Halmashauri za Wilaya na Manispaa zimeshauriwa kuwasaidia
wakulima na wajasiliamali wasindikaji katika kuhakikisha bidhaa zao zinafikia
viwango vya ubora vinavyotakiwa ili kujihakikishia soko la uhakika.
Ushauri huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt.
Christine Ishengoma alipotembelea mabanda ya wajasiliamali na wasindikaji
katika maonesho ya Nanenane katika Uwanja wa John Mwakangale -Uyole Mbeya
katika siku ya Iringa Day.
Dkt. Christine amesema kuwa wakulima wasindikaji wanafanya
kazi kubwa sana katika kusindika bidhaa za kilimo kwa kutumia juhudi zao
wenyewe, hivyo kujikuta wakikwama katika utaalam na kushauri wawe wanapatiwa
mafunzo na ushauri wa kitaalam ili kuufanya usindikaji wao uwe wa kisasa zaidi.
Amesema ni vizuri Halmashauri za Manispaa na Wilaya ziangalie
jinsi ya kuwasaidia kitaalam na kiufundi ili bidhaa za usindikaji ziweze
kufikia viwango vinavyokubalika na kupata lebo ya shirika la ubora (TBS). “watu
wengi sasa wanaangalia lebo ya TBS ili kijihakikishia ubora hivyo ni vizuri
mkahakikisha bidhaa zenu zinafikia ubora unaopkubalika na kupata lebo ya ubora”
amesisitiza Dkt. Christine.
Akiongelea changamoto zinazowakabili wajasiliamali
wasindikaji, mjasiliamali na mmiliki wa Fama Food Processing, Genovefa Barnabas
amesema kuwa changamoto kubwa inayowakabili wajasiliamali hasa wa Mkoa wa
Iringa ni maeneo mahususi ya kuwawezesha kuzalishia bidhaa zao ili ziweze
kupata uthibitisho wa ubora unmaotakiwa.
Akifafanua zaidi amesema “ili mjasiliamali anu wajasiliamali tuweze kutimiza
ndoto zetu za kufanya shughuli za ujasiliamali vizuri ni vizuri serikali
ikatusaidia kutenga maeneo ambayo yatakuwa mahususi kwa shughuli za
ujasiliamali ambapo kila kitu kitakuwa kinafanyika hapo”. Amesema “kuanzia
mazao na bidhaa zinapoletwa kutoka maeneo mbalimbali zinapokelewa katika eneo
hilo, zinaanza kutengenezwa katika eneo hilo, zinapakiwa katika kontena,
kufungwa na kuwekwa lebo hapohapo, kwa lugha nyingine mchakato wote unafanyika
katika eneo moja hadi kwenda kwa mlaji”.
Akitetea umuhimu wa eneo hilo kwa wajasiliamali, Barnabas
amesema kuwa eneo hilo lina umuhimu mkubwa kwa sababu kupatikana kwake
kutawawezesha kupata cheti cha ubora wa bidhaa toka shirika la viwango (TBS).
Amesema kitendo cha kupata lebo ya ubora toka TBS kutawafanya watu wengi zaidi
kujiridhisha na ubora wa bidhaa hizo.
Nunu Mtatifikolo ambaye ni Mwenyekiti kikundi cha Wanawake
cha JAFAKU amesema changamoto ya watanzania kukubali bidhaa zinazozalishwa na
wajasiliamali wazalendo wa ndani ni mwiba katika ukuaji wao. “amesema ipo
kasumba inayoendelea kutudidimiza ya wananchi kupenda bidhaa za nje tofauti na
zinazozalishwa na wajasiliamali wa ndani”.
Amesema ili kuondokana na kasumba hiyo elimu inahitajika
kutolewa kwa wananchi ili waweze kutumia bidhaa zinazozalishwa ndani ya nchi. “Elimu
hiyo itasaidia sana kubadili kasumba hii na elimu hii inatakiwa kuambatana na
matangazo ya bidhaa za wajasiliamali” amesisitiza Mtatifikolo.
Mwenyekiti wa kikundi cha Wanawake wa KKKT-Nduli, Laurencia
Malila amesema katika banda la Manispaa ya Iringa amesema kuwa wanawake
wajasiliamali Mkoani Iringa wanakabiliwa na changamoto ya masoko kwa maana ya
wanunuzi wa bidhaa zao. Amesema “pamoja na kuwa na bidhaa nzuri bado wananchi
wanamuitikio mdogo wa kuzinunua jambo linalowafanya washindwe kuzalisha bidhaa
kwa wingi”.
Malila ambaye pia kikundi chake kinajihusisha na kilimo cha
kisasa na ufugaji wa nyuki kikiwa na mizinga 47 ya nyuki ya kisasa, ametoa wito
kwa watu wanaopenda kujifunza kilimo cha kisasa cha mahindi na maharage pamoja
na ufugaji wa nyuki kuwatenbelea ili kujifunza katika mashamba darasa yao
yaliyopo katika kata ya Nduli.
=30=