Na
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Wananchi wilayani Iringa wametakiwa kuitumia vizuri
fursa ya kilimo cha zao la korosho ili kuweza kujiongezea kipato.
Kauli hiyo ilitolewa na mkuu wa mkoa wa Iringa, Amina
Masenza alipokuwa akizindua kilimo cha zao la korosho katika kijiji cha Idodi wilayani
Iringa jana.
Masenza aliwataka wananchi kutumia kilimo cha zao la
korosho kama fursa ya kuondokana na umasikini.
“Kuanzishwa kwa zao hili
wilayani Iringa ni fursa kubwa itakayousaidia Mkoa na watu wake kupambana na
umasikini na kuongeza mapato yake.” Alisema Masenza.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa aliwataka maafisa ugani na
viongozi wa vijiji, kata na tarafa zinazolima zao hilo kutimiza wajibu wao ili
kukifanya kilimo cha zao hicho kiwe chenye tija.
“Tunataka Mkoa ufanikiwe katika kilimo cha zao hili na ushauri wangu
itungwe sheria ndogo itakayomlazimisha kila mkulima kushiriki katika kilimo
hiki kinachotarajiwa pia kuchochea uanzishwaji wa viwanda vya kubangua korosho,”
alisema mkuu wa Mkoa.
Aidha, aliwataka viongozi wa vijiji kuwa mfano waa kuigwa
katika kilimo cha korosho na uhamasishaji wake ili wananchi waweze kujifunza
kupitia mashamba hayo.
Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesela alisema kuwa
kilimo cha korosho kitampatia mwananchi matokeo ya uhakika kwa sababu bei yake
ni nzuri. Alisema kuwa kwa taarifa za karibuni kilo moja ya korosho
zilizobanguliwa inauzwa hadi shilingi 4,000.
=30=
No comments:
Post a Comment