyokuwa na magonjwa ya mlipuko.

Kauli hiyo ilitolewa na mkuu wa mkoa wa Iringa, Amina Masenza wakati akifanya majumuisho ya ziara yake ya kukagua hali ya ujenzi wa vyoo katika halmashauri ya wilaya ya Iringa jana.

Masenza alisema “kasi ya ujenzi wa vyoo bora si ya kuridhisha. Kuna haja ya kufanya tathimini ya kampeni ya ujenzi wa vyoo katika mkoa wa Iringa ili tuone jinsi ya kujipanga zaidi na kubadilisha mkakati. Lazima ufike wakati tusema katika Mkoa wa Iringa kutokuwa na choo bora mwisho”. 

Aliongeza kuwa maafisa maendeleo ya jamii hawajatumika ipasavyo katika kampeni ya ujenzi wa vyoo. Aliziagiza mamlaka za serikali za mitaa kuwatumia maafisa hao ili wasaidie uhamasishaji jamii katika ujenzi wa vyoo bora kwa wananchi. Aidha, aliwataka watendaji wa Kata na Vijiji kutekeleza wajibu wao katika kusimamia ujenzi wa vyoo katika maeneo yao ili zoezi hilo likamilike mapema.

Wakati huohuo, kaimu afisa mazingira katika ofisi ya mkuu wa Mkoa wa Iringa, Hawa Mwechaga alisema kuwa baadhi ya vyoo vinavyojengwa ni vidogo kiasi cha kutosha kuwahifadhi watu wembamba pekee. Alishauri kuwa wananchi waelimishwe na kusimamiwa ili wajenge vyoo vyenye nafasi ya kutosha kuweza kuwahifadhi hata watu wanene. Alisema kuwa choo ni muhimu kiwe na nafasi kwa sababu kinamsitiri na kumuhifadhi mtumiaji wake.

Mkuu wa mkoa wa Iringa alifanya ziara ya kukagua hali ya usafi wa mazingira na ujenzi wa vyoo katika kata za Isakalilo, Mseke na Mgama katika halmashauri ya wilaya ya Iringa
=30=

WANAFUNZI WANUFAIKA WA TASAF WATAKIWA KUWASHIRIKISHA WALIMU MASUALA YA TAALUMA



Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Wanafunzi wanufaika wa mpango wa kunusuku kaya masikini nchini (TASAF) kupitia ruzuku ya elimu wametakiwa kuwashirikisha walimu katika masuala yanayohusu taaluma na ustawi wao ili waweze kufaulu.

Kauli hiyo ilitolewa na Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Wamoja Ayubu alipokuwa akiongea na wanafunzi wanufaika wa TASAF wa shule ya msingi Kitwiru iliyopo Kata ya Kitwiru Manispaa ya Iringa hivi karibuni.

Ayubu alisema “watoto wangu mpo hapa kwa ajili ya kusoma na wote kufaulu, si ndiyo. Walimu wenu wapo hapa kwa ajili ya kuwafundisha na kuwasaidia kufaulu hivyo msiwaogope. Wafuateni kwa ushauri na maelekezo ili muweze kusoma vizuri na wote kufaulu, sawa”. 

Alisema kuwa serikali inatoa fedha kwa wanafunzi hao kiasi cha shilingi 2,000 kwa mwezi ili waweze kununua mahitaji ya muhimu ya shule. Serikali inataka kuona kila mtoto wa kitanzania anasoma vizuri ili aweze kujitegemea na kuchangia katika kukuza pato la Taifa.

Nae mratibu wa TASAF Mkoa wa Iringa, William Kingazi aliwataka wanafunzi hao kusoma kwa bidii na kuwa wasikivu kwa walimu na wazazi. “Nyie wanafunzi lazima muwe na ndoto kwamba mtakapomaliza masomo mnataka kuwa watu wa aina gani. Ndoto hizo ziwasaidie kusoma kwa bidii ili muweze kuzifikia” alisema Kingazi. 

Aidha, aliwataka walimu kuwafuatilia wazazi wanufaika wa mpango wa TASAF ili waweze kuwanunulia watoto sare za shule kwa wale ambazo sare zao zimechanika ili wasijione tofauti na wengine.

Katibu Tawala Mkoa wa Iringa alifanya ziara maalum ya ufuatiliaji kwa wanafunzi wanufaika wa mpango wa TASAF kupitia elimu katika Manispaa ya Iringa kujifunza changamoto zinazowakabili. Katika ziara hiyo aliambatana na mratibu wa TASAF Mkoa, afisa mipango, mhasibu, mkaguzi wa ndani na afisa habari.
=30=