Thursday, January 18, 2018

MAAFISA UGANI WATAKIWA KITIMIZA WAJIBU KUHAMASISHA KILIMO CHA KOROSHO IRINGA



Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Maafisa ugani katika maeneo yanayolima zao la korosho wilayani Iringa wametakiwa kutimiza wajibu wao katika kukifanya kilimo cha korosho kuwa chenye tija.

Kauli hiyo ilitolewa na mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza alipokuwa akizindua kilimo cha zao la koroso katika kijiji cha Idodi wilayani Iringa jana.

Mkuu wa Mkoa wa Iringa aliwataka maafisa ugani na viongozi wa serikali kuanzia ngazi ya kijiji hadi tarafa wa maeneo yanayolima zao la korosho kutimiza wajibu wao katika kulifanya zao hilo kuwa na tija. 

Tunataka Mkoa ufanikiwe katika kilimo cha zao hili na ushauri wangu itungwe sheria ndogo itakayomlazimisha kila mkulima kushiriki katika kilimo hiki kinachotarajiwa pia kuchochea uanzishwaji wa viwanda vya kubangua korosho,” alisema mkuu wa Mkoa.

Vilevile, aliwataka viongozi hao kuanzisha mashamba darasa yatakayotumika kihamasisha wananchi na kutumika kwa mafunzo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, Robert Masunya alisema kuwa Halmashauri yake imezalisha miche 69,855 itakayotolewa bure kwa shule za msingi na sekondari na wananchi walio tayari kwa mashamba yao kupandwa. Alisema kuwa bodi ya korosho imedhamini upatikanaji wa miche hizo ili kuhamasisha zao hilo wilayani Iringa.

Masunya alisema kuwa katika awamu ya kwanza ya utekelezaji wa mpango huo shule za msingi zitapewa miche 3,672 itakayopandwa katika mashamba ya ekari 136. Aliongeza kuwa eneo la ekari 14 linalomilikiwa shule za sekondari litapandwa miche 378. Aliongeza kuwa wananchi watapewa miche 65,803 itakayopandwa katika eneo la ekari 2,437.

Vijiji vitakavyo zao la korosho linaweza kustawi ni Idodi, Mahuninga, Mlowa, Ilolompya, Mlenge, Itunundu, Kising’a, Kihorogota, Nyang’oro, Nzihi na Kiwele.
=30=

IRINGA WATAKIWA KUTUMIA FURSA YA KULIMA ZAO LA KOROSHO



Na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Wananchi wilayani Iringa wametakiwa kuitumia vizuri fursa ya kilimo cha zao la korosho ili kuweza kujiongezea kipato.

Kauli hiyo ilitolewa na mkuu wa mkoa wa Iringa, Amina Masenza alipokuwa akizindua kilimo cha zao la korosho katika kijiji cha Idodi wilayani Iringa jana.

Masenza aliwataka wananchi kutumia kilimo cha zao la korosho kama fursa ya kuondokana na umasikini. 

“Kuanzishwa kwa zao hili wilayani Iringa ni fursa kubwa itakayousaidia Mkoa na watu wake kupambana na umasikini na kuongeza mapato yake.” Alisema Masenza.

Mkuu wa Mkoa wa Iringa aliwataka maafisa ugani na viongozi wa vijiji, kata na tarafa zinazolima zao hilo kutimiza wajibu wao ili kukifanya kilimo cha zao hicho kiwe chenye tija. 

Tunataka Mkoa ufanikiwe katika kilimo cha zao hili na ushauri wangu itungwe sheria ndogo itakayomlazimisha kila mkulima kushiriki katika kilimo hiki kinachotarajiwa pia kuchochea uanzishwaji wa viwanda vya kubangua korosho,” alisema mkuu wa Mkoa. 

Aidha, aliwataka viongozi wa vijiji kuwa mfano waa kuigwa katika kilimo cha korosho na uhamasishaji wake ili wananchi waweze kujifunza kupitia mashamba hayo.

Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesela alisema kuwa kilimo cha korosho kitampatia mwananchi matokeo ya uhakika kwa sababu bei yake ni nzuri. Alisema kuwa kwa taarifa za karibuni kilo moja ya korosho zilizobanguliwa inauzwa hadi shilingi 4,000.
=30=

WAKUU WA WILAYA WATAKIWA KUSIMAMIA ELIMU BILA MALIPO



Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za mitaa mkoani Iringa watakiwa kusimamia utekelezaji wa maagizo ya Rais ya utoaji wa elimu bila malipo mkoani hapa.

Kauli hiyo imetolewa na mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza alipokuwa akiongea na walimu wakuu na wakuu wa shule katika kikao maalum cha kujiridhisha na utekelezaji wa maagizo ya Rais juu ya elimu bila malipo kilichofanyika katika shule ya sekondari Lugalo leo.
Walimu wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Iringa (hayupo pichani)

Niwaagize wakuu wa Wilaya kama yapo mambo kama hayo yanaendelea katika Wilaya zenu na nyie hamjui na hamjaniambia nayie mtakuwa mnanihujimu. Sasa nisingependa tabia ya kuhujumiana ikawa sehemu ya utawala katika Mkoa wetu” alisema Masenza.

Aidha, aliwataka Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikalai za Mitaa kusimamia shule katika Halmashauri zao ili suala la uchangishaji michango kinyume na maelekezo usiwepo. 

Alisema kuwa kikao hicho ni kikao cha kujiridhisha kama kuna shule inayoendesha michango na inasimamiwa na mwalimu. Alisema kuwa mwisho wa kikao hicho kila mkuu wa shule awe ameandika barua kumueleza mkuu wa Mkoa juu ya hali ya jambo hilo.

Aidha, mkuu wa Mkoa aliagiza kuwa kwenye elimu bure hakuna michango, na kupiga marufuku kwa mwalimu yeyote kuchangisha mchango na kuwarudisha nyumbani wanafunzi kwa kisingizio cha michango. Aidha, alipiga marufuku wanafunzi wote wanaoripoti shuleni kurudishwa nyumbani kwa kutokuwa na sare.

Wakati huohuo, amezitaka shule binafsi kuacha mara moja kukaririsha vidato wanafunzi wasiofikia wastani na kwamba shule zitakazokiuka agizo hilo zitafutiwa usajili.
=30=

WAKUU WA SHULE NA WALIMU WAKUU WATAKIWA KUTHIBITISHA KWA BARUA MICHANGO INAYOENDELEA KATIKA SHULE ZAO



Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Iringa
MKUU wa Mkoa wa Iringa Amina Masenza amewataka wakuu wa shule za sekondari na msingi kuthibitisha kwa barua iwapo kuna michango yeyote inayoendelea katika shule zao kinyume na maelekezo ya serikali.

Agizo hilo amelitoa leo katika kikao cha dharura na wakuu wa shule na walimu wakuu kufuatia agizo la Rais w Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alilolitoa jana kuhusu michango katika shule nchini.
 
Walimu waliohudhuria kikao cha dharura cha Mkuu wa Mkoa wa Iringa

Serikali imekwisha elekeza kuwa tunakwenda na elimu bila malipo. Mtu yeyote nayekwenda kinyume na hilo anakwenda kinyume na maelekezo ya serikali. Ni Rais aliyetoa amri hii yeye ndiye mwenye usemi wa mwisho katika mambo yote ya Taifa hili. Yeyote anayekiuka hili atakuwa anafanya kwa dharau” alisema Masenza.

Alisema kuwa waraka wa elimu Namba 3 wa mwaka 2016 kuhusu utekelezaji wa elimu ya msingi bila malipo ulitoa maelekezo ya utekelezaji wa jambo hilo.

Alisema kuwa alikwisha kuwa iwapo kuna hitaji lolote katika shule, libainishwe na jamii na jamii yenyewe ndiyo isimamie utekelezaji wa jambo hilo nje ya utaratibu wa mwalimu mkuu na walimu wengine.

Nimewaita hapa nijiridhishe, nitamtaka kila mwalimu mkuu wa shule ya msingi na sekondari kwa mkono wake aandike barua kwa mkuu wa Mkoa kuthibitisha kwamba ama upo mchango unaoendelea katika shule yake ama hakuna. Barua zenu zote tutazipitia moja baada ya nyingine. Baada ya hapo tutakuwa na ukaguzi na kuongea na bodi na kamati za shule ili zitumbie kama wanayo michango, michango hiyo iliidhinishwa na nani, ni kiasi gani na kwa madhumuni gani?” alihoji mkuu wa Mkoa.

Aliongeza kuwa eneo lolote litakalobainika kuwa mwalimu mkuu ndiye kichocheo cha huo mchango na yeye ndiye anasimamia hafai na kwa tamko la Rais hana kazi.

Mkuu wa Mkoa aliwataka walimu hao kuacha kuchezea maagizo ya serikali. Aidha, alionesha kuwashangaa waratibu wa elimu ambao katika maeneo yao kuna michango inayoendelea na wao hawafahamu. Aidha, aliwaelekeza waratibu hao kuwepo katika vikao vya bodi na kamati za shule ili kufahamu hli ya mambo inavyokwenda.
=30=