Mkoa
wa Iringa umedhamilia kuhakikisha kilimo kinainuka na kukua zaidi kwa
kuhamasisha matumizi ya zana bora za kilimo kwa lengo la kumletea maendeleo
mwananchi kupitia sekta ya kilimo.
Rai
hiyo imetolewa na Mhandisi wa Kilimo, Victor Byanjweli wakati akifafanua
mipango ya Mkoa katika kukuza kilimo na kukifanya kiwe cha kisasa katika
mkutano wa hadhara katika kijiji cha Ifunda kilichopo katika Halmashauri ya
Wilaya ya Iringa.
Mhandisi
Byanjweli amesema kuwa kilimo ni sekta kubwa inayoajiri idadi kubwa ya wananchi
katika mkoa wa Iringa, kwa msingi huo uongozi wa mkoa umedhamilia kuhakikisha
kilimo kinasonga mbele na kuwaletea maendeleo makubwa wananchi wake. Amesema
katika kuhakikisha hilo, Mkoa unaendelea kuhamasisha matumizi ya zana bora za
kilimo kwa lengo la kumletea maendeleo mwananchi. Amezitaja zana hizo kuwa ni
pamoja na matrekta makubwa na madogo na kilimo cha kutumia wanyama kazi.
Mhandisi
Byanjweli ambaye pia amebobea katika umwagiliaji na zana za kilimo amesema kuwa
mkakati mwingine wa Mkoa ni kuhakikisha kilimo kinakua kupitia kilimo cha
umwagiliaji. Amesema kutokana na mabadiliko ya tabia nchi na tabia za
kibinadamu za ukataji miti ovyo, sehemu kubwa ya Mkoa wa Iringa imekuwa ikipata
ukame mkubwa kutokana na upungufu wa mvua usio wa kawaida, Mkoa unahimiza
kilimo cha umwagiliaji ili kuondokana na changamoto ya upungufu wa chakula.
Mhandisi Byanjweli amesema kuwa kupitia kilimo cha umwagiliaji Mkoa utakuwa na uhakika wa chakula na kuondokana na aibu ya kuomba chakula cha njaa.
Wakati
huohuo, Afisa Elimu Mkuu, Mwl. Euzebio Mtavangu ametoa wito kwa ubia baina ya
walimu na wazazi katika kuhakikisha mwanafunzi anahudumiwa na kulelewa vizuri
ili aweze kufanya vizuri katika masomo yao. Amesema miongoni mwa ubai huo ni
kuhakikisha kuwa wazazi wanawapokea vizuri walimu wanaopangiwa katika maeneo
yao jambo litakalowafanya walimu hao nao kujiona ni miongoni mwa wanajamii na
wazazi wa wanafunzi wao. Amesema kufanya hivyo si tu kunamchango kwa mwalimu
kujisikia yupo nyumbani na mikononi mwa watu wanaomjali lakini pia kwa utoaji
mzuri wa elimu kwa wanafunzi.
Aidha,
amewataka wazazi kuhakikisha wanajipanga na kuwapatia wanafunzi chakula cha
mchana. Akielezea umuhimu wa chakula cha mchana kwa wanafunzi, Afisa Elimu Mkuu
amesema kuwa wanafunzi wanapokula chakula cha mchana kunawasaidia kurudi katika
hali ya kawaida na kuondokana na njaa na uchovu jambo linalowafanya wasome kwa
bidii na maarifa. Amesema kuwa mwanafunzi anapokuwa ameshiba hata uwezo wa
kufikiri na kufaulu unaongezeka sambamba na kupunguza utoro usio wa lazima.
Akihitinisha
mkutano huo, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma amewataka
wananchi wa kijiji cha Ifunda kuhakikisha wanaunda vikundi kwa ajili ya
shughuli za kiuchumi na kuimarisha vyama vya kuweka na kukopa Saccos kwa
manufaa yao. Amesema kuwa Serikali muda si mrefu pembejeo zitapitishiwa katika
Saccos imara hivyo wananchi watakao mufaika ni wale watakao kuwa wamejiunga
katika saccos hizo. Amesema kuwa mkoa wake unahamasisha uundaji wa vikundi vya
vijana na vikundi vya kiuchumi kwa malengo ya kuwafanya wananchi wawe na
vikundi vya kuzalisha mali kwa kuunganisha nguvu pamoja. Amesema kuwa umoja ni
nguvu hivyo watu wakiwa pamoja ni tofauti na anavyokuwa mtu mmoja mmoja.
=30=
No comments:
Post a Comment