Wednesday, December 12, 2012




HOTUBA YA MGENI RASMI MKUU WA MKOA WA IRINGA KATIKA UZINDUZI WA MRADI WA KAZI NJE-NJE KWA MKOA WA IRINGA TAREHE 12/12/2012 KATIKA UKUMBI WA CHUO KIKUU HURIA IRINGA.

Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya ya Iringa,
Mhe. Mstahiki Meya wa Manispaa ya Iringa,
Mhe. Kaimu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa,
Mkurugenzi PROMISE Tanzania,
Viongozi wa Serikali,
Viongozi wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, Viongozi wa Taasisi za Dini,
Mabibi na Mabwana.

Awali ya yote natumia fursa hii kutoa shukrani kwa waandaaji wa uzinduzi wa mradi huu ambao una umuhimu mkubwa kwa maendeleo ya Vijana wa Mkoa wa Iringa.

Aidha, nawakaribisha wote katika uzinduzi wa mradi huu, mradi huu binafsi, nimeupenda kwa kuwa malengo yake ni kuelimisha kundi kubwa la Vijana ili liweze kujiajiri na kufanya kazi kwa maendeleo ya Taifa.

Nawashukuru PROMISE kwa kushirikiana na ILO kwa kuandaa mpango huu wa kusaidia vijana kupitia Mradi wa Kazi Nje - Nje kwa Vijana wa Mkoa wa Iringa, hususani kwa Manispaa ya Iringa na Halmashauri ya Wilaya ya Iringa.

Ndugu Washiriki, Wageni Waalikwa Mabibi na Mabwana,

Mpango wa Mradi huu wa kazi Nje - Nje kwa vijana ambao umepewa jina la Oparesheni Moto wa Nyika, ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuwasaidia Vijana kupata ajira au kujiajiri wenyewe ili waweze kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa Taifa letu, na kufikia lengo la maisha bora kwa kila Mtanzania. Hivyo, napenda kuwapongeza kwa kuanzisha mpango huu katika Mkoa wa Iringa.
Mpango huu katika Mkoa wa Iringa utawasaidia Vijana namna ya kubuni, kuendeleza  na kutekeleza wazo la biashara au ujasiriamali  kwa kujua jinsi ya kutayarisha mpango na namna ya kupata  huduma toka katika taasisi za fedha.

Ndugu Washiriki, Wageni Waalikwa Mabibi na Mabwana,

Sote tunatambua kwamba, vijana wengi mijini na vijijini wamekuwa hawajitumi na hawana ajira ya kueleweka, hii imesababisha vijana wengi kujiingiza katika uhalifu,madawa ya kulevya,kukaa tu kwa muda wote bila ya kujishughulisha  na kusababisha kuzorota kwa maendeleo.
Pia, wimbi kubwa la Vijana wanakimbilia Mijini kutoka vijijini wakiamini kwamba mijini kunakazi na maisha mazuri. Ni ukweli usiopingika vijana hawa wakifika mijini huhangaika na kurandaranda mitaani.

Ndugu Washiriki, Wageni Waalikwa Mabibi na Mabwana,

Vijana hawa wakipata elimu ya kutosha hususani elimu ya ujasiliamali, watakuwa wazalishaji wakubwa katika maeneo ya mijini/vijijini na watajikwamua katika hali ya umaskini na Taifa letu litasonga mbele. Naamini, kupitia mpango huu tutapunguza wimbi la wahalifu na wazururaji na pia tutapunguza Vijana wanaokimbilia Mijini kutafuta kazi.

Ndugu Washiriki, Wageni Waalikwa Mabibi na Mabwana,

Napenda kuwaambia vijana kuitumia vizuri sana fursa hii ambayo ni adimu; wajitokeze kwa wingi kushiriki katika mpango huu wa kuwainua kimaisha. Wewe kijana unayenisikia mwambie na mwenzio habari hii njema  ili  vijana wote Mkoani Iringa muweze kujikomboa kwa kupitia mpango huu.  Nchi yetu  ya Tanzania tunawataka vijana wote kufanya kazi kwa bidii, hususani kazi za uzalishaji. Tunawahamasisha vijana kujiunga katika vikundi mbalimbali vya uzalishaji kama Kilimo. Ufugaji,Ufugaji Nyuki, Samaki, Uanzishaji wa Viwanda Vidogo Vidogo vya usindikaji n.k. Kupitia Vikundi hivyo, Vijana watakuwa na uwezo wa kufanya kazi kwa ushirikiano mkubwa na hatimae kufanikiwa kimaisha. 

Vijana wakijiunga katika vikundi vya uzalishaji ni rahisi kukopeshwa mitaji ambayo itawasaidia kusonga mbele. Mfano wa mitaji hiyo ni mikopo ya fedha kutoka kwenye Taasisi za Kifedha (benki na SACCOS) na Taasisi nyingine nyingi au Mikopo ya Matrekta kupitia Mpango wa Kilimo Kwanza (SUMA J.K.T.), n.k.
Nawasihi PROMISE kuwa mpango huu usambae Wilaya zote za Mkoa wa Iringa na kuweza kuwafikia vijana wengi.

Ndugu Washiriki, Wageni Waalikwa Mabibi na Mabwana,

Kwa nafasi hii pia naomba Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, taasisi mbali mbali zikiwemo za Vyuo Vikuu na Mashirika ya Dini katika Mkoa wa Iringa kuiga mfano huu wa kusaidia na kuinua maendeleo ya vijana, kwani vijana ndiyo nguvu kazi ya Taifa lolote duniani hivyo tunapaswa kuwaelekeza na  kuwawezesha.

Ndugu Washiriki, Wageni Waalikwa Mabibi na Mabwana,

Kabla ya kuzindua mpango huu rasmi, niwaase Vijana wa Mkoa wa Iringa mjitokeze kwa wingi na kuwa karibu sana PROMISE ili kujua utaratibu kamili kuhusiana na mafunzo haya ambayo yanatolewa bure kwa vijana wote. 

Pia nawasihi Mashirika Yasiyo ya Kiserikali  ni vyema kubuni mikakati mizuri ya kuisaidia jamii kwa kushirikiana na Serikali.nawashukuru wale wote, wanaoendelea na jamii katika maendeleo yao.
Kipekee, nawashukuru na kuwapongeza PROMISE na ILO kwa kuandaa mpango huu, na kuwaomba waendelee kusaidia vijana kama walivyokusudia. Mara tu mtakapowafundisha na kuwaelekeza Vijana naomba pamoja na Halmashauri husika kufanya tahmini kubaini waliofanikiwa na mpango huu.
Ndugu Washiriki,   Mwisho, 

Baada ya kusema haya yote, napenda nitamuake rasmi kuwa mpango huu wa Kazi Nje - Nje kwa vijana wa Mkoa wa Iringa.

UMEZINDULIWA RASMI.

Asanteni kwa kunisikiliza.

MKOA WAHIMIZA KILIMO CHA UMWAGILIAJI MAJI





Mkoa wa Iringa umedhamilia kuhakikisha kilimo kinainuka na kukua zaidi kwa kuhamasisha matumizi ya zana bora za kilimo kwa lengo la kumletea maendeleo mwananchi kupitia sekta ya kilimo.

Rai hiyo imetolewa na Mhandisi wa Kilimo, Victor Byanjweli wakati akifafanua mipango ya Mkoa katika kukuza kilimo na kukifanya kiwe cha kisasa katika mkutano wa hadhara katika kijiji cha Ifunda kilichopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Iringa.

Mhandisi Byanjweli amesema kuwa kilimo ni sekta kubwa inayoajiri idadi kubwa ya wananchi katika mkoa wa Iringa, kwa msingi huo uongozi wa mkoa umedhamilia kuhakikisha kilimo kinasonga mbele na kuwaletea maendeleo makubwa wananchi wake. Amesema katika kuhakikisha hilo, Mkoa unaendelea kuhamasisha matumizi ya zana bora za kilimo kwa lengo la kumletea maendeleo mwananchi. Amezitaja zana hizo kuwa ni pamoja na matrekta makubwa na madogo na kilimo cha kutumia wanyama kazi. 

Mhandisi Byanjweli ambaye pia amebobea katika umwagiliaji na zana za kilimo amesema kuwa mkakati mwingine wa Mkoa ni kuhakikisha kilimo kinakua kupitia kilimo cha umwagiliaji. Amesema kutokana na mabadiliko ya tabia nchi na tabia za kibinadamu za ukataji miti ovyo, sehemu kubwa ya Mkoa wa Iringa imekuwa ikipata ukame mkubwa kutokana na upungufu wa mvua usio wa kawaida, Mkoa unahimiza kilimo cha umwagiliaji ili kuondokana na changamoto ya upungufu wa chakula. 

Mhandisi Byanjweli amesema kuwa kupitia kilimo cha umwagiliaji Mkoa utakuwa na uhakika wa chakula na kuondokana na aibu ya kuomba chakula cha njaa.

Wakati huohuo, Afisa Elimu Mkuu, Mwl. Euzebio Mtavangu ametoa wito kwa ubia baina ya walimu na wazazi katika kuhakikisha mwanafunzi anahudumiwa na kulelewa vizuri ili aweze kufanya vizuri katika masomo yao. Amesema miongoni mwa ubai huo ni kuhakikisha kuwa wazazi wanawapokea vizuri walimu wanaopangiwa katika maeneo yao jambo litakalowafanya walimu hao nao kujiona ni miongoni mwa wanajamii na wazazi wa wanafunzi wao. Amesema kufanya hivyo si tu kunamchango kwa mwalimu kujisikia yupo nyumbani na mikononi mwa watu wanaomjali lakini pia kwa utoaji mzuri wa elimu kwa wanafunzi.

Aidha, amewataka wazazi kuhakikisha wanajipanga na kuwapatia wanafunzi chakula cha mchana. Akielezea umuhimu wa chakula cha mchana kwa wanafunzi, Afisa Elimu Mkuu amesema kuwa wanafunzi wanapokula chakula cha mchana kunawasaidia kurudi katika hali ya kawaida na kuondokana na njaa na uchovu jambo linalowafanya wasome kwa bidii na maarifa. Amesema kuwa mwanafunzi anapokuwa ameshiba hata uwezo wa kufikiri na kufaulu unaongezeka sambamba na kupunguza utoro usio wa lazima.

Akihitinisha mkutano huo, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma amewataka wananchi wa kijiji cha Ifunda kuhakikisha wanaunda vikundi kwa ajili ya shughuli za kiuchumi na kuimarisha vyama vya kuweka na kukopa Saccos kwa manufaa yao. Amesema kuwa Serikali muda si mrefu pembejeo zitapitishiwa katika Saccos imara hivyo wananchi watakao mufaika ni wale watakao kuwa wamejiunga katika saccos hizo. Amesema kuwa mkoa wake unahamasisha uundaji wa vikundi vya vijana na vikundi vya kiuchumi kwa malengo ya kuwafanya wananchi wawe na vikundi vya kuzalisha mali kwa kuunganisha nguvu pamoja. Amesema kuwa umoja ni nguvu hivyo watu wakiwa pamoja ni tofauti na anavyokuwa mtu mmoja mmoja.
=30=