Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Ongezeko kubwa la idadi ya watu
katika manispaa ya Iringa linaenda sambamba na ongezeko la shughuli kuichumi
hatimae kusababisha kuongezeka kwa mahitaji na matumizi ya ardhi.
|
Afisa Mipango Miji wa Manispaa ya Iringa, Immaculate Senje |
Kauli hiyo imetolewa na Afisa Mipango
Miji wa Manispaa ya Iringa, Immaculate Senje alipokuwa akiwasilisha mada ya
Mpango kamambe wa mji wa Iringa (Iringa Master Plan) 2015-2035 katika mkutano wa wadau wa maandalizi ya Mpango Kamambe
wa Mji wa Iringa uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa shule ya sekondari ya
Lugalo.
Senje amelitaja ongezeko la idadi ya
watu katika mji wa Iringa linaloenda sambamba na ongezeko la shughuli za
kiuchumi linasababisha kuongezeka kwa mahitaji na tumizi ya ardhi. Amesema ili
kukabiliana na ongezeko la mahitaji ya matumizi ya ardhi upo umuhimu wa kuwa na
mwongozo unaotoa dira ya ukuaji wa mji ambao ni endelevu.
Akiongelea matumizi ya ardhi, Afisa
Mipango Miji wa Manispaa ya Iringa amesema kuwa mji wa Iringa kama ilivyo miji
mingine nchini unayo maeneo ya makazi yaliyopangwa na kupimwa pamoja nay ale
yanayoenelezwa kiholela. Amesema kuwa eneo la makazi lililopangwa wakati wa
ukoloni liko katika makundi matatu ambayo ni ujazo wa chini, ujazo wa kati na
ujazo wa juu.
Akiongelea maeneo ambayo
yameendelezwa kiholela, ameyataja maeneo hayo kuwa yanapatikana katika kata za
Mwangata, Ruaha, Mkwawa, Mtwivila, Kihesa na Nduli. Amesema kuwa yapo maeneo ya
vijiji vilivyoingia katika Manispaa siku za karibuni kama Kigonzile, Nduli,
Mgongo, Mkoga na kitongoji cha Ulonge kuwa yana makazi yaliyotawanyika.
Akielezea matarajio yake baada ya
mkutano, Senje amesema kuwa masuala muhimu, kero na changamoto zinazowakabili
wakazi wa Iringa zitaibuliwa na kuwa msingi mkuu utakaoongoza uandaaji wa
Mpango Kamambe utakaokidhi mahitaji ya wakazi wa Manispaa ya Iringa.
=30=