HOSPITALI YA MKOA IRINGA YAPONGEZWA
Hospitali ya Mkoa wa Iringa imepongezwa kwa kutoa huduma nzuri kwa wagonjwa wanaohudhuria hospitali hiyo kwa matibabu.
Pongezi hizo zimetolewa na Mbunge wa viti maalum kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Ritta Semotto Kabati alipofanya ziara fupi ya kuwatembelea wagonjwa waliolazwa katika wodi ya akina mama na wodi ya watoto leo kwa lengo la kuwapa pole, na kuwatakia heri ya mwaka mpya 2011.
Mhe. Ritta Kabati, Mbunge wa CCM viti maalum (kulia) akimkabidhi baadhi ya zawadi
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa wa Iringa, Dkt. Oscar Gabone
katika viwanja vya Hospitali hiyo leo
Mhe. Kabati amesema “naipongeza hospitali ya mkoa wa Iringa kwa kutoa huduma nzuri na bora jambo linalowafanya wagonjwa kuridhika na huduma inayotolewa”. Ameongeza kuwa ametembelea hospitali mbalimbali lakini katika suala la usafi hospitali ya mkoa ipo juu.
Mhe. Kabati amesema lengo la kufanya ziara hiyo fupi ni kuwafariji na kuwatia moyo akina mama na watoto na kuwapa zawadi mbalimbali ikiwa ni pongezi zake kwa kufanikiwa kuuona mwaka mpya wa 2011. “Nawapa pole sana wagonjwa wote na nawatakia afya njema kwani kuugua si kufa na pia naomba wote tuuanze huu mwaka mpya kwa furaha na uwajibikaji ili kuweza kujiletea maendeleo”.
Sikujua Filango, mama aliyejifungua mtoto saa tisa usiku wa tarehe 01.01.2011 ameelezea kurithishwa na huduma za hospitalini hapo tangu alipowasili hadi alipojifungua.
Akielezea changamoto zinazoikabili hospitali ya mkoa, Katibu wa Hospitali, Dotto Zambalesi amesema kuwa hospitali hiyo inakabiliwa na upungufu wa watumishi wenye taaluma stahiki akidai waliopo kuwa ni wachache hatimae kuwa na jukumu zito kidogo kwa wataalamu waliopo kuweza kuziba pengo la watumishi wanaopungua. Aidha changamoto nyingine ameiongelea kuwa ni ufinyu wa bajeti jambo linalokwamisha ufanisi katika baadhi ya shughuli.
Mhe. Rita Kabati Mbunge viti maalum CCM (katikati) akiwa na
mama Felisha (kushoto) na mama ambaye mtoto hajampatia jina (kulia)
baada ya kuwakabidhi zawadi alipotembelea wodi ya akina mama leo
Akitoa shukrani zake kwa ziara hiyo mganga mfawidhi wa hospitali hiyo Dkt. Oscar Gabone amemshukuru Mhe. Mbunge na msafara wake na zawadi walizozitoa katika wodi ya akina mama na wodi ya watoto na kueleza matumaini yake kuwa ziara ijayo itahusisha zawadi za akina baba pia.