Saturday, November 5, 2011

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Jakaya Mrisho Kikwete ametoa salamu za Iddi El Hajji kwa watoto wa makao ya watoto ya Tosamaganga akiwatakia heri katika sherehe hiyo.

Salaam hizo zimetolewa na katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Gertrude Mpaka kwa niaba ya Rais, Dk. Kikwete katika kituo cha makao ya kulelea watoto ya Tosamaganga.
 Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Gertrude Mpaka (kulia) akikabidhi zawadi ya mbuzi kutoka kwa Rais Kikwete kwa kituo cha makao ya watoto cha Tosamaganga




 Baadhi ya watoto wqanaolelewa katika kituo cha makao ya watoto Tosamaganga


Gertrude amesema “nimekuja hapa kufanya mambo makubwa mawili: jambo la kwanza nimekuja kuwafikishia salamu za Iddi El Hajji kutoka kwa Mhe. Dk. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anawatakia heri na fanaka kwa iddi El Hajji”.

Gertrude amesema Mhe. Rais amefarijika sana kushiriki na watoto hao katika kusherehekea sikukuu hiyo ya Iddi El Hajji “alipenda kuwa nanyi hapa, lakini kutokana na majukumu kuwa mengi ametuma salamu za kuwatakia heri na fanaka kwa Iddi El Hajji”. Vilevile, amesema kuwa Mhe. Rais anawatakia watoto wote kusherehekea sikukuu ya Iddi El hajji kwa furaha, amani na kudumisha upendo.

Katibu Tawala Mkoa amelitaja jambo la pili kuwa ni zawadi alizotoa mhe. Rais. “ili muweze kusherehekea vizuri sikukuu hii, Mhe. Rais ametoa zawadi kwenu akiamini mtasherehekea pamoja nae kwa furaha”.

Zawadi alizotoa Rais Kikwete ni mchele kilo 150, mbuzi watatu na mafuta ya chakula lita 40 vyote vikiwa na thamani ya shilingi 555,000.

Akimkaribisha Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, Tinna Sekambo amesema Halmashauri yake inavituo vine vinavyotoa huduma ya kulea watoto na kusema kuwa kituo hiki cha Makao ya watoto Tosamaganga ndicho kikubwa na kuushukuru uongozi wa kitaifa kwa kuutambua mchango wa kituo hicho na kuweza kuungana nao katika malezi ya watoto.

Akitoa shukrani zake kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, msimamizi wa kituo hicho Sr Hellen Kihwele amesema “namshukuru sana Rais. Kikwete kwa kutukumbuka mara kwa mara hali inayoonesha upendo wake kwetu sote”.

Sr. Hellen ameyataja matarajio ya baadae ya kituo hicho kuwa ni kukamilisha jingo la shule ya chekechea ambalo halijamalizika kutokana na ukosefu wa fedha na kuiomba jamii iweze kusaidia kukamilisha ujenzi huo.

No comments:

Post a Comment