MKOA WA IRINGA UMELENGA KULINDA AFYA ZA WATUMISHI NA FAMILIA ZAO
Mkakati wa Mkoa wa Iringa wa kudhibiti UKIMWI unalenga kutekeleza mipango endelevu ya kupambana na UKIMWI mahala pa kazi hususani suala zima la kutoa elimu kuhusu maambukizi ya VVU na UKIMWI kwa watumishi ili kulinda afya zao na familia zao.
Taarifa hiyo imetolewa na Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Mama Gertrude Mpaka katika maadhimisho maalumu ya siku ya familia na UKIMWI mahala pa kazi kwa watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa yaliyofanyika katika viwanja vya ‘riverside campsite’ nje kidogo ya viunga vya Halmashauri ya wilaya ya Iringa.
Mama Mpaka amesema kuwa Mkoa wa Iringa uliandaa mpango mkakati wa miaka minne wa kudhibiti UKIMWI ukiwa na lengo la “kutoa elimu ya maambukizi ya VVU na UKIMWI kwa watumishi ili kulinda afya zao na familia zao na kupunguza unyanyapaa kwa wafanyakazi waishio na virusi vya UKIMWI”. Aidha ameongeza kuwa mkakati wa Mkoa unalenga pia kupunguza maambukizi na uwezekano wa maambukizi katika mahala pa kazi kwa manufaa ya wafanyakazi, familia na jamii kwa ujumla wake.
Katibu Tawala Mkoa amekumbusha kuwa Mkoa wa Iringa ndio unaoongoza kwa kiwango kikubwa cha maambukizi ya VVU na UKIMWI nchini ukilinganisha na mikoa mingine ambao unawastani wa asilimia 15.7 ya maambukizi. Aidha madhara ya janga hili ni makubwa sana katika sekta zote na ngazi ya familia na jamii kwa ujumla.
Alichukua fursa hiyo kuwataka watumishi hao kuzingatia mada zitakazofundishwa katika maadhimisho hayo ili yaweze kusaidia kupunguza kasi ya maambukizi ya VVU na UKIMWI na kuongeza nguvu kazi itakayoendeleza mkoa wa Iringa. Pia aliahidi kuongeza bajeti ya siku ya familia na mapambano dhidi ya UKIMWI mahapa pa kazi ili pamoja na mambo mengine ijumuishe na michezo ya bonanza toka kwa watumishi katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa.
Nae mratibu wa maadhimisho ya siku ya familia na mapambano dhidi ya UKIMWI mahala pa kazi mkoani, Samwel Nyagawa amesema kuwa mapambano dhidi ya UKIMWI mahala pa kazi ni eneo muhimu sana lililoainishwa katika mpango mkakati wa Mkoa wa niaka minne yaani 2008- 2012 wa kupambana na maambukizi ya UKIMWI unaomtaka kila mwajiri katika Mkoa wa Iringa kutenga muda ambao watumishi wake watakutana na kujadili kwa mapana jitihada za mapambano dhidi ya UKIMWI mahala pa kazi.