Na. Ofisi ya
Mkuu wa Mkoa, Iringa
Mkoa wa Iringa unatekeleza agizo la serikali ya
awamu ya tano la kuufanya ushirika kuwa nguzo ya kuwasaidia wakulima.
Kauli hiyo ilitolewa na kaimu Mrajis msaidizi wa
vyama vya ushirika mkoa wa Iringa, Robert George alipokuwa akisoma taarifa ya
hali ya ushirika katika mkoa wa Iringa katika jukwaa la ushirika mkoa wa Iringa
lililofanyika katika ukumbi wa Siasa ni Kilimo mjini Iringa hivi karibuni.
Kaimu Mrajis Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Iringa, Robert George |
George alisema kuwa mkoa unaendelea kutekeleza
agizo la serikali la kujenga ushirika imara unaomsaidia mkulima.
“Katika
kuhakikisha kuwa ushirika unakuwa imara na kuongeza idadi ya wanachama kama
lilivyo agizo la Serikali ya awamu ya tano ambalo linatuhitaji sisi kama
wasimamizi wa ushirika kuhakikisha kuwa ushirika unakuwa ndio nguzo ya
kumsaidia mkulima. Kwa mwaka 2017/2018 jumla ya vyama vya ushirika 8
vimeandikishwa zikiwepo SACCOS 5 na
AMCOS 3” alisema George.
Uhamasishaji wa vyama vilivyosinzia ili viweze
kuamka umefanyika kupitia chama kikuu cha ushirika na maafisa ushirika, jumla
ya vyama vya ushirika vitano vimeamka ambavyo ni Magulilwa AMCOS Ltd, Ipilimo
AMCOS Ltd, Matanana AMCOS Ltd, MVIKIMA SACCOS Ltd na Ikimo AMCOS Ltd.
Akiongelea utekelezaji wa maagizo ya serikali
kuhusu mazao ya kimkakati, Mrajis msaidizi mkoa wa Iringa alisema kuwa halmashauri
zimehamasisha kilimo cha mazao ya korosho na pamba katika kata za Nzihi na
Malengamakali kupitia vyama vya ushirika vya Nzihi mixed na Usolanga.
Aliongeza kuwa mkoa unaendelea kusimamia na
kuviimarisha vyama vya ushirika vitatu vinavyojishughulisha na kilimo cha chai.
Vyama hivyo alivitaja kuwa ni Mkonge Amcos, Sawala Amcos na Luhunga Amcos.
“Kwa mwaka 2017/2018 jumla ya vijiji vitano vimehamasishwa
kuanzisha vyama vya ushirika vya kilimo cha chai katika halmashauri ya Mufindi.
Vijiji hivyo ni Igoda, Kibao, Udumka, Mninga na Makalala” alisema George.
Halmashauri zinaendelea kuhamasisha kilimo cha kahawa,
korosho na pamba aliongeza. “Kwa msimu
huu wa mwaka 2017/2018 wakulima wa halmashauri wilaya ya Iringa wamepanda
karosho kwa wingi hivyo, kwa maeneo yote yaliooteshwa korosho uhamasishaji wa
kuanzisha vyama vya ushirika utafanyika katika msimu wa 2018/2019. Kutokana na
jiografia ya maeneo mbalimbali ndani ya mkoa wetu mazao yote ya kimkakati
yanaweza yakastawishwa na wanachama wa vyama vya ushirika” alisema George.
Jukwaa la ushirika ni jukwaa la pili kufanyika
ngazi ya mkoa, likishirikisha Katibu Tawala Mkoa, wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi
wa mamlaka za serikali za mitaa, wadau wa taasisi za kifedha na wanaushirika.
=30=
No comments:
Post a Comment