Mwenyekiti wa Kamati ya michezo ya Mkoa wa Iringa ameitaka timu ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa (Club ya RAS Iringa) kuhakikisha inafanya vizuri katika michuano ya shirikisko la michezo na wizara, mikoa, idara na wakala wa serikali kuu (SHIMIWI) na kurudi na kombe la ubingwa.
Mwenyekiti wa kamati ya michezo mkoa wa Iringa, Gertrude Mpaka (kushoto) akimkabidhi viatu vya michezo Mwenyekiti wa Club ya RAS Iringa Dr. Oscar Gabone tayari kwenda Tanga kushiriki mashindano ya SHIMIWI
Rai hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Michezo wa Mkoa wa Iringa, Gertrude Mpaka leo wakati akiiaga timu hiyo maarufu kama Ras Iringa inayojiwinda na michuano ya SHIMIWI inayotarajiwa kuanza kurindima jijini Tanga leo tarehe 5.11. 2011.
Mpaka amesema kuwa michezo ni furaha, upendo na afya hivyo ni jukumu lenu wanamichezo kuhakikisha michezo inatumika katika kudumisha furaha, upendo na afya.
Amesema hayo yakizingatiwa ni dhahiri kuwa timu hiyo itafanya vizuri na pamoja na kurudu na kombe la ushindi pia ameigaziza kurudi na ushindi wa nidhamu.
Akiongea kwa kujiamini, Mpaka ambaye pia ni Katibu Tawala Mkoa wa Iringa na aliyeanzia kazi katika Mkoa wa Tanga kwa nafasi hiyo aliyonayo kwa sasa amesema ninajivunia timu ya wanamichezo iliyojiandaa kiushindani na yenye wachezaji walioshiba vilivyo.
Amesema “SHIMIWI tunaenda kushindana pia kuadhimisha miaka 50 ya Uhuru chini ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo” na kuwataka wanamichezo kushindana huku wakitafakari mafanikio na changamoto zilizojitokeza katika miaka hiyo 50.
Awali akimkaribisha Mwenyekiti wa Michezo Mkoa wa Iringa, Mwenyekiti wa SHIMIWI Club ya RAS Iringa, Dk. Oscar Gabone amesema kuwa wanamichezo hao wameiva na kutokana na ari waliyonayo wanaona kama wanachelewa kuanza michuano hiyo ikiwa ni pamoja na kukabidhiwa ushindi wake.
Akitoa shukrani kwa niaba ya timu hiyo, Afisa Michezo katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kenneth Komba, amemshukuru Katibu Tawala Mkoa wa Iringa kwa utayari wake kuwasaidia wanamichezo na michezo kwa ujumla katika Mkoa wa Iringa. Paamoja na kuahidi kurudi na kombe pia alimhakikishia kuendelea kuwa wamoja.
Michezo hiyo inatarajiwa kufunguliwa na Waziri ,wenye dhamana ya michezo nchini, Dk. Emmanuel Nchimbi.